Sep 30, 2020 02:41 UTC
  • Jumatano tarehe 30 Septemba 2020

Leo ni Jumatano tarehe 12 Safar 1442 Hijria sawa na tarehe 30 Septemba mwaka 2020.

Leo tarehe 30 Septemba ni Siku ya Kimataifa ya Viziwi. Lengo la siku hii kupewa jina la Siku ya Kimataifa ya Viziwi ni kutaka kuimarisha utamaduni wa kuwa na mawasiliano ya watu wenye ulemavu huo, kustawisha maarifa ya lugha ya ishara na kuwazindua wanasiasa na watu wa kawaida kuhusu matatizo ya watu wa tabaka hilo.

Siku kama ya leo miaka 82 iliyopita kulifanyika mkutano wa kihistoria wa Munich huko Ujerumani. Mkutano huo uliwakutanisha pamoja viongozi wa Ujerumani Adolph Hitler, kiongozi wa Italia Benito Mussolini na mawaziri wakuu wa wakati huo wa Uingereza na Ufaransa. Lengo la mkutano huo lilikuwa kutafuta njia ya kutatua hitilafu za Ujerumani na Czechoslovakia. Matokeo ya mkutano huo yalikuwa kumegwa sehemu ya ardhi ya Czechoslovakia na kuunganishwa na Ujerumani. Mkataba huo ulikuwa na taathira kubwa katika matukio ya baadaye barani Ulaya na ulidhihirisha zaidi sura na tabia ya kikoloni ya nchi za Magharibi. Baada ya Vita vya Pili vya Dunia na kushindwa Ujerumani hapo mwaka 1945, Czechoslovakia ilichukua tena sehemu hiyo ya ardhi.


Mkutano wa kihistoria wa Munich

Siku kama ya leo miaka 54 iliyopita nchi ya Botswana ilifanikiwa kujipatia uhuru kutoka kwa mkoloni Mwingereza. Mwaka 1885 Botswana iliwekwa katika himaya ya Uingereza. Mapambano ya wapigania uhuru nchini humo yalishadidi tangu mwaka 1920 na mwaka 1966 nchi hiyo ilipata uhuru. Botswana inapatikana kusini mwa bara la Afrika na inapakana na nchi za Afrika Kusini, Zimbabwe na Namibia.

Botswana

Siku kama ya leo miaka 35 iliyopita alifariki dunia mvumbuzi wa kipimo kinachotumiwa kupimia nguvu ya mitetemeko ya ardhi Charles Richter. Akishirikiana na mhakiki mwingine, Richter alipima mitetemeko hiyo kwa mujibu wa nishati inayotokana na mawimbi ya mitetemeko ya ardhi toka daraja moja hadi 9 na kusajili kipimo cha Rishta. Kabla ya hapo wataalamu walikuwa wakipima mitetemeko ya ardhi kwa mujibu wa athari ya nje ya kipimo ambacho hakikuwa cha kuaminika.

Charles Richter