Sep 18, 2019 10:40 UTC
  • Ruwaza Njema (15)

Assalaam Aleikum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran, na karibuni kusikiliza sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Ruwaza Njema. Kipindi hiki kama mnavyojua huzungumzia Hadithi tofauti kutoka kwa watu wa Nyumba ya Mtume Mtukufu (saw) ambazo hutuongoza na kutuwezesha kuiga tabia njema za mtukufu huyo katika maisha yetu ya kila siku.

Leo tutazungumzia tabia yake nyingine njema ya kukinai na kufanya subira alipokosa chakula na wakati huohuo kuvutiwa sana na suala zima la kuwapa chakula watu wengine na kumshukuru Mwenyezi Mungu kutokana na neema zake nyingi anazowapa wanadamu. Kuweni nasi hadi mwisho wa kipindi, karibuni.

***********

Tunaanza wapenzi wasikilizaji kwa kunukuu Hadithi ifuatayo kutoka kwa Allama as-Sayyid Hashim al-Bahrani katika kitabu cha Hilyatul Abrar ambapo Imam Ja'ffar as-Swadiq (as) amenukuliwa akisema: 'Siku moja Mtume (saw) aliingia nyumbani kwa Ummu Salama (MA) naye akamkaribisha kwa mkate mkavu. Mtume (saw) akauliza, je, hakuna mchuzi? Umma Salama akamjibu: Hapana ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Sina chochote isipokuwa siki. Akasema Mtume (saw): Siki ni mchuzi mzuri ulioje! Bila shaka nyumba iliyo na siki si kuwa huwa haina kitu.' Imam Swadiq (as) pia amesema: 'Mchuzi uliompendeza zaidi Mtume (saw) ni siki na mafuta ya zeituni, na akasema (as): Hiki ni chakula cha Mitume (as).'

Na Sheikh as-Swadouq amenukuu katika kitabu cha Uyun Akhbar ar-Ridha (as) Hadithi ambayo imepokelewa kutoka kwa Imam Ali bini Abi Talib (as) kwamba alisema: 'Tulikuwa pamoja na Mtume (saw) tukichimba handaki (kabla ya Vita vya Khandaq) ambapo alifika hapo Bibi Fatwimah huku akiwa amebeba kipande cha mkate na kumpa Mtume (saw). Mtume (saw) akamuuliza, je, kipande hiki cha mkate ni nini? Fatwimah (as) akajibu: Ni sehemu ya mkate nilioupika kwa ajili ya Hassan na Hussein, ambao nimekuletea kipande chake. Mtume (saw) akasema: Hakika hiki ni chakula cha kwanza kuingia katika kinywa cha baba yako baada ya kupita siku tatu.' Na Imam Ali al-Murtadha (as) anasema katika Hadithi nyingine: 'Mtume (saw) aliletewa chakula, akasogeza kidole chake karibu na chakula hicho na kuhisi kuwa kilikuwa moto. Alisema: Acheni kipoe kwa sababu kina baraka nyingi zaidi katika hali hiyo. Hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu hatulishi moto.'

 

 

Tunaashiria hapa hii Hadithi nyingine ambapo Mtume (saw) ambaye ni mbora wa tabia kati ya viumbe wote alidhihirisha wazi sifa yake ya kuvutia ya kuwapa chakula wahitaji. Thiqatul Islam Ahmad al-Barqi (MA) anaashiria katika kitabu chake cha al-Mahasin akimnukuu Abdulrahman bin al-Hajjaj kwamba alisema: 'Tulikuwa kwa Imam Swadiq (as) ambapo chombo cha wali kililetwa nasi tukawa tunaomba radhi (hatutaki kula). Imam (as) akasema mnafanya mambo gani haya? Mtu anayetupenda zaidi ni yule anayekula vizuri zaidi kwetu. Abdurahman akasema: Nilifungua sehemu moja ya chakula na nikaanza kula. Akasema Imam (as): Ni vizuri sasa. Kisha akawa ananihadithia kwamba siku moja mtume Mtukufu (saw) aliletewa chombo kilichokuwa na wali kutoka kwa Answar na akawa amewaita Salman, Miqdad na Abu Dhar (MA). Walipofika waliomba radhi (hawakutaka kula). Mtume (saw) aliwauliza: Ni kwa nini mnafanya hivyo? Mtu anayetupenda zaidi ni yule anayekula vizuri zaidi chakula chetu. Hapo, wakaanza kula vizuri sana. Imam (as) akasema: Mwenyezi Mungu awarehemu, awaridhie na kuwatumia salamu.'

**********

Ndugu wasikilizaji, tunanukuu Hadithi zifuatazo kutoka juzuu ya sita ya kitabu cha al-Kafi ambazo zinazungumzia adabu ya kula.

Hadithi ya kwanza inasema: 'Mtume (saw) alipokuwa akiwekewa chakula mbele yake alikuwa akisema: 'Umetukuka ewe Mwenyezi Mungu! Neema zako ni za kuvutia kiasi gani kwetu! Umetukuka! Ni mengi kiasi gani unayotupa! Umetukuka! Huruma yako kwetu ni kubwa kiasi gani! Ewe Mwenyezi Mungu! Tuzidishie riziki, pamoja na masikini wote waumini wa kiume na wa kike na Waislamu wa kiume na wa kike.'

Dua hii ya Bwana Mtume ni ya kuvutia kisasi gani! Hii ni kwa sababu inajumuisha kuhimidi na kumshukuru Mwenyezi Mungu na kumwomba baraka na neema zake. Ilikuwa ni kawaida ya Mtume (saw) baada ya kumaliza kula chakula kwa watu fulani, kuwashukuru na kuwaombea dua pia. Thiqatul Islam al-Kuleini amemnukuu Imam Ja'ffar (as) akisema: 'Mtume (saw) alipomaliza kula chakula kwa watu fulani, aliwaambia: 'Waliofunga wapate kula kwenu, wakule kwenu watu wema na wakuswalieni Malaika wateule.'

 

Tunanukuu hapa Hadithi ya tatu ambayo inatufundisha na kutushauri tufanye nini tunapomaliza kula chakula, Hadithi ambayo imepokelewa kutoka kwa Imam wetu anayefanana sana na Mtume Mtukufu (saw) al Imam Ja'ffar as-Swadiq (as) anayesema: 'Meza ya chakula ilipoondolewa Mtume (saw) alikuwa akisema: Allahumma! Umetupa kwa wingi neema zako, kutusafishia (kututakasia neema hizo) na kutubariki kwazo; umetushibisha na kutunywesha. Hamdu na shukurani zote ni za Mwenyezi Mungu ambaye analisha hali ya kuwa Yeye mwenyewe hana haja ya kula.'

Na hii ndiyo njia bora zaidi ya kumshukuru Mwenyezi Mungu baada ya kumaliza kula. Mtume mwenyewe, ambaye ni mwongozaji mkuu na mbora wa viumbe wote  (saw) ametubashiria kwamba hii ndio njia bora zaidi ya kumshukuru Mwenyezi Mungu na kwamba ni moja ya sababu zinazompelekea mwanadamu aweze kufanikiwa kusamehewa dhambi zake na Mwenyezi Mungu. Thiqatul Islam al-Kuleini amenukuu Hadithi kutoka kwa Imam Swadiq (as) kwamba alisema: 'Kila mtu anayeikusanya pamoja familia yake na kuweka kati yao chakula na kisha yeye na familia yake hiyo kutamka, 'Bismillahi' kabla ya kula na kumshukuru Mwenyezi Mungu baada ya kumaliza kula, Mwenyezi Mungu huwaghufiria.'

Tunahitimisha kipindi hiki wapenzi wasikilizaji kwa kutaja Hadithi tukufu ifuatayo ambayo ni miongoni mwa hamdu na shukrani kwa Mwenyezi Mungu, nayo ni ya kumswalia Mtume wake (saw) ambaye Mungu Muumba alitupa neema na fadhila kubwa kupitia kwake. Imepokelewa katika kitabu cha al-Kafi kupitia Ibn Bakir kwamba alisema: 'Tulikuwa kwa Aba Abdillahi as-Swadiq (as), tukakula na kisha tukanyanyua juu mikono yatu na kusema: Alhamdulillah. Aba Abdillah (as) akasema: 'Allahuma! Hii (hiki chakula/riziki) ni kutoka kwako na kutoka kwa Muhammad, Mtume wako. Allahumma! Hamdu zote ni zako, mswalie Muhammad na Aali za Muhammad.'

Na suala hili linasisitizwa na kuzungumziwa kwa njia ya kuvutia sana katika sehemu ya Aya ya 74 ya Surat Baraa au at-Tauba kwa kusema: Ila kuwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake amewatajirisha kutokana na fadhila zake.

**********

Na kufikia hapa wapenzi wasikilizaji, ndio tunafikia mwisho wa kipindi hiki cha Ruwaza Njema mlichokitegea sikio kutoka Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Basi hadi tutakapokutana tena juma lijalo panapo majaliwa, tunakuageni nyote kwa kusema Wassalaam Aleikum Warahmatullahi Wabarakatuh.

 

Tags