Nov 18, 2019 07:28 UTC
  • SPOTI, NOV 18

Ufuatao ni mkusanyiko wa baadhi ya matukio muhimu ya michezo yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita kitaifa na kimataifa....

Iran yatwaa tena Taji la Kabaddi

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeibuka mshindi wa Duru ya Kwanza Mashindano ya Vijana ya Kabaddi yaliyofanyika katika mji wa pwani wa Kish kusini mwa Iran. Timu hiyo ya Iran imeibuka kidedea na kutunukiwa medali ya dhahabu baada ya kuizidi maarifa Kenya katika mchezo wa fainali uliopigwa Ijumaa. Vijana hao wa Iran waliwashinda mahasimu wao wa Kenya kwa alama 44-22 na kulibakisha taji hilo nyumbani. Kenya imetwaa medali ya fedha, huku washindi wa tatu Pakistan na Bangladesh wakizawadiwa shaba kwa pamoja. Wachezaji wa Kenya wamefurahia kuibuka katika nafasi ya pili, wakisisitiza kuwa kujituma na bidii yao ya mchwa ndiyo imewafikisha walikofika.

Timu ya mchezo wa kabadi ya Iran

 

Timu hiyo ya vijana ya mchezo wa kabaddi ya Iran ilitinga fainali ya mashindano hayo baada ya kuzichambua kama karanga Thailand, Turkmenistan, na Malaysia katika mechi za makundi kabla ya kuzilaza China Taipei na Bangladesh katika michuano ya robofainali na nusufainali kwa usanjari huo.  India ambayo ni muasisi wa mchezo huu haikushiriki mashindano hayo ya dunia ya vijana, yaliyoanza Novemba 11 hadi 15.

FIFA yaipiga faini Bahrain kwa kuvunjia heshima wimbo wa taifa wa Iran

Shirikisho la Soka Duniani FIFA limeipiga Bahrain faini ya franca 20,000 za Uswisi kwa kuuvunjia heshima wimbo wa taifa wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, wakati wa mechi kati ya timu hiyo na Iran mwezi uliopita. Taarifa iliyotolewa Ijumaa na Kamati ya Nidhamu ya FIFA imesema kuwa, "Bahrain imetozwa faini ya franca 20,000 za Uswisi kwa kukiuka nidhamu na usalama wakati wa mechi, na pia kwa ajili ya utovu wa nidhamu wa wachezaji na maafisa wa timu." Masoud Soltanifar, Waziri wa Michezo na Vijana wa Iran iliwasilisha malalamishi rasmi ya Jamhuri ya Kiislamu kwa Shirikisho la Soka Duniani FIFA kutokana na mienendo na miamala mibaya ya wachezaji na mashabiki wa Bahrain pamoja na maafisa wao dhidi ya wachezaji wa Iran wakati wa mchuano baina ya timu mbili hizo uliopigwa Oktoba 15.

Nembo za Bahrain na FIFA

 

Mashabiki hao wa Bahrain walifanya kioja cha kupiga kelele na kuudhihaki wimbo wa taifa wa Iran wakati wa mchuano huo wa mzunguko wa pili wa kusaka tiketi ya kushiriki fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika nchini Qatar mwaka 2022. Iran ilikubali kichapo cha bao 1-0 katika mchezo huo wa Kundi C uliopigwa katika Uwanja wa Riffa nchini Bahrain. FIFA pia imewakosoa pia wachezaji wa Iran kwa kukataa kuwapa mkono wachezaji wa Bahrain baada ya mchuano huo.

Soka Afrika; Tiketi za AFCON

Timu ya taifa ya soka ya Tanzania Taifa Stars imeanza vyema kwenye mbio za kusaka tiketi ya kushiriki michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2021. Hii ni baada ya kuisasambua Equatorial Guinea mabao 2-1 kwenye mchezo uliochezwa wikendi katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Stars iliyo chini ya mkufunzi Etienne Ndayiragije iliyoanza kwa kasi kipindi cha kwanza haikuweza kutumia vema nafasi saba za kipindi cha kwanza na kuruhusu wapinzani wao Equatorial Guinea kuandika bao la kwanza dakika ya 15 kupitia kwa Pedro Obiang akimtungua kipa mkongwe wa Tanzania, Juma Kaseja kwa shuti la mbali. Dakika tano baada ya kuanza kipindi cha pili, kocha huyo Mrundi wa Tanzania, Etienne Ndayiragijje alianza na mabadiliko ya kuongeza nguvu katika safu ys ushambuliaji, akimtoa beki wa kulia Hassan Ramadhani Kessy na kumuingiza mshambuliaji, Ditram Nchimbi. Ni mabadiliko hayo yaliyoisaidia Taifa Stars kupata bao la kusawazisha lililofungwa na kiungo mshambuliaji wa Difaa Hassan El-Jadidi ya Morocco, Simon Msuva dakika ya 68 akimalizia mpira uliookolewa na kipa baada ya yeye mwenyewe kuunganisha kwa kichwa kona ya beki wa kushoto, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’. Taifa Stars iliongeza kasi ya mashambulizi baada ya bao hilo na juhudi zao zilizaa matunda dakika ya 90 baada ya kiungo wa Azam FC, Salum Abubakar Junior ‘Sure Boy’ kufunga bao la ushindi kwa shuti la mbali.

Kombe la AFCON

 

Baada ya ushindi huo, Taifa Stars wamesafiri kuwafuata Libya katika Uwanja wa Taifa wa Tunisia. Mchezo huo wa pili utakaopigwa Jumanne ya Novemba 19 utachezewa Tunisia kutokana na ukosefu wa usalama Libya. Siku ya Jumapili, Uganda Cranes iliishushia kichapo cha mbwa Malawi na kuizaba mabao 2-0. Cranes walipata ushindi huo muhimu katika mechi ya Kundi B kwa kuwa walikuwa wanausakata nyumbani katika Uwanja Taifa wa Namboole, na bila shaka mcheza kwao hutuzwa. Mabao ya Uganda yalifungwa na Emmanuel Okwii and Fahad Bayo. Kocha Mkuu wa Uganda Cranes amewapongeza mahasimu kwa kucheza kwa kasi katika kipindi chote cha mchezo licha ya kuwa ugenini.

Huku hayo ya kiarifiwa, timu ya taifa ya soka ya Kenya, Harambee Stars iliambulia sare ya bao 1-1 ilipoocheza na Mafarao wa Misri, kwenye mechi yao ya kufuzu michuano ya AFCON 2021 iliyogaragazwa Alhamisi, Novemba 14 katika uga wa Burj El Alarb. Michael Olunga, anayecheza soka ya kulipwa nchini Japan alifunga bao la kusawazisha dakika ya 67 ya mchezo huo, baada ya Mahmoud Kahraba kuifungia Misri bao laa ina yake katika kipindi cha kwanza. Harambee Stars ambayo ipo kundi G pamoja na Visiwa vya Comoro na Togo; ina kibarua cha ziada Jumatatu, Novemba 18 jijini Nairobi.

Wakati huohuo, Senegal na Nigeria zilikuwa kati ya timu zilizoanza kampeni ya kufuzu kushiriki Kombe la Afrika (Afcon) mwaka 2021 kwa kishindo. Licha ya nyota wa klabu ya Liverpool, Sadio Mane kubanwa vilivyo dhidi ya Congo Brazzaville, Teranga Lions ya Senegal ilitumia uwanja wake wa nyumbani wa Lat Dior mjini Thies kuponyoka na ushindi wa mabao 2-0 katika mechi ya Kundi I. Katika mechi ya Senegal, wachezaji Sidy Sarr na Habibou Diallo, ambao wanasakata soka ya malipo nchini Ufaransa, walifunga mabao hayo muhimu dakika ya 26 na 28. Nigeria, ambayo ilizoa nishani ya shaba kwenye Afcon nchini Misri mwezi Julai mwaka jana, ilitoka nyuma bao moja na kulipua majirani Benin mabao 2-1 mjini Uyo, katika mechi hiyo ya Kundi L. Wenyeji Cameroon hawakufungana na wageni Cape Verde, huku Lesotho wakilazimisha sare ya bao 1-1 dhidi ya Sierra Leone, jijini Freetown. Jamhuri ya Afrika ya Kati nayo iliifunga Burundi mabao 2-0 katika mechi ya Kundi E. Burkina Faso iliisasambua Sudan Kusini mabao 2-1 katika mechi yao ya Kundi B iliyopigwa siku ya Jumapili. Siku ya Alkhamisi, Rwanda walianza kampeni hizi kwa mguu wa kushoto, baada ya kukubali kichapo cha mabao 2-0 walipovaana na Msumbiji mjini Maputo katika mechi ya Kundi E, kabla ya kutoana jasho na Cameroon Jumapili. Zimwi la mkosi liliendelea kuwaandama vijana wa Amavubi, kwani walijikuta wakikubali kulimwa bao 1-0 katika mchuano huo wa Jumapili.

CECAFA: Tanzania yaidhalilisha Sudan Kusini

Timu ya taifa ya soka ya wanawake ya Tanzania Bara au Kilimanjaro Queens imeanza vyema  michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA Challenge). Hii ni baada ya ushindi mnono wa mabao 9-0 dhidi ya Sudan Kusini katika mchezo uliopigwa katika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi mjini Dar es Salaam. Kila mchezaji wa Kilimanjaro Queens, mabingwa mara mbili mfululizo wa michuano hiyo aling’ara siku hiyo nyumbani, lakini nyota wa mchezo huo wa Kundi A alionekana kuwa Mwanahamisi Omar Shaluwa ‘Gaucho’ ambaye alifunga mabao matatu ya hatrick. Kilimanjaro Queens inasaka taji la tatu mfululizo la mashindano ya Afrika Mashariki na Kati kwa upande wa wanawake ikiwa imefanya hivyo mara mbili pindi yalipofanyika Burundi na Uganda. Kocha mkuu wa Kilimanjaro Queens Bakari Shime, amesema anataka kuweka historia nyumbani ya kubaki na kombe katika michuano ya CECAFA kwa upande wa wanawake.

Mashirikisho ya soka ya nchi wanachama wa CECAFA

 

Katika mchezo uliotangulia wa Kundi A, Burundi iliifanyia mauaji ya kimbari Zanzibar kwa kuigaragaza mabao 5-0. Harambee Starlets ya Kenya siku ya Jumapili ilishuka dimbani kuvaana na Ethiopia katika Uwanja wa Chamanzi jijini Dar es Salaam. Kenya ambayo ipo Kundi B pamoja na Uganda na Djibouti, iliwasasambua Wahabeshi mabao 2 bila jibu katika mchuano huo. Mabao ya Starlets wa Kenya yalifungwa na Jentrix Shikangwa na Cynthia Shilwatso, huku Kocha Mkuu wa timu hiyo, David Ouma akisema ana imani wataenda mbali zaidi.

Mashindano hayo ya kikanda kwa upande wa wanawake yanatazamiwa kuendelea kwa muda wa siku 10.

…………………….TAMATI……………..