Dec 13, 2020 01:49 UTC
  • Jumapili, 13 Disemba, 2020

Leo ni Jumapili tarehe 27 Mfunguo Saba Rabiu Thani mwaka 1442 Hijria sawa na tarehe 13 Disemba 2020 Miladia.

Miaka 1088 iliyopita katika siku kama ya leo, aliaga dunia Ibn Miqsam mpokeaji hadithi na mwandishi wa Kiislamu. Alizaliwa huko Baghdad na alifunzwa na maulamaa wakubwa wa mji huo kama Abbas bin Fadhil.  Hata kama Ibn Miqsam aliandika vitabu katika uwanja wa elimu ya sintaksia lakini alijibidisha zaidi katika kujifunza elimu ya Qurani. Moja ya athari za mwandishi huyo wa Kiislamu ni kitabu chake alichokipa jina la " Al Anwar fi Tafsiril- Quran. 

Ibn Miqsam   

Siku kama ya leo miaka 89 iliyopita sawa na Disemba 13 mwaka 1931 Miladia, aliaga dunia Gustave Le Bon mwanafikira wa masuala ya mashariki na mwandishi mtajika wa Kifaransa. Gustave Le Bon mwanafikra na mwandishi wa Kifaransa aliyekuwa amebobea katika historia ya utamaduni wa Kiislamu alizaliwa mwaka 1841 nchini Ufaransa. Gustave alianza kusoma masomo ya utabibu baada ya kukamilisha masomo ya awali hata hivyo kile kilichompelekea kuwa maarufu ni utafiti wa kihistoria na kijamii alioufanya. Hii ni kwa sababu  alikuwa na hamu ya kujifunza saikolojia ya jamii mbalimbali, kuendeleza na kukamilisha nadharia ya saikolojia ya jamii. Gustave Le Bon kimsingi alifanya utafiti wake wake wa kijamii kuhusu masuala ya saikolojia ambapo aliandika vitabu vingi katika uwanja huo; vitabu ambavyo viliungwa mkono na wanafikra kutoka nchi mbalimbali na kufasiriwa katika lugha tofauti. Hatimaye Dakta Gustave Le Bon aliaga dunia tarehe 13 mwezi Disemba mwaka 1931 karibu na Paris akiwa na umri wa miaka 90. 

Gustave Le Bon   

Tarehe 13 mwezi Disemba mwaka 1963 Sheikh Mahmood Shaltoot Mkuu wa Chuo Kikuu cha Al Azhar na Mufti Mkuu wa zamani wa Misri aliaga dunia. Mwanazuoni huyo mkubwa wa Misri alizaliwa mwaka 1892 nchini Misri. Akiwa na umri wa miaka 14 alianza masomo ya shule ya upili katika Chuo cha Kidini cha Alexandria kilichokuwa tawi la Al Azhar. Alipata chetu cha chuo kikuu mwaka 1918 na kuanza kufunza katika chuo hicho hicho na kisha hatimaya akahamia chuo kikuu cha al Azhar mwaka 1927. Alizidi kupanda cheo kielimu na kuteuliwa kuwa mwanachama wa baraza la Fatwa chuoni hapo. Mwaka 1958 aliteuliwa kuwa mkuu wa Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Al Azhar ambapo alitoa huduma kubwa. Kati ya hatua muhimu alizochukua Sheikh Shaltoot katika kipindi cha uongozi wake ni jitihada za kuimarisha umoja na mshikamano kati ya madhehebu za Kiislamu. Baada ya kuandikiana barua kadhaa na Ayatulahil Udhma Borujerdi aliyekuwa marjaa na kiongozi mkuu wa Waislamu wa madhehebu ya Shia, Sheikh Shaltut alitambua rasmi madhehebu ya Shia Ithnaashari. Aliamrisha madhehebu ya Shia yafunzwe katika Chuo Kikuu cha Al Azhar sawa na madhehebu zingine za Kiislamu. Aidha alitoa fatwa mashuhuri na kusema kuwa, inajuzu kwa Mwislamu yeyote kufuata madhehebu ya Shia Jaafariya. Sheikh Shaltoot aliaga dunia mwaka 1963 akiwa na umri wa miaka 72.

Sheikh Shaltoot   

Na miaka 17 iliyopita katika siku kama ya leo dikteta wa zamani wa Iraq alitiwa mbaroni akiwa katika maficho yake karibu na Tikrit huko kaskazini mwa Baghdad. Saddam alijificha katika eneo hilo baada ya Iraq kuvamiwa na majeshi ya Marekani na Uingereza mwezi Machi 2003. Kutiwa nguvuni dikteta huyo wa Iraq aliyemwaga damu za raia wengi wa nchi hiyo kuliwafurahisha sana Wairaki na nchi kama vile Iran na Kuwait ambazo zimepatwa na maafa makubwa kutokana na udhalimu za Saddam Hussein dhidi ya nchi hizo. Katika upande mwingine, pamoja na kuwa walimwengu walikuwa wakisubiri kwa hamu kusikia jinai zilizotendwa na dikteta huyo wa zamani wa Iraq wakati wa utawala wake, Marekani ilimweka dikteta huyo chini ya uangalizi wake baada ya kumtia nguvuni lengo likiwa ni kuzuia kufichuliwa ushirikiano wa karibu uliokuwapo kati ya dikteta huyo na serikali za Magharibi khususan ikulu ya Rais wa Marekani, White House.  

Saddam akiwa mahakamani