Dec 20, 2020 02:48 UTC
  • Jumapili, Disemba 20, 2020

Leo ni Jumapili tarehe 5 Jamadil Awwal mwaka 1442 Hijria, inayosadifiana na tarehe 20 Disemba mwaka 2020 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1437 iliyopita, sawa na tarehe 5 Jamadil Awwal mwaka wa 5 Hijria, Bi Zainab (SA) binti mtukufu wa Imam Ali (AS) na Bibi Fatima (SA) alizaliwa. Bibi Zainab alikuwa mashuhuri miongoni mwa wananchi kutokana na maarifa na elimu kubwa aliyokuwanayo. Katika tukio la Karbala, Bi Zainab (SA) alisimama kidete na kukabiliana barabara na dhulma za watawala madhalimu na majahili wa zama hizo ili kutimiza malengo matukufu ya kaka yake, Imam Hussein (AS). Bi Zainab alipelekwa Sham pamoja na mateka wengine wa nyumba tukufu ya Mtume (saw) baada ya mapambano ya Imam Hussein (AS). Hotuba za Bi Zainab (SA) mbele ya majlisi ya Ibn Ziyad mtawala wa Kufa na huko katika ikulu ya Yazid bin Muawiya huko Sham zilikuwa na taathira kubwa katika kufichua dhulma na ukandamizaji wa Bani Umaiyya na kuonesha jinsi Watu wa Nyumba Tukufu ya Mtume walivyodhulumiwa. Ni vyema kuashiria hapa kuwa Iran ya Kiislamu inasherehekea siku za kuzaliwa Bi Zainab (AS) kama 'Siku ya Wauguzi'.

 

##########

Siku kama ya leo miaka 85 iliyopita, Sheikh Izzuddin Qassam ambaye alikuwa miongoni mwa viongozi wa harakati ya mapambano ya ukombozi wa wananchi wa Palestina dhidi ya uvamizi wa Wazayuni maghasibu na ukoloni wa Uingereza, aliuawa shahidi. Baada ya kukamilisha masomo yake ya awali huko Syria, Sheikh Qassam aliendeleza masomo yake katika Chuo Kikuu cha al Azhar huko Misri. Wananchi wa Palestina walianza mapambana dhidi ya mkoloni Mwingereza mwaka 1930 chini ya uongozi wa Sheikh Izzuddin Qassam. Hata hivyo baada ya kupita miaka kadhaa Wazayuni maghasibu walishirikiana na wakoloni wa Kiingereza na kumuuwa kigaidi kiongozi huyo wa harakati ya mapambano ya Palestina.

Sheikh Izzuddin Qassam

##########

Miaka 69 iliyopita katika siku kama ya leo, nchi ya Oman ilipata uhuru kufuatia makubaliano yaliyosainiwa kati ya nchi hiyo na Uingereza. Oman ina historia kongwe na hadi kabla ya kudhihiri Uislamu, nchi hiyo kuna wakati iliwahi kuwa chini ya mamlaka ya Iran. Nchi hiyo iliwekwa chini ya mamlaka ya Waislamu baada ya kuaga dunia Mtume Muhammad (saw). Karibu karne moja baadaye kundi la Khawarij lilianzisha ghasia na uasi huko Oman na kuitawala nchi hiyo kwa karne kadhaa. Baadaye Oman ikakoloniwa na Ureno na Waingereza.

Bendera ya Oman

##########

Na siku kama ya leo miaka 55 iliyopita, aliaga dunia John Steinbeck mwandishi wa riwaya wa Kimarekani baada ya kuishi kwa miaka 66. Alizaliwa mwaka 1902. Katika ujana wake Steinbeck alijishughulisha na kazi mbalimbali na hatimaye akaichagua taaluma ya uandishi. Mwandishi huyo alionesha kipaji cha hali ya juu alichokuwa nacho katika uwanja wa uandishi. Machungu ya Steinbeck katika maisha yake yalimuandalia uwanja wa kubainisha masaibu na machungu ya watu wasiojiweza katika maandishi na vitabuu vyake. Miongoni mwa vitabu vyake ni Travels with Charley, East of Eden, A Russian Jornal na Burning Bright.

John Steinbeck