Feb 03, 2020 08:13 UTC
  • Ulimwengu wa Spoti, Feb 3

Ufuatao ni mkusanyiko wa baadhi ya matukio muhimu ya michezo yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita kitaifa na kimataifa....

Futsal: Mabinti wa Iran watwaa taji la CAFA

Timu ya taifa ya wasichana ya mchezo wa futsal ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetwaa ubingwa wa mashindano ya Mabingwa wa Futsal Wenye Chini ya Miaka 19 ya Asia Mwaka huu 2020 kwa kushinda mechi zake zote katika mashindano hayo. Katika mchezo wake wa mwisho siku ya Jumatano, akina dada hao wa Iran wanaonelewa na Nilloofar Ardalan waliigaragaza Jamhuri ya Kyrgyzstan mabao 2-0.

Kabla ya hapo, timu hiyo ya taifa ya wasichana ya mchezo wa futsal ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilikuwa imeifanyia mauaji ya kimbari Turkmenistan kwa kuisagasaga mabao 12-0. Kadhalika akina dada hao wa Kiirani waliichabanga Tajikistan mabao 15-0 katika mchuano wa ufunguzi, kabla ya kuibamiza Afghanistan mabao 16-1 katika mchuano uliofuata. Timu hiyo pia ilichabanga Uzbekistan siku ya Jumanne kabla ya kutoana udhia na Jamhuri ya Kyrgyzstan katika mchuano wa mwisho siku ya Jumatano.

MABIGWA! Timu ya taifa ya wasichana ya mchezo wa futsal ya Iran

 

Muirani Roghaye Someye ametangazwa mchezaji aliyefunga mabao mengi zaidi, kwa kucheka na nyavu mara 18, huku Maral Torkaman akitawazwa kuwa mchezaji mwenye thamani kubwa zaidi kwenye mashindano hayo. Mashindano hayo ya kibara ya 'U19 Girl’s Futsal Championship 2020' yaliandaliwa na Shirikisho la Soka Asia ya Kati (CAFA) kwa kushirikiana na mashirikisho ya kandanda ya timu zinazocheza, yalianza Januari 24 na kufunga pazia lake Januari 29 katika mji wa Dushanbe, Tajikistan.

Karate; Vijana wa Kenya wang'ara UAE

Klabu ya Karate ya Munawwar ya Kenya imeibuka kidedea katika Duru ya 16 ya Kombe la JKS mjini Sharjah katika Umoja wa Falme za Kiarabu. Klabu hiyo ya vijana wadogo ya Mombasa Pwani ya Kenya ilitangazwa kuwa timu bora katika mashindano hayo ya mabingwa wa karate kwa kuzoa jumla ya medali 16 Ijumaa, zikiwemo 10 za dhahabu, fedha 4 na shaba 2. Chena Adi Karanja ambaye ni binti pekee aliyeiwakilisha Kenya katika mashindano hayo alitwaa medali ya dhahabu katika kategoria ya kata ya vijana wenye umri wa miaka 9. Wengine waliotwaa dhahabu katika kategoria tofauti ni Labib Said Mohamed, Hemed Tawfiq Fernandes, Omar Feisal Salim, Abdulrahman Abdallah Hemed, Amir Faraj Amir na Awadh Amir Awadh. Timu hiyo ambayo aghalabu ya wachezaji wake ni Waislamu ilipokewa kwa mbwembwe na vifijo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Moi mjini Mombasa, iliporejea kutoka Imarati.

Kijana Abdulrahman Abdalla aliyeshinda medali mbili za dhahabu Sharja UAE

 

Karate ni mojawapo ya michezo ambayo inaendelea kupata umaarufu katika jimbo la Pwani na hasa katika Kaunti ya Mombasa ambapo kuna klabu kadhaa za mchezo huo. Wanakarate kadhaa wamewahi kushiriki kwenye mashindano ya kitaifa na kimataifa na kufanya vizuri.

Masumbiwi: Mtanzania ambwaga Mthailand

Bondia Mtanzania Salim Mtango amefanikiwa kushinda mkanda wa Ubingwa wa Dunia (UBO) uzito wa lightweight baada ya kumtoa kamasi Suriya Tatakhun kutoka Thailand aliyeonekana kuwa hatari kwa Watanzania wanne aliowahi kupigana nao na kuwapiga. Mthailand alibwagwa katika raundi ya 7 kwa gumi zito la kiufundi Technical Knock Out (TKO) katika pambano la raundi 10 lililochezwa katika uwanja wa Mkwakwani Tanga. Mtango anakuwa bondia wa kwanza wa Tanzania kuwahi kumpiga Suriya aliyeonekana kuwa hatari baada ya wanne wa mwanzo wote kupoteza dhidi ya Bondia huyo, hivyo Mtango ni sawa na kulipa kisasi cha watanzania wenzake waliowahi kupigwa na Suriya.

RC wa Tanga na mashabiki wakishangilia ushindi wa Salim Mtango

 

Mtango aeleze furaha ya ushindi wake. Mkuu wa Mkoa wa Tanga Martine Shigela amemuahidi zawadi ya kiwanja bondia Salim Mtango baada ya ushindi wake wa Ubingwa wa Dunia (UBO) dhidi ya Suriya Tatakhun, Mtango alishinda round ya 7 kwa Technical Knock Out (TKO) katika pambano la round 10.

Ligi Kuu ya Soka Uingereza

Tunatamatisha kwa kutupia jicho baadhi ya matokeo ya Ligi Kuu ya Soka Uingereza na tuanze na mchezo wa Jumapili usiku ambao matokeo yake yalikuwa kinyume na matarajio ya wengi, lakini soka haina bingwa wa bingwa. Klabu ya Tottenham ikiupigia nyumbani iliishushia kichapo cha mbwa Manchester City cha mabao 2-0 katika mchezo huo. Ni mchezo ambao ulishuhudia mshambuliaji Steven Bergwijn akifunga bao lake la kwanza lilikuwa limeenda skuli kunako dakika ya 63. Ni mchezo ulioshuhudia msisimko wa aina yake, kwani Ilkay Gundogan alipoteza penati huku Oleksandr Zinchenko akipigwa kadi nyekundu na kutimuliwa uwanjani. Son Heung-Min aliwaongeza vijana wa Spurs bao la pili katika dakika ya 71 ya mchezo. Kwengineko klabu ya Arsenal imeendelea kuvuma kama wafalme wa kugawana alama kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) baada ya kupiga sare yake ya 13 msimu huu ilipotoka 0-0 dhidi ya Burnley uwanjani Turf Moor, Jumapili. Vijana wa Mikel Arteta, ambao walipoteza nafasi nyingi nzuri dhidi ya Burnley na pia kuponea chupuchupu kufungwa, sasa wameandikisha sare nne mfululizo. Waliingia mechi ya Burnley wakiwa wametoka 1-1 na Crystal Palace na Sheffield United na 2-2 dhidi ya Chelsea. “Wanabunduki” wa Arsenal wamesalia katika nafasi ya 10 kwa alama 31 sawa na nambari 11 Burnley, ambao wako nyuma kwa sababu ya tofauti ya magoli. Arsenal inaongoza katika timu zilizotoka sare msimu huu wa 2019-2020 baada ya kupiga sare 13 ikifuatiwa na Wolves (11), Palace na Sheffield (tisa kila mmoja) na Watford (nane) katika nafasi tano za kwanza kwenye jedwali la timu zilizopiga sare nyingi. Liverpool inaongoza msimu kwa alama 73 baada ya kupiga Southampton 4-0 Jumamosi na kudumisha rekodi yake ya kutoshindwa ligini msimu huu kuwa 24. Mchezo wa Norwhich na New Castle pia uliishia kwa sare tasa, huku mechi ya Leicester na Chelsea ikiishia kwa sare ya mabao 2-2. Mancheter United pia ililazimishwa sare tasa na Wolverhampton huku mchezo wa Westaham na Brighton ukimalizika kwa sare ya mabao 3-3. Liverpool inasalilia kileleni mwa jedwali la ligi ikiwa na alama 73, ikifuatiwa na Man City pointi 51, huku Leicester ikifunga orodha ya tatu bora kwa alama 49. Man U kwa sasa hawana budi kuridhika na nafasi ya 7 wakiwa na pointi 35, alama 4 zaidi ya Gunner ambao wametuama katika nafasi ya 10.

Samatta ndani ya EPL

Mbwana Samatta siku ya Jumamosi alikuwa Mtanzania wa kwanza sio tu kucheza Ligi Kuu ya Soka Uingereza (EPL) bali alifanikiwa kuifungia timu yake ya Aston Villa bao moja ilipokuwa mwenyeji wa Bournemouth kwenye Uwanja wa Vitality. Hata hivyo Villa waliangukia pua kwenye mchuano huo licha ya bao la Samatta na kuzabwa 2-1.

Ally Mbwana Samatta aliposhinda tuzo huko nyuma

 

Huo ulikuwa mchezo wa pili kwa Samatta kucheza England tangu ajiunge na klabu hiyo mwezi uliopita kwa dau la paunti milioni 10, wakati alipocheza mchezo wa pili wa marudiano wa nusu fainali wa Kombe la Carabao dhidi ya Leicester City, ambako kwenye hatua hiyo walishinda jumla ya mabao 2-1. Kwa ushindi huo, Aston Villa sasa itacheza dhidi ya Manchester City katika mchezo wa fainali wa Kombe la Carabao. Samatta, ambaye msimu uliopita aliongoza kwa kufunga mabao mengi katika Ligi Kuu ya Ubelgiji, akichezea klabu ya KR Genk, amesajiliwa na Villa kwa dau la zaidi ya pauni milioni 8 ili kuisaidia timu hiyo ambayo haiku vizuri katika Ligi Kuu ya England. 

 

……………………TAMATI..………………