Jumanne tarehe 26 Januari 2021
Leo ni Jumanne tarehe 12 Jamadithani 1442 Hijria sawa na tarehe 26 Januari 2021.
Miaka 799 iliyopita katika siku kama ya leo, alifariki dunia Abul Hassan Ali bin Abdu Samad Hamdani, mtambuzi wa lugha, fakihi na mfasiri wa Qur'ani katika karne ya 7 Hijria. Alizaliwa huko Sakha katika viunga vya Misri na akaondokea kuwa mashuhuri kwa lakabu ya Sakhawi. Akiwa na lengo la kujiendeleza kielimu, Abul Hassan Ali bin Abdu Samad alielekea Sham na kuishi Damascus katika Syria ya leo. Msomi huyo wa Kiislamu ameandika vitabu mbalimbali katika elimu za Tajweed, teolojia na hadithi. Baadhi tu ya vitabu vyake mashuhuri ni pamoja na al Jawahir na Sifrus Sa'ada.

Siku kama ya leo miaka 198 iliyopita, yaani mwaka 1823, alifariki dunia Edward Jenner tabibu wa Kiingereza aliyegundua chanjo ya ndui yaani (smallpox). Jenner alizaliwa mwaka 1749 Miladia. Tabibu huyo alifanikiwa kugundua chanjo ya ndui akiwa na umri wa miaka 45 wakati alipoelekea nchini India. Kuanzia hapo ugonjwa huo wa ndui uliweza kutibiwa kwa kutumia chanjo hiyo. Na ilipofika mwaka 1979 maradhi hayo yalitokomezwa kabisa duniani.
Siku kama ya leo miaka 71 iliyopita, Mfumo wa Jamhuri ulitangazwa nchini India na siku hii ikapewa jina la Siku ya Kitaifa ya India. Baada ya India kupata uhuru kutoka kwa mkoloni Muingereza Jawaharlal Nehru alichaguliwa kuwa Waziri Mkuu huku Rajendra Prasad akichaguliwa kuwa Rais wa kwanza wa nchi hiyo. Kwa mujibu wa mfumo wa India, wadhifa wa urais ni wa kiheshima tu na Waziri Mkuu ndiye mtendaji mkuu wa shughuli za serikali.
Katika siku kama ya leo miaka 25 iliyopita aliaga dunia Ayatullah Sayyid Abdul Aziz Tabatabai Yazdi. Alizaliwa mwaka 1348 Hijria katika mji mtakatifu wa Najaf huko Iraq na kupata elimu kwa wanazuoni wakubwa wa mji huo akiwemo Atayullah Sayyid Abdul Aala Musawi Sabzavari, Sheikh Sadra Badkubeh na Sayyid Abul Qassim al Khui. Alielekea katika mji mtakatifu wa Qum nchini Iran mwaka 1354 Hijria Shamsia na kujishughulisha na kazi za uandishi na uhakiki. Alkuwa miongoni mwa wataalamu mashuhuri na wakubwa wa historia, hadithi na Ilmu rijali na amefanya kazi kubwa ya kutayarisha faharasa ya Maktaba Kuu ya Haram ya Imam Ridhaa (as) katika mji mtakatifu wa Mahs'had na Maktaba ya Amirul Muuminin katika mji wa Najaf. Ayatullah Abdul Aziz Tabatabai Yazdi ameandika makumi ya vitabu vikiwemo vya Adhwaa A'ala al Dhari'a na al Mahdi fii al Sunna Annabawiyyah.
Na siku kama ya leo miaka 18 iliyopita, alifariki dunia mtaalamu wa masuala ya Kiislamu wa Ujerumani, Bi Annemarie Schimmel. Bibi Schimmel alipendelea mno kutalii na kupata maarifa kuhusu ustaarabu wa Kiislamu na alipata shahada ya uzamivu katika taaluma ya masuala ya Kiislamu katika Chuo Kikuu cha Berlin akiwa na umri wa miaka 19. Prof. Annemarie Schimmel alifundisha kwa miaka mingi historia ya dini na irfani ya Kiislamu katika vyuo vikuu vya Marekani, Ujerumani na Uturuki. Mbali na kujua lugha za Kijerumani na Kiingereza, Bi Schimmel alijifunza pia lugha za Kiarabu, Kifarsi, Kiurdu, Kibengali na Kituruki kwa ajili ya kupata maarifa zaidi kuhusu masuala ya Kiislamu. Prof. Annemmarie Schimmel ameandika vitabu kadhaa kuhusu masuala ya Kiislamu ikiwa ni pamoja na kile cha "Muhammad, Mtume wa Mwenyezi Mungu" na "Mwanamke katika Irfani ya Kiislamu."