Sep 18, 2019 11:18 UTC
  • Ruwaza Njema (18)

Hamjambo wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikikutangazieni kutoka mjini Tehran. Ni matumaini yetu kuwa mko tayari kabisa kutegea sikio sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Ruwaza Njema ambacho huchambua Hadithi na Riwaya tofauti kuhusiana na tabia njema na ya kupigiwa mfano ya Mtume wetu Mtukufu Muhammad (saw).

Baada ya kuzipitia Hadithi hizo tunachotakiwa kufanya sisi Waislamu ni kuiga mfano wa maisha ya mtukufu huyo kama tunavyoamrishwa kufanya na Qur'ani Tukufu. Leo tutachambua baadhi ya Hadithi zinazozungumzia ibada ya Mtume Muhammad (saw) ya kuhudumia waja na viumbe wa Mwenyezi Mungu kwa kuwafanyia mambo ya heri na kuwaongoza kwenye njia nyoofu inayowadhaminia wongofu na saada ya humu duniani na huko Akhera. ThiqatuL Islam al-Kuleini amenukuu katika kitabu chake cha aL-Kafi Hadithi ya kuaminika kutoka kwa Muhammad bin Muslim akisema: 'Siku moja nilienda kwa Abu Ja'ffar (Imam Baqir) (as) nikampata akiwa anakula naye akanikaribisha nikule pamoja naye. Alipomaliza kula alisema: Ewe Muhammad! Unadhani tokea alipobaathiwa na Mwenyezi Mungu hadi alipoaga dunia, Mtume (saw) aliwahi kula chakula hali ya kuwa ameegemea kitu? Imam mwenyewe alijibu swali hlo kwa kusema: La Wallahi! Sikuwahi kumwona Mtume akila chakula huku akiwa ameegemea kitu tokea alipobaathiwa na Mwenyezi Mungu hadi alipomfisha. Kisha alisema (as): Ewe Muhammad! Je, unadhani kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu tokea alipobaathiwa na Mwenyezi Mungu hadi alipoaga dunia, aliwahi kula mkate wa shayiri hadi akashiba kwa siku tatu mfululizo? Imam mwenyewe (as) alijibu kwa kusema: Hapana Wallahi! Hakuwahi kula mkate wa shayiri hadi akashiba kwa siku tatu mfululizo, tokea alipobaathiwa na Mwenyezi Mungu hadi alipoaga dunia. Sisemi kuwa hakuwa akipata mkate (chakula) wa kutosha wa kuweza kumshibisha, la hasha! Tazama! Baadhi ya wakati mtukufu huyo alikuwa akimzawadia mtu mmoja ngamia mia moja. Hivyo, kama angelitaka angeweza kula hadi ashibe.'

 

Ndugu wasikilizaji, Imam Baqir (as) anasema kwamba uzuri na mvuto wa kumwabudu Mwenyezi Mungu na kupenda kuwahudumia na kuwafikishia heri waja wake ndio iliompelekea Mtume (saw) akatae kujichukulia funguo za hazina (utajiri) ya ardhi. Imam (as) anasema: 'Jibril alimkabidhi Mtume (saw) mara tatu, funguo za hazina ya ardhi, huku akimhakikishia kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu hangempunguzia chochote katika yale aliyomuandilia Siku ya Kiama, lakini alikataa kuzichukua na kuamua kumyenyekea Mola wake Mtukufu. Kisha Imam Baqir akasema: Wala hakuombwa kitu na kusema; sina; bali alipeana kama alikuwa nacho na kama hakuwa nacho alisema: Itakuwa (kitapatikana) Inshaallah.'

**********

Na mpokezi wa Hadithi hii, Muhammad bin Muslim anasema: 'Kisha Imam (as) alinipa chakula kwa mkono wake mwenyewe na kusema: Kiongozi wenu alikuwa akiketi kama wanavyoketi watumwa, akila kama wao, akiwalisha watu mkate wa ngano na nyama na yeye mwenyewe kurudi nyumbani na kula mkate wa shayiri na mafuta ya zeituni. Aliponunua nguo (kanzu) mbili za Sumbulani (vazi linalonasibishwa na mji mmoja wa Roma) alikuwa akimwambia mfanyakazi wake achukue iliyo bora zaidi kati ya mbili hizo naye kuvaa iliyobaki. Ilipokuwa ndefu zaidi kuliko vidole vya mkononi alikuwa akikata sehemu iliyozidi na vilevile ilipozidi kifundo cha mguu. Alipokabiliwa na mambo mawili ambayo yote mawili yanamridhisha Mwenyezi Mungu, alichagua lile lililokuwa gumu zaidi kwa mwili wake. Aliwaongoza watu kwa miaka mitano lakini hakuwahi kujilimbikizia mali hata kidogo wala kupeana ardhi (mali ya umma) kwa mtu yoyote yule. Hakuacha urithi wowote katika dirhamu wala dinari ila dirhamu mia saba zilizozidi katika mali yake ambazo alitaka familia yake inunuliwe (huduma za) mfanyakazi (wa nyumbani). Hakuna mtu aliyekuwa na uwezo wa kufanya aliyoyafanya yeye. Ali bin Hussein (as) alikuwa akipitia vitabu vyake (maandish yake Ali (as)) na kisha kuviweka ardhini huku akisema: Ni nani aliye na uwezo wa kuyatekeleza haya?!'

*********

Ndugu wasikilizaji, Thiqatul Islam, as-Sheikh al-Kuleini katika juzuu ya nane ya kitabu chake cha Alkafi ananukuu Hadithi kutoka kwa Imam Swadiq (as) kwamba alisema: 'Katika vita vya Dhatu ar-Riqaa' Mtume (saw) alifiki chini ya mti mmoja uliokuwa kwenye bonde. Alipokuwa hapo, mafuriko yalitokea na kumtenganisha yeye na masahaba zake. Mtu mmoja kati ya mushrikina alimwona Mtume (saw) akiwa katika hali hiyo na Waislamu nao walikuwa upande wa pili wa bonde wakisubiri mafuriko yakatike. Mushrik huyo akiwa na wenzake alisema: Mimi nitamuua Muhammad! Akamkaribia Mtume (saw) na kumyanyulia upanga huku akisema: Ewe Muhammad! Sasa ni nani atakayekunusuru kutoka kwenye makucha yangu?! Mtume akamjibu: Ni Mungu wangu na Mungu wako! Hapo Ghafla Malaika Jibril akamuangusha kichalichali mushrik huyo kutoka juu ya farasa wake. Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) akasimama na kuchukua upanga wake, akaketi kwenye kifua chake na kumuuliza: Ni nani atakayekuokoa mbele yangu, ewe Ghaurath? Akasema: Ni msamaha na ukarimu wako ewe Muhammad! Mtume akaachana naye, naye (huyo mushrik) akawa ameamka huku akisema: Ninaapa kwa jina la Mwenyezi Mungu, wewe ni mbora na mwenye ukarimu zaidi kuniliko mimi.'

Hakika nyinyi mnayo ruwaza njema kwa Mtume wa Allah kwa anayemtaraji Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, na akamkumbuka Allah sana.

 

Mnaona hapa wapenzi wasikilizaji upeo wa mapenzi na huruma ya kimaumbile aliyokuwa nayo Mtume Mtukufu (saw), jambo ambalo lilidhihiri wazi kutoka kinywani mwa mushrik yule alipomuhutubu Mtume (saw) kwa kusema: 'Ninaapa kwa jina la Mwenyezi Mungu, wewe ni mbora na mwenye ukarimu zaidi kuniliko mimi.' Mapenzi na upendo huo bila shaka ulimwondoa mushrik huyo kutoka kwenye kina cha giza na kumuingiza kwenye nuru ya Tauhidi.

Imepokelewa katika kitabu cha al-Kafi kutoka kwa Imam Swadiq (as) akihadithia kisa kimoja kutoka kwa Imam Ali (as) kwamba: 'Siku moja Imam Ali (as) aliandamana na 'dhimmi' mmoja (mtu asiyekuwa Mwislamu anayeishi chini ya himaya ya dola la Kiislamu) naye huyo dhimmi akamuuliza Imam: Unaelekea wapi ewe mja wa Mwenyezi Mungu?! Imam (as) akamjibu: Ninaelekea Kufa. Walipofika kwenye makutano ya njia, dhimmi yule akawa amechukua njia tofauti naye Imam akawa anamfuata. Dhimmi akamwambia: umeacha njia ya kwenda Kufa! Imam (as) akamjibu: Ninafahamu hilo. Dhimmi akasema: Basi mbona licha ya kuwa unalifahamu vyema hilo, bado unanifuata? Imam (as) akamjibu: Hili linatokana na ukamilifu wa urafiki ambapo mtu aliyeandamana na mwenzake safarini anatakiwa kumuaga kwa kutembea naye hatua kadhaa kuelekea anakokwenda, njia zinapotengana. Mtume wetu (saw) ametufundisha hivi. Dhimmi akauliza: Alikwambieni hivyo? Imam (as) akajibu: Ndio. Dhimmi akasema: Ni wazi kuwa kila mtu anayemfuata mtukufu huyo amefanya hivyo kutokana na matendo yake mema. Ninashuhudia kwamba mimi pia niko katika dini yako. Dhimmi huyo alirejea na Imam Ali (as) mjini Kufa na kusilimu baada ya kuwa amemtambua na kumjua vyema.'

*************

Na kufikia hapa wapenzi wasikilizaji ndio tunafikia mwisho wa kipindi hiki cha Ruwaza Njema kilichokujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikikutangazieni kutoka mjini Tehran. Ni furaha yetu kuwa mmekuwa nasi hadi mwisho wa kipindi huku tukitumai kuwa mmenufaika vya kutosha na yake mliyoyasikia katika kipindi hiki. Basi hadi tutakapokutana tena juma lijalo panapo majaaliwa, tunakuageni nyote kwa kusema, Wassalaama Aleikum Warahmatullahi Wabarakatuh.

 

 

Tags