Apr 06, 2020 02:31 UTC
  • Jumatatu 6 Aprili 2020

Leo ni Jumatatu tarehe 12 Shaabani 1441 Hijria inayosadifiana na tarehe 6 Aprili mwaka 2020.

Siku kama ya leo miaka 943 iliyopita aliaga dunia Hassan bin Hafiz Andalusi Ghassani mpokeaji hadithi na tabibu mashuhuri wa Andalusia, sehemu ya Uhispania ya leo. Ghassani alikuwa mwanafasihi mahiri na tabibu mweledi. Aidha alikuwa na hati za kuvutia sana na mwenye kipaji kikubwa cha kutunga mashairi.

Siku kama ya leo miaka 440 iliyopita, ardhi ya Ureno moja kati ya nchi zilizokuwa na nguvu barani Ulaya katika karne za 15 na 16 iliunganishwa na Uhispania. Ureno ilikuwa mpinzani wa kisiasa na kikoloni wa Uhispania huko Asia, Afrika na Marekani. Hata hivyo kutokana na raia wa nchi hiyo kuhamia kwa wingi katika nchi makoloni ya Ureno na vile vile hali mbaya ya kiuchumi taratibu Ureno ilianza kupoteza satwa na nguvu yake ya kisasa. Udhaifu na kutokuwa na nguvu Ureno uliipelekea Uhispania kuivamia nchi hiyo. Pamoja na hayo yote hatimaye mapambano ya ukombozi ya wananchi wa Ureno ya mwaka 1640 yalipelekea kukombolewa tena nchi hiyo.

Bendera ya Ureno

Siku kama ya leo miaka 75 iliyopita mwaka 1945 Miladia, yalianza mashambulizi makubwa ya vikosi vya Marekani dhidi ya kisiwa cha Okinawa nchini Japan. Mashambulizi hayo yaliyotokea mwishoni mwa Vita vya Pili vya Dunia, yanahesabiwa kuwa vita vya mwisho na vikubwa zaidi vya baharini na nchi kavu kuwahi kupiganwa baina ya Marekani na Japan. Vita hivyo vya siku 83 vilizishirikisha meli 1300 na karibu ndege za vita 10,000 za Marekani. Katika vita hivyo Wajapani walipambana vikali kutetea ardhi yao, kiasi kwamba makumi ya meli za kivita za Marekani zilitokomezwa na kuharibiwa vibaya kutokana na mashambulizi makali ya marubani wa Kijapani katika operesheni za kujiojitolea mhanga kikosi cha marubani waliojulikana kwa jina la Kamikaze. Katika mashambulizi hayo ndege za kivita za Marekani 769 zilitunguliwa. Hata hivyo Wajapani walipata hasara kubwa katika kutetea kisiwa cha Okinawa kiasi kwamba kati ya wapiganaji 120,000 110,000 waliuawa na kujeruhiwa. Jeshi la Japan lilipoteza meli 16 na ndege za kivita 7830.

Hujuma ya ndege za kikosi cha Kamikaze dhidi ya meli za kivita za Japan

Miaka 35 iliyopita katika siku kama hii ya leo Ja'far Nimeiry, Rais wa zamani wa Sudan alipinduliwa na Jenerali Abdulrahman Swarul Dhahab aliyekuwa Waziri wa Ulinzi ambaye alichukua madaraka ya kuiongoza Sudan. Ni vyema kuashiria hapa kuwa Nimeiry pia aliingia madarakani kufuatia mapinduzi ya kijeshi yaliyotokea Sudan mwaka 1969. Nimeiry aliongoza Sudan kimabavu kwa miaka 16 na kuanzisha uhusiano mkubwa  kati ya nchi hiyo na Marekani.

Ja'far Nimeiry

Katika siku kama ya leo miaka 26 iliyopita, Wahutu wenye misimamo mikali wa Rwanda walianzisha mauaji makubwa dhidi ya Watutsi. Katika mauaji hayo Wahutu wenye misimamo mikali waliwauwa raia wa Kitutsi na Wahutu wenye misimamo ya wastani karibu milioni moja na kuwafanya mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi. Wahutu wanaunda asilimia 84 ya jamii ya Rwanda na kabila hilo lilikuwa madarakani hadi mwaka 1994.

Karibu Watusi Milioni moja waliuawa katika kipindi cha siku mia moja nchini Rwanda.

 

Tags