Uimwengu wa Michezo, Feb 17
Hujambo mpenzi msikilizaji na karibu tuangazie baadhi ya matukio yaliyogonga vichwa vya habari katika uga wa spoti, ndani ya siku saba zilizopita katika pembe mbalimbali za dunia.
Karate: Iran yatwaa medali lukuki
Timu ya karate ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetwaa jumla ya medali sita kwenye Ligi Kuu ya Karate 1 mjini Dubai, huko Imarati. Makarateka wa Iran wametwaa medali moja ya dhahabu, moja ya fedha na shaba nne katika kategoria tofauti kwenye mashindano hayo. Dhahabu ya Iran ilitwaliwa na Zabihollah Poorshab baada ya kumzidi maarifa Mkazaki, Daniyar Yuldashev kwa alama 8-5, kwenye pambano la fainali la makarateka wenye kilo zisizozidi 84.

Mahdi Khodabakhshi alitwaa medali ya fedha baada ya kumchachafya raia mwingine wa Kazakhstan, Igor Chikhmarev 1-0 kwenye mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu kwenye kitengo hicho. Makarateka 600 kutoka nchi 85 duniani wameshiriki mashindano hayo ya kimataifa, ambapo Uhispania imeibuka kidedea kwa kuzoa medali 2 za dhahabu, 3 za fedha na shaba moja. Italia imemaliza ya pili, Uturuki ya tatu, China ya nne huku Iran ikifunga orodha ya tano bora.
Kocha mpya wa Iran: Nitairejesha Team Melli kwenye mkondo
Mkufunzi mkuu mpya wa timu ya taifa ya soka ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema atafanya juu chini ili kuhakikisha kuwa kikosi hicho kinachojulikana hapa nchini kama "Team Melli" kinarejea kwenye mkondo wa kuimarika na kuboreka zaidi. Dragan Skocic alisema hayo Jumamosi katika kikao chake cha kwanza na waandishi wa habari baada ya kupewa mkataba wa kuionoa timu hiyo ya taifa ya Iran. Raia huyo wa Croatia amesema kibarua kikubwa ambacho kiko mbele yake kwa sasa ni kuhakikisha kuwa timu hiyo ya kandanda ya Iran inashiriki na kufanya vyema kwenye Kombe la Dunia nchini Qatar mwaka 2022.

Amesema yuko tayari kushirikiana na wadau wote wa soka hapa nchini, kama ambavyo hatasita kumjumuisha mchezaji wa klabu yoyote ya hapa nchini kwenye timu hiyo ya taifa, madhali ana kipaji na moyo wa kujituma. Timu hiyo ina mechi kadhaa za lazima kushinda ili itinge Kombe la Dunia 2020 nchini Qatar na Kombe la Asia 2023 nchini China. Skocic sio mgeni hapa nchini, kwani amewahi kuzinoa klabu mbalimbali za hapa nchini. Anakuwa raia wa tano wa Croatia kuinoa timu ya taifa ya mpira wa miguu ya Iran, huku watangulizi wake wakiwa ni Stanko Poklepovic, Tomislav Ivic, Miroslav Blazevic bila kumsahau Branko Ivankovic. Kocha huyo anakuja kurithi mikoba ya Mbelgiji Marc Wilmots ambaye aliondoka nchini mapema mwezi Disemba.
Soka; Zamalek, klabu bingwa Afrika
Klabu ya Zamalek ya Misri imetwaa taji la Super Cup Afrika baada ya kuizaba Esperance ya Tunisia mabao 3-1 katika mchuano wa fainali uliopigwa Qatar. Katika mchezo huo wa Februari 14, Wamisri waliitandaza ngozi na kuonana vizuri kwa pasi za tiki-taka. Ashraf Bensharki alifanikiwa kucheka na nyavu mara mbili, baada ya Yusuf Muhammad "Osama" kuipa Zamalek bao la ufunguzi kupitia kichwa, chini ya dakika 2 baada y kupulizwa kipenga cha kuanza ngoma. Bao kufutia machozi la Esperance lilifungwa na Mohamed Ali Ben Hamouda kunako dakika ya 86.
Hii ni mara ya nne kwa Zamalek kutwaa kombe hilo la kibara, baada ya kuiadhibu Esperance ambao ni mabingwa watetezi wa Kombe la Shirikisho Afrika. Michuano ya Super Cup Afrika ambayo iliasisiwa mwaka 1993 imekuwa ikisakatiwa barani humo, lakini kuanzia mwaka jana ilihamishiwa Qatar.
Riadha: Mganda avunja rekodi ya Mkenya
Mwanariadha wa Uganda Joshua Cheptegei Jumapili aliweka rekodi mpya ya dunia katika mbio za kilomita 5 akitumia muda wa dakika 12 na sekunde 51. Bingwa huyo wa dunia wa mita 10,000 alitumia vizuri mazingira katika duru ya pili ya mbio hizo za Monaco na kuvunja rekodi iliyowekwa na Mkenya Rhonex Kipruto ya dakika 13 na sekunde 18 mwezi uliopita huko Valencia. Mganda huyo mwenye asili ya Kenya mwenye umri wa miaka 23 amesema tangu mwanzoni mwa mbio hizo alikuwa amepania kukata utepe kwa chini ya dakika 13. Mfaransa Jimmy Gressier alimaliza wa pili kwa kutumia dakika 13:18, na kuvunja rekodi ya mwaka jana ya Julien Wanders ya dakika 13:29. Oktoba mwaka jana, Cheptegei alitwaa medali ya dhahabu kwenye mbio za mita 10,000 za mabingwa wa dunia zilizofanyika Doha, huku Kipruto akitia kibindoni medali ya shaba.
Dondoo za Hapa na Pale
Umoja wa Mashirikisho ya Soka Ulaya (UEFA) umetangaza kuifungia klabu ya Manchester City ya Uingereza kwa misimu miwili mfululizo kwa kutenda makosa mawili. Kwa mujibu wa UEFA ni kuwa Man City imefungiwa kushiriki michuano ya Ulaya ngazi ya klabu sambamba na kupigwa na faini ya pauni milioni 24.9 kwa kosa la kuvunja sheria za UEFA za leseni ya vilabu na malipo 'Financial Fair Play'. Bodi ya Kusimamia Masuala ya Fedha ya UEFA imesema City imevunja sheria kwa kuweka kiwango cha juu zaidi cha fedha katika mapato yake ya ufadhili kwenye mahesabu yake; na katika ripoti ya fedha iliyowasilishwa kwa shirikisho hilo kati ya 2012 na 2016 ilionesha kwamba hawakupata hasara wala faida." Aidha UEFA inasema kuwa klabu hiyo haikutoa ushirikiano wakati ikifanya uchunguzi wake.

Kwengineko waandaaji wa Michezo ya Olimpiki ya Tokyo mwaka huu 2020 wamesisitiza kuwa hawana mpango wowote wa kuakhirisha mashindano hayo ya dunia kutokana na virusi vya corona ambavyo vimeua watu karibu elfu 2 nchini China. Mkurugenzi Mkuu wa mashindano hayo ya Tokyo 2020, Yoshiro Mori ameondoa wasiwasi huo kwenye mkutano na maofisa wa ngazi ya juu wa Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa.
Ligi ya EPL
Tunatamatisha kwa kutupia jicho baadhi ya mechi zilizopigwa wikendi za Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza. Klabu ya Arsenal yafufuka! Ndivyo unavyoweza kusema kuhusu mchuano wa Jumapili usiku kati ya Gunners na New Castle. Wabeba Bunduki wakiupigia nyumbani Emirates, waliinyoa kwa chupa New Castle kwa kuitandika mabao 4 bila jibu. Ni mchuano ambao ulishuhudia Mfaransa Alexandre Lacazette akitamatisha ukame wa mabao, kwani alifanikiwa kuifungia Arsenal bao la nne katika dakika za majeruhi. Kipindi cha kwanza kilimalizika bila timu hizo kufungana. Hata hivyo mvua ya mabao ilifunguliwa na Pierre-Emerick Aubameyang katika dakika ya 54 kabla ya Nicolas Pepe kuongeza la pili dakika tatu baadaye. Mesut Ozil alifanikiwa kucheka na nyavu kunako dakika ya 90, kabla ya Lacazette kulizamisha kabisa jahazi la wageni. Kwa ushindi huo wa kishindo, Arsenal ambao wapo katika nafasi ya 10 kwenye msimamo wa ligi wamefikisha alama 34. Kwengineko klabu ya Aston Villa Jumapili ilikubali kichapo cha mabao 3-2 ilipovaana na Tottenham, huku goli la ushindi la Spurs likifungwa katika dakika za nyongeza. Hadi wanaenda mapumzikoni, Spurs ilikuwa inaongoza kwa mabao 2-1, huku kipindi cha pili Bjorn Engels akiweka mizani sawa dakika ya 53. Hii ilikuwa mechi ya pili kwa Mbwana Samatta wa Tanzania kucheza ndani ya Ligi Kuu ya Uingereza baada ya kujiunga na Villa akitokea klabu ya Genk ya Ugiriki. Spurs iliwamaliza nguvu Villa kwa bao la ushindi la dakika za nyongeza. Aston Villa ipo nafasi ya 17 ikiwa na pointi zake 25 na Spurs nafasi ya tano ikiwa na pointi 40 zote zimecheza mechi 26. Liverpool ambayo hivi karibuni iliizaba Norwich bao 1-0 inasalia kileleni mwa jedwali la EPL ikiwa na alama 76, ikifuatiwa na Manchester City yenye alama 51. Leicester wanafunga orodha ya tatu bora kwa alama 50.
.................................TAMATI....................