Nov 25, 2019 08:06 UTC
  • Kongamano la Saba la Kimataifa la Robotiki na Mekatroniki lafanyika Iran

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika makala hii ya 102 ambayo huangazia baadhi ya matukio muhimu kuhusu sayansi na teknolojia nchini Iran na maeneo mengine duniani. Ni matumaini yangu kuwa utaweza kunufaika.

Watafiti 12 Wairani wametambuliwa katika Orodha ya Watafiti Waliotajwa Kwa Wingi mwaka 2019 ambayo imetayarishwa na shirika la Clarivate Analytics.

Taasisi ya Web Science Group ambayo inamilikiwa na Clarivate Analytics, mnamo Novemba 19 ilitangaza orodha yake ya kila mwaka ya Watafiti Waliotajwa Kwa Wingi. Orodha hii huwatambua watafiti wenye ushawishi mkubwa duniani na ambao kazi zao hutajwa na watafiti wenzao. Watafiti wa Iran waliotajwa wamehusika katika utafiti wa kilimo, hisabati na uhandisi. Kwa ujumla asilimia 3 ya orodha hiyo inajumuisha watafiti kutoka nchi za Kiislamu ambazo mbali na Iran ni Saudi Arabia, Malaysia na Uturuki.

Hivi karibuni pia, orodha ya vyuo vikuu bora zaidi duniani ya Times Higher Education imebaini kuwa vyuo vikuu 40 vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kati ya vyuo vikuu bora zaidi duniani.

Taasisi ya Elimu ya Juu ya Times Higher Education katika ripoti yake ya mwaka 2019 imeorodhesha vyuo vikuu 40 ambavyo ni kati ya vyuo vikuu bora duniani mwaka huu.

@@@

Makamu wa Rais wa Iran anayeshughulikia masuala ya sayansi na teknolojia amesema Iran inapaswa kuacha kutegemea pato la uuzaji mafuta ghafi ya petroli na badala yake ijiimarishe katika shughuli za kiuchumi ambazo msingi wke ni teknolojia. Akizungumza Novemba 23 katika mkoa wa Mazandaran kaskazini mwa Iran, Sattari amesema nchi zenye kutegemea pato la mafuta zinadorora katika ustawi kutokana na kushuka bei ya mafuta ghafi ya petroli duniani. Kwa msingi huo amesema Iran inapaswa kuacha kutegemea pato la mafuta huku akibaini kuwa, hivi sasa hakuna nchi inayoenda kwa nchi zinazozalisha mafuta kwa wingi duniani kutafuta teknolojia.

Katika upande mwingine, Kongamano la Saba la Kimataifa la Robotiki na Mekatroniki lilifanyika katika mji mkuu wa Iran, Tehran kuanzia Novemba 20 hadi 21 katika Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Shariff. Kongamano hilo liliandaliwa na Jumuiya ya Robotiki ya Iran kwa ushirikiano na jumuiya zinginezo za kisayansi nchini. Kongamano hilo liliwaleta pamoja wanasayansi na watafiti katika nyuga mbali mbali za robotiki na mekatroniki. Watafiti walijadili masuala kama vile mapinduzi katika uga wa roboti, maendeleo katika uga wa magari yasiyo na madereva, na vifaa vya kitiba vyenye muundo wa roboti vinavyoweza kuvaliwa na wagonjwa.

@@@

Kufuatia azma ya mataifa mengi kutaka kutumia mbinu ya teknolojia ya mionzi au radiation ili kuondoa uwezo wa mbu kuzaliana na hivyo kudhibiti magonjwa kama vile dengue, chikungunya na zika,  mashirika ya Umoja wa Mataifa yameanda mwongozo mpya kwa ushirikiano na wadau wengine ili kuhakikisha kuwa mbinu hiyo inatakelezwa kwa njia salama na kwa ufanisi.

Taarifa ya Shirika la Afya Duniani, WHO, iliyotolewa Novemba 14 huko Geneva, Uswisi inasema kuwa mbinu hiyo inayojulikana kwa kiingereza kama Sterile Insect Technique, kwa kifupi, SIT, ni aina ya njia za uzazi wa mpango kwa wadudu  ambapo mchakato wake unahusisha kuwafuga katika eneo maalumu mbu dume kisha kuwapiga mionzi ya kuondoa uwezo wa kuzalisha mayai na halafu wanaaachiliwa porini ili wakutane na mbu jike. Na kwa kuwa hawana uwezo wa kuzaa, idadi ya wadudu hao baada ya muda hupungua.

Mradi maalumu wa utafiti na mafunzo kwa magonjwa ya kitropiki, TDR na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki, IAEA kwa ushirikiano na Shirika la Chakula na Kilimo Duniani, FAO na WHO wameandaa mwongozo huo kwa mataifa ambayo sasa yanataka kutumia mbinu ya kufanya tasa madume ya mbu aina ya Aedes wanaosababisha ugonjwa wa Zika, Chikungunya na Dengue.

Wakati mwongozo huu unaandaliwa, Dkt. Soumya Swaminathan ambaye ni mwanasayansi mkuu wa WHO amesema kuwa, “nusu ya wakazi wa dunia wako hatarini kuambukizwa ugonjwa wa dengue na licha ya harakati zote bora zilizofanyika, na juhudi za sasa za kudhibiti bado hazijakuwa na mafanikio. Amesema kuna haja ya kuwa na mbinu mpya na hivyo mpango huu mpya wenye kutegemea teknolojia ya mionzi unatia matumaini.

WHO inasema kuwa katika miongo ya hivi karibu, visa vya homa ya dengue vimeongezeka kwa kiasi kikubwa kutokana na mabadiliko ya kimazingira, ukosefu wa usimamizi bora wa miji, na ukosefu wa mbinu toshelezi na endelevu za usimamizi wa kuenea kwa wadudu.

Hivi sasa milipuko ya dengue inatokea katika maeneo mengi, hususan bara la Asia ambako Bangladesh ndio inaoongoza zaidi kwa kuwa na mlipuko mbaya zaidi wa dengue tangu iripoti ugonjwa huo mwaka 2000. Aidha eneo la mwambao wa  Afrika Mashariki nalo pia limeathiriwa vibaya na ugonjwa wa dengue hivyo mbinu hii mpya ya teknolojia inatazamiwa kuleta matumaini katika eneo hilo.

@@@@

Shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa,  UNEP, limesema taka za kielektroniki ni mbaya na hatari kwani haziyeyuki na zinachafua mazingira. Hata hivyo hivi sasa baadhi ya vijana katika nchi mbalimbali ikiwemo Nigeria wameamua kuwa wabunifu na kugeuza taka hizo kuwa mali.

Katikati ya jiji la Lagos mji mkuu wa Nigeria taka za elektoniki kwa miaka zimekuwa shida kubwa lakini sasa zinageuzwa kuwa thamani kwa kutumia mchakato mbadala wa kiuchumi.

Lengo la mchakato huo ni kulinda mazingira na kutoa ajira salama kwa maelfu ya Wanigeria na hasa vijana. Kwa mujibu wa UNEP kila mwaka Nigeria huzalisha tani 290,000 za taka za elektroniki pamoja na kupokea zaidi ya tani 70,000 za vifaa vilivyotumika kwa elektroniki kutoka katika mataifa yaliyoendelea.

Lakini sasa vifaa hivyo vya elektroniki vikifikia mwisho wa matumizi yake na kutupwa vinakusanywa na vijana kutoka sekta isiyo rasmi na vifaa ambavyo bado vinaweza kutumika husafishwa na kuuzwa tena na visivyofaa huharibiwa au kuchomwa katika maeneo maalum ya kutupa taka hizo na kuwapatia kipato vijana hao. Hata hivyo wataalamu wa afya wanaonya kwamba kemikali za sumu zilizo katika taka za elektroniki husababisha madhara ya ngozi, matatizo ya kupumua, kupunguza maisha ya wanaoziharibu, kuchafua hewa, maji na udongo.

 

Katika kuepukana na yote haya UNEP inasema sasa Nigeria inaboresha sheria ya uwajibikaji kwa watengenezaji ili kuhakikisha wanawajibika na bidhaa wanazozalisha kwa muda wote wa mzunguko wa maisha ya bidhaa hizo.

Kwa mantiki hiyo sekta salama na yenye ufanisi ya matumizi mbadala ina fursa kubwa kwa uchumi wa Nigeria, kwani vifaa hivyo vya elektoniki vilivyoharibika vina vitu vyenye thamani kubwa ndani yake kama dhahabu, madini ya platinum na vitu vingine adimu vya thamani.  Sekta hiyo ya kushughgulika na taka za elektroniki sasa inatoa ajira kwa watu zaidi ya 100,000 Nigeria.

@@@

Naam wapenzi wasikilizaji na hadi hapo ndio tunafika mwisho wa makala yetu ya sayansi na teknolojia. Ni matumaini yangu kuwa umeweza kunufaika na niliyokuandalia.

 

Tags