Nov 25, 2020 02:42 UTC
  • Jumatano, Novemba 25, 2020

Leo ni Jumatano tarehe 9 Mfunguo Saba Rabiuthani 1442 Hijria inayosadifiana na tarehe 25 Novemba mwaka 2020 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 140 iliyopita sawa na Novemba 25 mwaka 1880, kijidudu maradhi kinachosababisha maradhi ya Malaria kiligunduliwa na  Charles Luis Alphonse Laveran, tabibu mashuhuri wa Kifaransa. Ugunduzi huo wa kijidudu maradhi cha malaria ulitayarisha uwanja mzuri wa kukabiliana na kuangamiza maradhi hayo. Mnamo mwaka 1907 Dakta Alphonse Laveran alitunukiwa Tuzo ya Nobeli kutokana na utafiti wake katika masuala ya tiba.

Charles Luis Alphonse Laveran

Siku kama ya leo miaka 55 iliyopita dikteta wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo au Zaire ya zamani, Jenerali Mobutu Sese Seko alitwaa madaraka ya nchi kupitia mapinduzi ya uwagaji damu. Mobutu alizaliwa mwaka 1930 nchini Congo na mwaka 1950 alijiunga na harakati ya ukombozi ya Patrice Lumumba. Baada ya uhuru wa Congo, Jenerali Mobutu alishika uongozi wa jeshi la nchi hiyo na mwaka 1960 alikuwa waziri mkuu akiwa na umri wa miaka 30. Tarehe 25 Novemba mwaka 1965 Mobutu alipindua serikali na kushika hatamu za nchi hiyo aliyeitawala kidikteta. Tarehe 16 Mei 1997 Mobutu alilazimika kukimbia nchi hiyo na kwenda Morocco ambako alifia na kuacha nyuma faili jesi la ukatili na mauaji.

Jenerali Mobutu Sese Seko

Katika siku kama ya leo miaka 45 iliyopita yaani sawa na tarehe 25 Novemba 1975, nchi ya Suriname ambayo kijiografia ipo katika Amerika ya Kusini ilijitangazia rasmi uhuru wake toka kwa Uholanzi. Mwanzoni mwa karne ya 16 nchi hiyo ilikuwa chini ya utawala wa Uingereza. Mwaka 1954 Suriname ilijipatia utawala wa ndani na miaka 21 baadaye ikajipatia uhuru kamili. Nchi hiyo inapakana na Brazil na Guyana na iko katika pwani ya Bahari ya Atlantic.

Bendera ya Suriname

Miaka 41 iliyopita katika siku kama ya leo jeshi la kujitolea la Basiji liliundwa kutokana na amri ya Imam Khomeini mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya kuundwa jeshi la watu milioni 20 nchini Iran. Taasisi hiyo ya wananchi kutoka matabaka mbalimbali ya kijamii, kwa kuwa na wapiganaji wenye imani, moyo wa kujitolea na ari ya kuchapakazi imekuwa na nafasi muhimu katika matukio mbalimbali ya Mapinduzi ya Kiislamu hasa kipindi chote cha vita vya kujitetea kutakatifu vya taifa la Iran dhidi ya uvamizi wa Iraq. Jeshi la Basiji bado linashiriki katika masuala mbalimbali ya kijamii, kiutamaduni na kijeshi hapa nchini Iran.

Siku kama ya leo miaka 9 iliyopita alifariki dunia Vasiliy Ivanovich Alekseyev, bingwa mnyanyuaji uzani wa nchini Russia na kimataifa. Alekseyev alipata ushindi mwaka 1972 mjini Munich, Ujerumani na mwaka 1976 Montréa, Canada kwa kujinyakulia medali za dhahabu. Katika kipindi cha ushindi wake, Vasiliy Ivanovich Alekseyev aliweka rekodi ya dunia. Yeye alikuwa mnyanyuaji uzani ambaye aliweza kuweka rekodi ya kunyanyua kilogramu 645 kwa kupindukia kilogramu 600. Mwaka 1993 Shirikisho la wanyanyuaji uzani duniani lilimteua Alekseyev kuwa mmoja wa mabingwa wakubwa katika fani hiyo. Alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 69 nchini Ujerumani kutokana na matatizo ya moyo.

Vasiliy Ivanovich Alekseyev

 

Tags