Ijumaa, 5 Februari, 2021
Leo ni Ijumaa tarehe 22 Mfunguo Tisa Jamadithani mwaka 1442 Hijria sawa na tarehe Tano Februari 2021 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1051 iliyopita sawa na tarehe 22 Jamadithani mwaka 391 Hijria kwa mujibu wa riwaya mbalimbali alifariki dunia malenga wa Kiislamu kwa jina la Ibn Hajjaj. Ibn Hajjaj alizaliwa mjini Baghdad, Iraq na alijikita katika taaluma ya mashairi akiwa bado kijana na kutokea kuwa maarufu katika uwanja huo. Alitunga mashairi mengi yanayowaenzi na kuwasifu Ahlul bait wa Mtume (saw) na kuwashambulia wapinzani wa Uislamu na Mtume. Miongoni mwa athari za malenga huyo ni pamoja na diwani ya mashairi yenye juzuu kumi inayohifadhiwa katika maktaba mbalimbali duniani.***
Katika siku kama ya leo miaka 140 iliyopita alifariki dunia mwanahistoria, mwanafalsafa na mtaalamu mashuhuri wa masuala ya mashariki wa Scotland, Thomas Carlyle. Mwanafalsafa huyo alizaliwa mwaka 1795 katika familia ya watu wa kijijini na mbali na lugha ya Kijerumani, alijifunza pia lugha ya Kiarabu na baadaye alianza kufunza lugha hiyo katika Chuo Kikuu cha Cambridge,London. Katika safari zake nyingi katika nchi za Kiislamu, mwanahistoria huyo alijifunza utamaduni na ustaarabu wa Kiislamu na kuathirika mno na dini hiyo. Thomas Carlyle anasema kuhusu Qur'ani kwamba: "Qur'ani ni sauti isiyokuwa na wasita kutoka kwenye roho ya ulimwengu, na wanadamu wanapaswa kuisikiliza, la sivyo hawapaswi kusikiliza maneno mengineyo." Mwanafalsafa huyo wa Scotland anasema kuhusu Mtume Muhammad (SAW) kwamba: Mwenyezi Mungu amemfunza hikima na elimu shakhsia huyu adhimu. Alijiepusha na kupenda jaha na ni miongoni mwa watu waliotakaswa na kupendwa mno na Mola Muweza."***
Miaka 42 iliyopita katika siku kama ya leo kufuatia kutangazwa kuundwa serikali ya muda ya Mapinduzi nchini Iran, mamilioni ya wananchi Waislamu na Wanamapinduzi wa Iran waliandamana katika miji mbalimbali nchini ili kuuunga mkono na kuidhinisha uamuzi huo wa Imamu Khomeini (M.A). Katika siku hiyo wananchi Waislamu wa Iran walimiminika kwenye mitaa mbalimbali na kwa sauti moja wakitaka kuondoka madarakani serikali kibaraka ya Bakhtiyar. Siku hiyo hiyo pia Jenerali Huyser (inasomwa Haizer) Mjumbe Maalumu wa Marekani ambaye alitumwa Tehran ili kusaidia kuubakisha madarakani utawala wa Pahlavi na kutangaza uungaji mkono wa Marekani kwa makamanda wa jeshi la Shah na kuandaa uwanja wa kujiri mapinduzi dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu hatimaye alirejea nchini kwake mwezi mmoja baada ya kufeli jitihada zake hizo katika uwanja huo. ***