Alkhamisi tarehe 21 Januari 2021
Leo ni Alkhamisi tarehe 7 Jamadithani 1442 Hijria sawa na tarehe 7 Januari 2021.
Miaka 917 iliyopita katika siku kama ya leo, arifu mkubwa wa Kiislamu Ainul Qudhaat Hamedani mwenye lakabu ya Abul Fadhl, aliuawa shahidi kwa kunyongwa huko Hamedam. Alikuwa fakihi, mwanafasihi, msomi na malenga mahiri. Ainul Qudhaat alizaliwa mwaka 492 Hijria. Msomi huyo katu hakuwa akiogopa kubainisha itikadi yake. Ni kutokana na misimamo yake hiyo thabiti ambapo mwaka 525 Hijria alitiwa mbaroni na kufungwa huko Baghdad. Baada ya muda alihamishiwa Hamedan na kunyongwa kando na shule yake. Miongoni mwa vitabu vya msomi huyo ni al Tamhiidat na Haqaiqul Qur’an.
Siku kama ya leo miaka 284 iliyopita tufani kubwa ililikumba eneo la Ghuba ya Bengali mashariki mwa India na kuua watu laki tatu. Tufani hiyo ilitambuliwa kuwa kimbunga kilichosababisha maafa makubwa zaidi katika eneo hilo.
Ghuba ya Bengali iko kaskazini mwa Bahari ya Hindi na kusini mwa Asia na ni miongoni mwa maeneo ambayo hukumbwa na mafuriko na vimbunga vya mara kwa mara vinavyosababisha maafa makubwa ya nafsi na mali.

Siku kama ya leo miaka 228 iliyopita Mfalme Louis XIV wa Ufaransa alinyongwa. Alichukua hatamu za uongozi mwaka 1774 na kuathiriwa mno na mkewe Marie-Antoinette. Mwaka 1789 wananchi wa Ufaransa walianzisha mapambano dhidi ya Mfalme Louis XIV kutokana na hali mbaya ya kiuchumi na kijamii na miaka mitatu baadaye serikali ya kifalme ilifutwa rasmi nchini Ufaransa. Hata hivyo kutokana na kuwa mfalme Louis alikuwa ameomba msaada wa nchi za kigeni kwa siri alituhumiwa kuwa amefanya uhaini na kuhukukiwa kifo. Watu kadhaa wa familia ya Mfalme Louis XIV akiwemo mkewe Marie-Antoinette pia walinyonwa.
Katika siku kama ya leo miaka 82 iliyopita yaani tarehe 19 Jamadut-Thani mwaka 1360 Hijria, aliaga dunia Ayatullah Abu Abdullah Zanjani mmoja wa maulama wakubwa wa Kiislamu. Alimu huyo aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 51 na kuzikwa mahala alipozaliwa yaani Zanjan kaskazini magharibi mwa Iran. Alijifunza elimu za fasihi, falsafa na itikadi akiwa kijana mdogo. Baadaye Ayatullah Zanjani alielekea Najaf Iraq kwa shabaha ya kujiendeleza zaidi kielimu. Historia ya Qur'ani, Historia ya Maisha ya Mtume Muhammad SAW na Adhama ya Hussein bin Ali ni baadhi tu ya vitabu vya Ayatullah Zanjani vyenye thamani kubwa.
Siku kama ya leo miaka 42 iliyopita, inayosadifiana na tarehe Pili Bahman 1357 Hijria Shamsia, watu kadhaa waliuawa na wengine kujeruhiwa, baada ya kujitokeza mapigano ya barabarani kati ya wananchi wa Iran na vikosi vya utawala wa Kifalme hapa nchini. Wananchi Waislamu wa Iran walikuwa kwenye maandalizi ya kumpokea Imam Khomeini. Wananchi wa matabaka mbalimbali kutoka mijini na vijijini walikuja mjini Tehran kwa shabaha ya kumlaki Imam Khomeini akitokea uhamishoni nchini Ufaransa. Wakati harakati hiyo ya wananchi ikiendelea, maafisa wasiopungua elfu nne wa Jeshi la Anga, walionyesha uungaji mkono wao kwa wananchi, na kutangaza mgomo wa kula chakula, sanjari na kutaka washauri wa Kimarekani waliokuwepo hapa nchini waondoke haraka iwezekanavyo.