Feb 09, 2021 04:11 UTC
  • Jumanne tarehe 9 Februari 2021

leo ni Jumanne tarehe 26 Jamadithani 1442 Hijria inayosadifiana na tarehe 9 Februari mwaka 2021.

Siku kama ya leo miaka 1434 iliyopita vita vya Dhatus Salasil vilimalizika kwa Waislamu kujipatia ushindi. Vita hivyo vilianza baada habari kusambaa kuwa kikundi cha washirikina kilitaka kushambulia mji wa Madina. Baada ya habari hiyo kumfikia Mtume Mtukufu (saw), aliwaamuru baadhi ya Waislamu waenda kukabiliana na washirikina hao wakiongozwa na kamanda mmoja aliyetoka upande wa Muhajirina. Hata hivyo baada ya kujua uwezo mkubwa waliokuwa nao maadui, kundi hilo la Waislamu lilirejea. Mtume alimtuma kamanda mwingine lakini naye pia alirejea na ndipo Mtume Mtukufu (s.a.w) alipomteua Ali bin Abi Twalib (a.s) aongoze Waislamu katika mapigano hayo. Imam Ali (as) aliwashambulia maadui kwa umahiri mkubwa na kurejea Madina na ushindi.

Siku kama ya leo miaka 65 iliyopita, Abbas Iqbal Ashtiyani, mhakiki, mwandishi, mtambuzi wa lugha na mwanahistoria wa zama hizi wa Kiirani alifariki dunia. Alizaliwa mwaka 1275 Hijria Shamsia na baada ya kuhitimu masomo yake ya awali nchini Iran mwaka 1304 alifanikiwa kupata shahada ya Uzamili katika Chuo Kikuu cha Sorbonne cha Ufaransa. Ashtiyani alirejea hapa nchini na kuanza kufundisha katika Chuo Kikuu cha Tehran.

Abbas Iqbal

Katika siku kama ya leo miaka 42 iliyopita majenerali wa utawala wa Shah waliongeza muda wa serikali ya kijeshi katika mji wa Tehran. Majenerali hao walichukua hatua hiyo ili kuwazuia wananchi kuwaunga mkono na kuwasadia wanajeshi wa kikosi cha anga ambao walikuwa wakishambuliwa na kikosi cha gadi ya Shah, na kwa njia hiyo waweze kumtia mbaroni Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu pamoja na shakhsiya wengine muhimu waliokuwa katika harakati za Mapinduzi au kuwauwa. Lakini Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa kuona mbali na kusoma vyema nyakati, aliwatolea mwito wananchi kupuuza kizuizi hicho kilichowekwa na majenerali wa Shah cha kuongeza muda wa serikali ya kijeshi au sheria za kutotoka nje. Wananchi wanamapinduzi wa Iran pia waliitikia agizo hilo la Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu na kumininika katika mitaa mbalimbali na kueneza mapambano yao katika vituo vingine vya kijeshi vya utawala wa kidikteta wa Shah katika mji wa Tehran na miji mingineo.

Na siku kama ya leo miaka 29 iliyopita, baada ya Chama cha Wokovu wa Kiislamu cha Algeria (FIS) kupata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa Bunge, wanajeshi waliokuwa wakitawala nchini humo, walibatilisha matokeo ya uchaguzi huo na kukipiga marufuku chama hicho, hali iliyopelekea kuzuka machafuko makubwa. Machafuko hayo yalipelekea kuuawa watu wengi nchini Algeria.

 

Tags