Mar 02, 2020 06:32 UTC
  • Ulimwengu wa Spoti, Machi 2

Hujambo mpenzi msikilizaji na karibu katika dakika hizi chache za kutupia jicho baadhi ya matukio muhimu ya spoti yaliyojiri kitaifa na kimataifa ndani ya siku saba zilizopita.....

Muirani azoa medali za dhahabu UAE

Bingwa wa mchezo wa kunyanyua vyuma vizito wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametwaa medali tatu za dhahabu katika Mashindano ya Mabingwa wa Uzani wa Asia Magharibi yaliyofunga pazia lake Jumamosi mjini Dubai, Imarati. Sohrab Moradi ambaye alikuwa mwakilishi pekee wa Iran kwenye mashindano hayo alizoa medali hizo katika kategoria za kunyanyua uzani wa kilo 157, 163 na 166 kwa upande wa wanaume wenye kilo 96. Moradi amerejea ulingoni kwa kishindo, baada ya kutoshiriki mashindano ya mchezo huu tokeo Julai mwaka jana kutokana na jeraha la bega.

Sohrab Moradi akinyanyua bendera ya Iran baada ya kuibuka kidedea

 

Muirani huyo anasalia kuwa mashikilizi wa rekodi ya wanyanyua uzani wa kilo (186kg) na (216kg) aliyoiweka katika mashindano ya kibara ya Turkmenistan mwaka 2018. Timu ya wanaume na wanawake za Iran za mchezo huu zilifuta safari zao za kwenda kushiriki mashaindano haya ya UAE, kwa hofu ya homa inayosababishwa na virusi hatari vya Corona. Mashindano haya ya West Asian Championships yanatazamwa kama jukwaa la kusaka tiketi za kushiriki Michezo ya Olimpiki ya mwaka huu 2020 jijini Tokyo, Japan.

Katika habari ya tanzia, bingwa wa unyanyua uzani duniani, Siamand Rahman wa Iran ameaga dunia akiwa na miaka 32. Nyota huyo wa michezo ya walemavu alifariki dunia siku ya Jumapili kutokana na mshtuko wa moyo. Siamand Rahman aliaga dunia akiwa katika Hospitali ya Nabi Akram katika mji wa Oshnavieh, mkoani Azerbaijan Magharibi. Alivunja rekodi ya uzani wa kilo 300 katika Michezo ya Paralimpiki ya Rio mwaka 2016, kwa kunyanyua uzani wa kilo 310 katika safu ya wanaume wenye kilo 107.

Simand Rahman, bingwa wa kunyanyua uzani wa Iran

 

Bingwa huyo wa uzani wa Iran alitwaa medali za dhahabu katika olimpiki za London 2012 na Rio Brazil 2016, mbali na dhahabu tano na fedha moja katika mashindano ya Para-Asian huko Guangzhou China 2010, Incheon 2014 na Jakarta 2018. 

Riadha: Bekele avunja rekodi ya Mo Farah

Mwanariadha nyota wa Ethiopia, Kenenisa Bekele amevunja rekodi ya bingwa wa riadha Uingereza, Mo Farah katika mbio za nusu marathon za London siku ya Jumapili. Bekele alikata utepe kwa kutumia saa moja na sekunde 22, na kuvunja rekodi iliyowekwa na Farah mwaka jana 2019 kwa dakika moja na sekunde 18. Mo Farah hakushiriki London Half-Marathon mwaka huu kutokana na jereha la mguu. Katika mbio hizo za Jumapili, Muingereza Christopher Thompson alimaliza wa pili huku nafasi ya tatu ikitwaliwa na Jake Smith. Bekele amesema ushindi huo ni zawadi kubwa kwake wakati huu akijiandaa kwa mbio za nyika za London zikazotifua mavumbi Aprili 26, ambapo atakutana na miamba ya riadha duniani kama Eliud Kipchoge wa Kenya.

Tukiwa bado katika riadha, wanariadha Joseph Panga na Magdalena Shauri wameitoa kimasomaso Tanzania kwa kutwaa dhahabu katika mbio za Tigo nusu marathon za mashindano ya Kilimanjaro marathoni yaliyofanyika wikendi kwenye viwanja vya ushirika mjini Moshi. Panga ameibuka kidedea upande wa wanaume wakati Magdalena aking'ara upande wa wanawake na kuwapiku wanariadha wengine 5,500 waliokimbia mbio za nusu marathoni. Tangu mwanzo wa mbio, Panga alikuwa akiongoza akifuatiwa na Watanzania, Josephat Joshua aliyetwaa medali ya fedha, Francis Damiano na Joshua Elisante ambao hata hivyo walipitwa na Mkenya, Joseph Kimathi aliyetwaa medali ya shaba zikiwa zimebakia mita 500 kumaliza mbio.

Soka Wanawake; Tanzania yaiadhibu Uganda

Timu ya Taifa ya soka ya Tanzania ya wanawake wenye chini ya miaka 17, imeichabanga Uganda kwa mabao 2-1 katika mchezo wa kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia uliofanyika Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Mshambuliaji wa Tanzania, Aisha Masaka alifunga mabao mawili na kuiweka timu yake katika mazingira mazuri ya kusonga mbele kwenye fainali. Tanzania inahitaji kulinda ushindi wake au kuongeza mabao zaidi katika mchezo wa marudiano utakaopigwa Machi 13 nchini Uganda ili kupata nafasi ya kucheza na mshindi wa mechi kati ya Sao Tome & Principe na Cameroon, na mshindi wa mechi hiyo atafuzu moja kwa moja fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika kuanzia Novemba 2 hadi 21 nchini India.

Dondoo za Hapa na Pale

Klabu ya Aston Villa ya Uingereza Jumapili ya Machi Mosi ilishuhudia ubingwa ukiponyoka na kuangukia mikononi mwa wapinzani wao Manchester City. Villa inayonolewa na Dean Smith ilikubali kichapo cha mabao 2-1 kwenye mchezo huo wa fainali wa Kombe la Carabao uliochezwa katika Uwanja wa Wembley. City ilianza kuandika bao la kwanza dakika ya 20 kupitia kwa Muargentina Sergio Arguero akimalizia pasi ya Philip Foden na bao la pili dakika ya 30 kupitia kwa Rodri Hernandez akimalizia pasi ya İlkay Gundogan. Mbwana Samatta wa Tanzania alipachika bao dakika ya 41 kwa kichwa kilichozama nyavuni jumlajumla akimalizia pasi ya kiungo Mholanzi, Anwar El Ghazi. Baada ya kazi yake nzuri ambayo hata hivyo haikuisaidia Aston Villa kupata taji, kocha Dean Smith alimpumzisha Samatta dakika ya 80 na kumuingiza kinda wa England, Keinan Davis.  Ushindi huo unamaanisha Manchester City inatwaa taji la Carabao kwa mara ya tatu mfululizo na kujifariji katika msimu ambao hawana matokeo mazuri kwenye Ligi Kuu.

Mbali na hayo, klabu ya Arsenal ya Uingereza imeondolewa katika michuano ya Europa League kwa kufungwa mabao 2-1 na Olympiacos ya Ugiriki licha ya kuupigia nyumbani katika uwanja wa Emirates. Vijana wa Mikel Arteta walikuwa wamelemea Wagiriki hao 1-0 ugenini mnamo Februari 20. Lakini walizamishwa na bao la Youssef El-Arabi, sekunde 60 kabla ya dakika 30 za nyongeza kutamatika. Olympiacos ilimaliza muda wa kawaida uwanjani Emirates ikiwa bao 1-0 juu, baada ya Pape Abou Cisse kutikisa nyavu dakika ya 53. Bao lake lilifanya dakika 30 ziongezwe ili kuamua mshindi. Arsenal ilijipatia matumaini ya kuingia raundi ya 16-bora mshambuliaji Pierre-Emerick Aubameyang aliposawazisha 1-1 kupitia bao safi la makasi dakika ya 113. Bao la Aubameyang liliweka Arsenal mbele 2-1, kwa sababu ilikuwa imeshinda mechi ya mkondo wa kwanza kupitia bao la Alexandre Lacazette. Hata hivyo, ndoto yao ilizimwa baada ya El-Arabi kupatia Olympiacos bao la pili kunako dakika ya 119.

Nao wafalme wa mwaka 2003 na 2011, Porto walikubali vichapo viwili kutoka kwa Bayer Leverkusen na kusalimu amri kwa jumla ya mabao 5-2. Klabu zingine kubwa zilizofunganya virago kutoka Ligi ya Uropa ni Benfica, Sporting Lisbon na Braga kutoka Ureno, Celtic (Scotland) na AZ Alkmaar (Uholanzi).

Man City, bingwa wa Carabao tena!

 

Na mchezaji tenisi namba mbili duniani Rafael Nadal ameshinda taji lake la tatu la Michuano ya Wazi ya Mexico baada ya kumenyana na kumshinda Taylor Fritz kwa seti 6-3 na 6-2 kwenye fainali. Nadal hajapoteza hata seti moja kwenye mashindano na kumzidi nguvu Fritz huko Acapulco akiondoka na taji lake la 85 kwa mchezaji mmoja mmoja, na la kwanza katika msimu huu.

Rafael Nadal

 

Mataji mawili ya Mexico aliyopata Mhispania huyo yalikuwa ni mwaka 2005 na 2013. Naye Fritz ambaye yupo namba 35 duniani amekutana na Nadal kwa mara ya kwanza, licha ya kwamba amecheza kwa mara ya tano kwenye fainali za ATP. Mmarekani huyo mwenye miaka 22 amesema mpinzani wake alikuwa na uwezo mkubwa sana.

…………………...TAMATI………………