Ulimwengu wa Spoti, Feb 24
Ulimwengu wa Spoti, Feb 24
Hujambo mpenzi mwanaspoti na karibu tuzamie baadhi ya matukio yaliyogonga vichwa vya habari viwanjani ndani ya siku saba zilizopita. Nakusihi tuwe sote hadi tamati ya kipindi....
Iran bingwa wa mieleka Asia
Timu ya taifa ya mieleka ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetwaa ubingwa wa mashindano ya Asia ya mieleka huru (freestyle) mwaka huu 2020 yaliyofanyika New Delhi nchini India. Wanamieleka wa Iran wamezoa jumla ya medali 8 katika kategoria tofauti za mashindano hayo ya siku mbili ya kibara yaliyofunga pazia lake Jumapili. Katika siku ya mwisho ya mashindano hayo, Muirani Mohammadjavad Mohammadebrahim alitwaa medali ya dhahabu baada ya kumzidi ujuzi na maarifa Mjapani Takuma Otsu katika fainali ya kitengo cha wanamieleka wenye kilo 92. Dhahabu nyingine ya Iran ilitwaliwa na Mojtaba Goleij baada ya kumpeleka mchakamchaka mwenyeji Salywart Kadian katika safu ya kilo 97. Siku ya Jumamosi wanamilekea wa Iran walizoa medali 4 katika vitengo vitano.

Timu ya taifa ya mieleka ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeibuka kidedea kwa kuzoa 168, ikifuatiwa na mwenyeji India alama 159, huku Kazakhstan ikifunga orodha ya tatu bora kwa pointi 146.
Mpira wa Kikapu: Iran yailaza Qatar
Timu ya taifa ya mpira wa kikapu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran siku ya Jumapili iliitia skulini Qatar na kuichabanga vikapu 95-52, katika michuano ya kusaka tiketi ya kushiriki Kombe la Asia mwakani. Katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Azadi hapa jijini Tehran, Iran iliumiliki vizuri mpira na kucheza kwa kasi ya juu licha ya kutokuwepo mashabiki uwanjani hapo kwa hofu ya virusi vya corona. Kiungo wa kati wa Qatar, Emir Mujkic alifunga vikapu 14, alama nyingi zaidi katika mchezo huo, akifuatiwa na Muirani Hamed Haddadi alama 13. Kabla ya hapo, Iran ilikuwa imeitandika Syria vikapu 94-48 siku ya Alkhamisi katika mchezo mwingine wa Kundi E.

Nchi 24 zipo mbioni kusaka tiketi ya Kombe la Asia mwaka ujao 2021, mashindano ya kibara ambayo huandaliwa na Shirikisho la Basketboli Duniani FIBA.
Mechi zaakhirishwa kwa hofu ya corona Iran
Kitengo cha Afya cha Shirikisho la Michezo Iran kimesimamisha michezo na mechi mbalimbali kutonana na hofu ya virusi vya corona hapa nchini. Waziri wa Michezo wa Iran, Masoud Soltanifar amekiagiza kitengo hicho kuunda kamati ya dharura ya kupambana na tishio la corona kwenye michezo hapa nchini. Kamati hiyo siku ya Jumamosi ilitangaza kufuta michezo yote hapa nchini zikiwemo mechi za soka za ligi za daraja za chini kwa muda wa siku kumi. Hata hivyo michuano ya Ligi Kuu ya Soka ya Iran inaendelea ingawaje bila uwepo wa mashabiki viwanjani.

Mathalan, siku ya Jumapili klabu ya Esteghlal iliizaba Zob Ahan mabao 2-1 katika mchuano wa ligi kuu bila uwepo wa mashabiki uwanjani. Aidha mkoani Mashhad, kaskazini mashariki mwa nchi, kulishuhudiwa mechi nyingine ya ligi kuu bila mashabiki uwanjani. Shah Khodro ilitoka nyuma na kuibamiza Naft Masjed Soleyman mabao 2-1. Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Iran, watu 12 wamepoteza maisha kutokana na virusi vya Corona na wengine zaidi ya 40 wameambukizwa maradhi hayo kufikia sasa hapa nchini.
Matukio ya Spoti Afrika
Timu ya Taifa ya soka ya Wanawake ya Tanzania Twiga Stars imeibuka ya pili kwenye michuano ya Mataifa ya Afrika Kaskazini (UNAF) yaliyokamilika Jumamosi nchini Tunisia. Mabingwa wa mashindano hayo ambayo yalihusisha mataifa matano ikiwa ni pamoja na Morocco, Mauritania, Algeria na wenyeji Tunisia ni nchi ya Morocco. Awali Twiga Stars ilipocheza na Mauritania kwenye mashindano hayo iliifunga 7-0, kisha ikaibana mbavu Algeria kwa 3 -2. Hata hivyo walishindwa kufurukuta mbele ya Morocco na kufungwa 3-2 na hatimaye walipocheza na Tunisia walitoka sare ya 1-1.

Mbali na hayo, duru za habari zimefichua kuwa, Shirikisho la Soka Afrika CAF limetengua uteuzi wa Didier Drogba kama mshauri wa Rais wa CAF Ahmad Ahmad. Julai 2019 staa wa zamani wa Chelsea na Ivory Coast Didier Drogba na staa wa zamani wa Barcelona na Cameroon Samwel Eto’o waliteuliwa kuwa washauri wa Ahmad Ahmad lakini Drogba hajafanya chochote toka uteuzi huo utangazwe. Drogba na CAF bado hawajathibitisha taarifa hizo lakini zimeenda mbali zaidi kwa kueleza Drogba toka ateuliwe hajawahi kushauri chochote kama majukumu yake yanavyotaka lakini pia hajawahi kuhudhuria shughuli yoyote ya CAF ikiwemo mechi hata moja ya AFCON 2019.
Wakati huohuo, Katibu Mkuu wa zamani wa shirikisho hilo la kandanda Afrika, Amr Fahmy, amefariki dunia kwa ugonjwa wa saratani. Amr aliyekuwa na umri wa miaka 36 alichaguliwa kuwa katibu mkuu wa CAF November 2017 kumrithi Hicham El Amrani lakini hakudumu hata kwa miaka miwili katika nafasi hiyo. Amr mwaka jana kabla ya mauti yake alitangaza kuwa na nia ya kugombea Urais wa shirikisho la soka Afrika (CAF) ifikapo mwaka 2021, Amr aliondoka CAF katika nafasi ya ukatibu mkuu baada ya kushindwa kuelewana na Rais wa CAF Ahmad Ahmad.
Dondoo za Hapa na Pale
Mwanamasumbwi mahiri Tyson Fury ameishangaza dunia kwa kumpiga kwenye raundi ya 7 kwa gumi zito la kiufundi TKO bondia Deontay Wilder katika pambano lililofanyika Las Vegas Marekani na kutwaa Ubingwa wa Dunia wa Uzani wa Juu wa WBC. Wilder alikimbizwa hospitali mara baada ya pambano hilo kwa kuvuja damu kwenye sikio lake, huku akishindwa kuongea na waandishi wa habari kama ilivyokuwa imepangwa. Bondia Tyson Fury wa Marekani alitoka sare na raia huyo wa Uingereza katika pambano lao la kwanza ila hili la marudiano alifuta makosa yake na kuandika rekodi ya kuwa bondia wa kwanza kumpiga Wilder. Kabla ya hapo hakuwahi kupoteza pambano.

Na kwa mara nyingine tena, Japan imesisitiza kuwa ipo tayari kuandaa mashindano ya Olimpiki ya Tokyo na mashindano ya Walemavu wakati wa msimu wa joto mwaka huu kama ilivyopangwa, licha ya hali ya maambukizi ya virusi vya korona kuwa mbaya zaidi. Katibu mkuu wa Baraza la Mawaziri nchini Japan Yoshihide Suga amesema, watafuatilia kwa karibu kwa pamoja na Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki IOC, kamati ya maandalizi na serikali ya Tokyo, na kuendelea na maandalizi ili kuhakikisha wanariadha na watazamaji wanaweza kuwa salama wakati wa mashindano hayo. Huku hayo yakiarifiwa, wenyeji Inter Milan waliokuwa wakutane na Sampdoria ni miongoni mwa mechi nne za Serie A zilizopaswa kuchezwa wikendi lakini zimezuiwa kwa hofu ya kuenea kwa virusi vya korona. Zuio hilo limetangazwa na waziri mkuu wa Italia Giuseppe Conte kwenye mkutano na wanahabari siku ya Jumamosi. Michezo mingine iliyozuiwa ni pamoja na Torino dhidi ya Parma, Verona waliokuwa wacheze na Cagliari na Atalanta dhidi ya Sassuolo.
……………………..TAMATI………………...