SPOTI JAN 20
Ulimwengu wa Michezo, Jan 20
Matukio muhimu ya spoti ndani ya siku saba zilizopita......
Iran yaikosoa AFC kwa kuingiza siasa kwenye michezo
Timu za Esteqhlal, Perspolis, Sepahan na Shahre-Khodroo zinazoiwakilisha Iran katika mashindano ya Mabingwa wa Soka wa Asia katika mwaka huu wa 2020 zimeamua kujitoa kwenye mashindano hayo kulalamikia uamuzi wa kisiasa uliochukuliwa na Shirikisho la Soka la Asia (AFC) wa kuzitaka timu hizo zicheze michezo yao yote katika nchi ya tatu. Timu hizo zimetangaza uamuzi huo Jumamosi na kusisitiza katika taarifa yao kwamba: Hazitatii uamuzi huo wa kiuonevu uliochanganyika na matashi ya kipropaganda dhidi ya hali ya usalama ya Iran. Katika barua kwa Shirikisho la Soka la Iran, Shirikisho la Soka la Asia limetangaza kuwa, kamati ya utendaji ya shirikisho hilo inakusudia kuandaa mechi za timu za Iran na washindani wao katika nchi isiyoelemea upande wowote. Kisingizio kilichotumiwa na Shirikisho la Soka la Asia kuchukua uamuzi huo wa kiafriti ni kutokuwepo amani na usalama nchini Iran. Waziri wa Michezo na Vijana wa Iran, Masoud Soltanifar ametetea uamuzi wa klabu hizo akisisitiza kuwa, zimechukua hatua hiyo kwa lengo la kupigania haki na fahari ya taifa hili.

Iran yaondolewa Ubingwa wa AFC U23
Timu ya vijana wenye chini ya umri wa miaka 23 ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imebanduliwa nje ya Mashindano ya Mabingwa wa Soka Asia licha ya kuicharaza China bao 1 bila jibu. Katika mchezo huo wa Jumatano katika Uwanja wa Tinsulanon nchini Thailand, goli la nahodha Omid Noorafkan alilolifunga kupitia mkwaju wa penati kunako dakika ya 87 halikutosha kuisogeza mbele Iran. Kabla ya hapo, timu hiyo ya Omid (Matumaini) ya Iran inayonolewa na Hamid Estili ililazimishwa sare katika michezo miwili ya kwanza ya Mashindano ya Mabingwa wa Soka Asia 2020 nchini Thailand. Matumaini ya Omid ya Iran kutinga Michezo ya Olimpiki Japan yamezimwa baada ya kutoonyesha matokeo ya kuridhisha kwenye mashindano hayo ya kikanda. Mashindano hayo yanayofanyika nchini Thailand tangu Januari 8 yatamalizika Januari 26. Nchi tatu zitakazoibuka kidedea zitajikatia tiketi ya kushiriki Michezo ya Olimpiki ya Julai mwaka ujaohuu 2020 jijini Tokyo Japan. Timu hiyo ya soka ya vijana ya Iran ilishiriki michezo ya Olimpiki mara ya mwisho mwaka 1976 jijini Munich.
Dondoo kutoka Afrika
Ndoto ya mshambuliaji nyota wa klabu ya KRC Genk ya nchini Ubelgiji na nahodha wa timu ya taifa ya soka ya Tanzania, Ali Mbwana Samatta inaelekea kutimia naada ya mwanasoka huyo nyota kujiunga na klabu ya Aston Villa inayocheza Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza kwa dau la pauni milioni 10. Samatta alitambulishwa rasmi kwenye klabu hiyo Jumapili mara baada ya kufanyiwa vipimo vya afya. Awali, ilielezwa kuwa Samatta angetua Norwich City au Newcastle, lakini Aston Villa wameibuka na kumchangamkia. Samatta anakuwa mchezaji wa kwanza wa Tanzania kucheza soka katika Ligi Kuu ya Uingereza.
Usajili wa Samatta Aston Villa unaweza kuwa sahihi kwake licha ya kwamba timu hiyo ipo kwenye nafasi mbaya na hatari ya kushuka daraja. Inatazamiwa kuwa, uwepo wa Samatta kikosini hapo unaweza kuwa chachu ya kuifanya timu hiyo ikabaki EPL. Samatta mwenye umri wamiaka 27 lianza kucheza nje ya Tanzania alipojiunga na TP Mazembe ya Kongo DR akitokea Simba na kuichezea kwa mafanikio hadi alipoamua kutoka nje ya bara la Afrika akijiunga na KRC Genk ambayo ameiwezesha kucheza Europa League au Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Mbali na hayo, kwa mwaka wa pili mfululizo, mwanariadha nyota wa Kenya Eliud Kipchoge ameteuliwa kuwania tuzo ya mwanamichezo bora duniani ya Laureus ambayo mshindi atajulikana mnamo Februari 17, mwaka huu 2020 jijini Berlin, Ujerumani. Mshikilizi huyo wa rekodi ya dunia ya mbio za kilomita 42 ya saa 2:01:39, ambaye pia ni mtu wa kwanza kutimka umbali huo chini ya saa mbili (alipokimbia saa 1:59:40 kwenye mbio maalum za INEOS 1:59 Challenge nchini Austria mwezi Oktoba 2019), atawania tuzo hiyo dhidi ya wanamichezo wengine watano akiwemo mwanasoka bora duniani Lionel Messi kutoka Argentina. Mwanatenisi shapavu Rafael Nadal (Uhispania), mwendeshaji mahiri wa pikipiki Marc Marquez (Uhispania), mchezaji gofu mtajika Tiger Woods (Marekani) na dereva mashuhuri wa magari ya langalanga Lewis Hamilton (Uingereza) wanakamilisha orodha ya wawaniaji wa kitengo hicho cha juu. Kipchoge amenyakua mataji mengi tu katika siku za hivi karibuni likiwemo la mwanariadha bora duniani.
Kwengineko, awamu inayofuata ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2021) hatimaye itachezwa nchini Cameroon kuanzia Januari 9 hadi Februari 6 badala ya Juni hadi Julai mwakani. Jumatano ya Januari 15, serikali ya Cameroon na Shirikisho la Mpira wa Miguu barani Afrika (CAF) wamekubaliana kuhusu mabadiliko ya tarehe hizo jijini Yaounde, kutokana na msimu wa mvua katika ukanda huo. Mabadiliko haya yanatarajiwa kujadiliwa tena katika mkutano ujao wa Kamati ya Utendaji ya CAF, ambao utafanyika pambizoni mwa michuano ya Kombe la Afrika la Futsal itakayotifua mavumbi kuanzia Januari 28 hadi Februari 7 huko Laayoune.

Na kwa mara nyingine tena bilionea namba moja barani Afrika, Aliko Dangote amesema kuwa anatarajia kuinunua klabu ya Arsenal inayoshiriki Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza ifikapo wakani. Dangote ambaye ndiye tajiri namba moja barani Afrika kwa mujibu wa jarida la Forbes anakadiriwa kuwa na utajiri wenye thamani ya dola za Kimarekani bilioni 10.3 kupitia biashara zake. Anasisitiza kuwa, kufikia mwaka ujao 2021, ndoto yake hiyo ya kuinunua Gunners itakuwa imekamilika. Kwa muda mrefu bilionea huyo wa Nigeria amekuwa akihusishwa na kutaka kuichukua Arsenal ambayo inamilikiwa na shirika la Kroenke Sports & Entertainment (KSE). Mwaka 2018, Dangote aliwahi kuiambia Reuters kuwa “Tutaifuata Arsenal 2020, hata kama kuna mtu atainunua, bado tutaifuata.” Bilionea huyo mwenye umri wa miaka 62, amekuwa akijihusisha na na miradi mbalimbali ya kibiashara ikiwemo saruji.
Ligi ya EPL
Tunatamatisha kwa kutupia jicho baadhi ya matokeo ya Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza. Klabu ya Liverpool Jumapili usiku ilishuka katika dimba la nyumbani la Anfiled kuvaana na Manchester United katika mchezo uliokuwa wa kusisimua. Kocha Mkuu wa Liverpool Jurgen Klopp alimzidi mbinu mpinzani wake Ole Gunnar Solksjaer wa Man U kwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 kwenye mchezo huo wa Ligi Kuu Uingereza. Liverpool inazidi kuongeza nguvu za kuufukuzia ubingwa kutokana na kushindikana kupoteza mechi ilizocheza mpaka sasa kwenye ligi. Bao la kwanza kwa Liverpool lilifungwa na beki kisiki, Virgil Van Dijk dakika ya 14 kipindi cha kwanza kwa kichwa, huku bao la pili likifungwa na Mohamed Salah katika dakika za lala salama. Ushindi huo unaifanya Liverpool kujikita kileleni ikiwa na jumla ya pointi 64 kwa mechi 22 ilizocheza huku mabingwa watetezi Manchester City wakiwa nafasi ya pili na pointi 47. United ipo nafasi ya tano na pointi 34 ikiwa imecheza mechi 23. Burnley ilipata ushindi hafifu wa mabao 2-1 ilipotoana jasho na Leicester City katika Uwanja wa Turf Moor Jumapili. Jumamosi, Arsenal walilazimishwa sare ya 1-1 na Sheffield United wakati ambapo New Castle walikuwa wanaibamiza Chelesea bao moja la uchungu bila jibu.
............................TAMATI...................