Jun 11, 2020 04:30 UTC
  • Juamatano tarehe 10 Juni mwaka 2020

Leo ni Jumatano tarehe 18 Shawwal 1441 Hijria sawa na tarehe 10 Juni mwaka 2020.

Miaka 230 iliyopitaka katika siku kama ya leo inayosadifiana na tarehe 10 Juni 1790 vikosi vya Jeshi la Uingereza viliivamia ardhi ya Melaya inayojulikana hii leo kama Malaysia. Wakati huo Uholanzi ilikuwa ikiikoloni Maleya na kupora utajiri mkubwa wa nchi hiyo wa madini ya bati. Kwa kuingia vikosi vya Uingereza Maleya iliibidi Uholanzi ianze kuondoka nchini humo na ilipofikia mwaka 1824 Uholanzi ilikubali kuiachia Uingereza ardhi hiyo kwa sharti kwamba nayo iachiwe Indonesia ambayo ilikuwa ina umuhimu mkubwa kwa Uholanzi. Malaysia ilijipatia uhuru wake mwaka 1957 na Indonesia mwaka 1956.

Katika siku kama ya leo miaka 208 iliyopita, vita vya Marekani na Uingereza vilianza. Miongoni mwa matukio muhimu ya historia ya Marekani katika nusu ya kwanza ya karne ya 19 ni vita hivyo vilivyodumu kwa miaka miwili. Sababu ya kuanza vita hivyo inasemekana kuwa ni kuzingirwa Ufaransa na Uingereza kutokea baharini na kuzuiwa safari za meli za Marekani katika maji yanayozunguka nchi za Ulaya. Lakini pamoja na hayo Marekani ilikuwa na sababu zingine za kuanzisha vita hivyo, muhimu kati yazo ikiwa ni madai ya uungaji mkono wa siri wa Uingereza kwa Wahindi Wekundu wa Marekani dhidi ya serikali kuu ya nchi hiyo. Kufuatia vita hivyo, tarehe 18 Juni 1812 askari jeshi wa Marekani walivamia vituo na mali za Uingereza huko Canada na kuuteketeza mji wa Toronto. Vita hivyo vilipamba moto kiasi kwamba, mwezi Agosti 1814 Uingereza ilituma askari wake katika pwani ya mashariki ya Marekani na kuendesha vita hadi katika mji mkuu wa nchi hiyo, Washington DC. Hatimaye mazungumzo ya amani baina ya nchi mbili hizo yalitiwa saini huko Ubelgiji na kupelekea kusimamishwa vita hivyo mwezi Disemba mwaka huhuo wa 1814.

Katika siku kama ya leo miaka 187 iliyopita, alizaliwa msomi wa Kiislamu Hajj Mirza Hussain Nuri katika eneo la Nur huko kaskazini mwa Iran. Msomi huyu mkubwa alifikia daraja ya juu katika ibada, ucha-Mungu na ukamilifu wa nafsi. Hajj Mirza Hussein alikuwa hodari katika elimu za fiqhi, hadithi, tafsiri ya Qur'ani tukufu na mashairi na mwandishi aliyebobea wa vitabu. Vitabu vyake vingi vilihusu elimu za hadithi, tafsiri na ufafanuzi kuhusiana na maisha ya wasomi wa Kiislamu. Mirza Hussain Nuri alilipa umuhimu mkubwa suala la kueneza athari za Ahlul-Baiti wa Mtume (saw). Msomi huyo mkubwa wa Kiislamu ameandika vitabu vingi na miongoni mwa athari zake mashuhuri ni pamoja na kitabu cha "Mustadrakul Wasaail", "Maalimul Sabr", "Jannatul Maawa" na "Nafasur Rahman". Mirza Hussein Nuri amezikwa katika mji mtakatifu wa Najaf nchini Iraq. 

Hajj Mirza Hussain Nuri

Miaka 46 iliyopita katika siku kama ya leo sawa na tarehe 21 Khordad mwaka 1353 kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani, alifariki dunia Daktari Muhamaad Khaz'ali, mwasisi wa Tasisi ya Kuongoza na KuwasaidiaVipofu ya Iran. Dakta Khaz'ali alipokuwa mtoto alipoteza macho yake kutokana na ugonjwa wa ndui, na alipata elimu katika shule maalumu ya vipofu. Dakta huyo kwa kutumia uwezo wake mkubwa wa kuhifadhi mambo, alipata mafanikio makubwa katika masomo yake na kufanikiwa kuhitimu shahada ya uzamilifu ya sheria katika chuo kikuu cha Tehran. Dakta Khaz'ali alifahamu vyema lugha ya Kiarabu, Kifaransa na Kiingereza na aliandika na kutafsiri vitabu mbalimbali. Miongoni mwa masuala aliyojishughulisha nayo Dakta Khaz'ali ni kupigania kupatiwa huduma muhimu vipofu katika uga wa kimataifa na alikuwa pia mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Mashariki ya Kati katika Baraza la kitaifa la kuwahudumia vipofu.

Daktari Muhamaad Khaz'ali

Siku kama ya leo miaka 20 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 10 Juni mwaka 2000, alifariki dunia Rais Hafidh Assad wa Syria baada ya kuugua kwa muda mrefu. Hafidh Assad alizaliwa mwaka 1930 na aliteuliwa kuwa kamanda wa vikosi vya Jeshi la Anga la Syria mwaka 1964, miaka mitatu baadaye alichaguliwa kuwa Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo. Mwaka 1970 kupitia mapinduzi ya kijeshi, Hafidh Assad alitwaa madaraka ya nchi hiyo na baadaye kuchaguliwa kuwa kiongozi wa chama cha Baath. Miongoni mwa sifa za siasa za nje za Syria wakati wa urais wa Hafidh Assad, zilikuwa ni kutofanya mapatano na utawala wa Kizayuni wa Israel na kuimarisha uhusiano na nchi zinazopinga Uzayuni kama Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Hafidh Assad

 

Tags