Jul 01, 2020 08:11 UTC
  • Jumatano tarehe Mosi Julai mwaka 2020

Leo ni tarehe 9 Dhulqaada 1441 Hijria inayosadifiana na tarehe Mosi Julai mwaka 2020.

Siku kama ya leo miaka 232 iliyopita alizaliwa Jean Victor Poncelet mwasisi wa uchambuzi wa maumbo. Victor Poncelet aliyekuwa mtaalamu maarufu wa hisabati wa Ufaransa, alitambulika kuwa mwasisi wa uchambuzi wa maumbo. Poncelet alikuwa mmoja wa maafisa wa jeshi la Napolione na alitekwa nyara na Warusi wakati jeshi la Ufaransa lilipokuwa likirejea nyuma kutoka Urusi ya zamani. Hata hivyo katika kipindi cha kutekwa alijiendeleza kielimu na kukamisha elimu yake ya uhandisi. Jean Victor Poncelet alifariki dunia tarehe 22 Disemba 1867.

Jean Victor Poncelet

Siku kama ya leo miaka 153 iliyopita, nchi ya Canada ilijitangazia uhuru kutoka kwa mkoloni Mwingereza. Canada iligunduliwa mwishoni mwa karne ya 15 Miladia na kuanzia wakati huo kwa zaidi ya karne mbili, Uingereza na Ufaransa zilikuwa zikishindana katika ardhi ya nchi hiyo kwa lengo la kupanua udhibiti wao. Ushindani huo ulipelekea kujiri vita kati ya mataifa hayo ya kikoloni ambapo mwaka 1689 vita hivyo vilidumu kwa karibu miaka 75 vilimalizika kwa kushindwa Ufaransa. Kuanzia mwanzoni mwa karne ya 19 taratibu zilianza harakati za kupigania uhuru wa Canada ambazo zilizaa matunda mwaka 1867 katika siku kama ya leo.

Bendera ya Canada

Miaka 60 iliyopita katika siku kama ya leo, sehemu mbili za Somalia ya Uingereza na ya Italia ziliungana na kuunda nchi moja ya Somalia yenye kujitawala. Karne kadhaa nyuma, Somalia iliwahi kujitawala kwa kipindi kifupi. Mwaka 1884 Uingereza iliiweka katika himaya yake sehemu ya ardhi ya nchi hiyo. Miaka mitano baadaye Italia nayo ikakoloni baadhi ya sehemu za Somalia. Harakati za mapambano za Muhammad Abdullah Hassan dhidi ya Waingereza kuanzia mwaka 1901 hadi 1920 hazikuzaa matunda. Mwaka 1950 Umoja wa Mataifa uliitaka Italia iandae mazingira ya kujitawala na kuwa huru nchi ya Somalia.

Somalia katika ramani ya dunia

Katika siku kama ya leo miaka 58 iliyopita, nchi ndogo ya Burundi ilijitangazia uhuru wake. Kuanzia mwaka 1899 hadi 1917 Burundi pamoja na Rwanda ilikuwa sehemu ya makoloni ya Mjerumani huko Afrika Mashariki. Baada ya Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia na kushindwa Ujerumani katika vita hivyo, Umoja wa Mataifa uliikabidhi Ubelgiji ardhi ya Burundi. Mwaka 1962 Burundi ilipata uhuru ikiwa na mfumo wa utawala wa kifalme. Hata hivyo miaka minne baadaye wapigania jamhuri walimuondoa madarakani mfalme na kuanzisha mfumo wa serikali ya jamhuri. 

Bendera ya Burundi

Na siku kama ya leo miaka 58 iliyopita, Rwanda ilipata uhuru. Rwanda ina historia inayofanana na jirani yake wa kusini yaani Burundi ambapo kabla ya nchi hizo kujitangazia uhuru zilikuwa zikikoloniwa na Ubelgiji. Baada ya mapambano mtawalia ya wapigania uhuru wa Rwanda, hatimaye mnamo mwaka 1962, nchi hiyo ilipata uhuru na kabila kubwa la Wahutu likashika hatamu za uongozi wa nchi. Mwaka 1973, Meja-Jenerali Juvenal Habyarimana alichukua madarakani baada ya kufanya mapinduzi yasiyo na umwagaji damu. Hata hivyo mwaka 1994 kulitokea mauaji ya kimbari ambapo zaidi ya watu laki 8 waliuawa wengi wao wakiwa ni wa kabila la Tutsi.

Bendera ya Rwanda

Na tarehe 11 Tir miaka 38 iliyopita Ayatullah Muhamad Saduqi alimu mkubwa, mwanamapambano na Imamu wa Ijumaa wa mji wa Yazd huko katikati mwa Iran, aliuawa shahidi na vibaraka wa kundi la kigaidi la Munafiqiin na kuwa shahidi wa nne aliyeuawa katika mihrabu ya Swala katika historia ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran. Ayatullah Muhammad Saduqi alikamilisha masomo yake ya kidini katika Hauza ya mji mtakatifu wa Qum, Iran na kustafidi na bahari kubwa ya elimu kutoka kwa walimu mashuhuri wa kituo hicho cha kielimu kama vile Ayatullah Burujerdi na Ayatullah Khansari.

Ayatullah Muhamad Saduqi