Mchango wa Maulamaa wa Kishia (19) +SAUTI
Ahlan Wasahlan wapenzi wasikilizaji na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu, ambacho huwatambulisha na kuwazungumzia Maulamaa wakubwa wa Kishia, mchango wao katika Uislamu pamoja na vitabu na athari zao.
Kipindi chetu kilichopita kilizungumzia Radhiuddin Ali bin Mussa bin Jaafar mashuhuri kwa jina la Sayyid Ibn Tawus alimu na msomi wa Kishia aliyeIshi katika zama za utawala wa Mongolia. Aidha tulieleza kuwa, alimu huyu ameandika vitabu vingi ambapo miongoni mwa vitabu vyake hivyo ni: Misbahul Al-Mujtahid, Muhaasabatun Nafs na Iqbaalul A’mal. Hata hivyo kitabu mashuhuri zaidi cha msomi huyu ni al-luhuf alaa Qatla al-Tufuf. Sehemu ya 19 ya mfululizo huu juma hili, itamzungumzia Khajeh Nasir al-Din Tusi mmoja wa wanazuoni na wasomi wakubwa wa Kishia katika karne ya 7 Hijria ambaye kiasili ni Muirani. Kuweni nami hadi mwisho wa dakika hizi chache.
Zama za kuanza kipindi cha Ghaibatul Kubra 'Ghaiba Kubwa' kilikwenda sambamba na kuanza zama za mafakihi wabeba bendera kwa niaba ya Imam Mahdi ATFS kwa minajili ya kutetea na kulinda hukumu, sheria na matukufu ya Uislamu na Ushia. Kuanzia wakati huo hadi leo, Maulamaa wa Kiislamu walitumia uwezo wao wote katika njia hii ya panda shuka na kutekeleza majukumu yao kwa njia mbalimbali.

Kila mahala walipoona kuna haja na ulazima, basi walijitokeza na kutumia silaha ya kalamu, maneno, kualifu vitabu na kueneza mafundisho na maarifa ya Uislamu. Aidha ilipolazimu hawakusita hata kutoa mali, uhai na heshima yao katika njia hiyo. Baina yao, walikuwemo wasomi waliokuwa na vipawa ambao walijumuisha elimu na amali na dini na siasa na kuwa na mchango mkubwa na usio na kifani katika tufani na misukosuko ya dunia na kufanikiwa kuifikisha katika ufukwe meli ya utamaduni na ustaarabu wa Kiislamu wa Kishia. Miongoni mwa sakhsia hao wakubwa ni Khajeh Nasir al-Din Tusi ambaye ni mmoja wa maulamaa wakubwa wa Kishia aliyeishi katika karne ya 7 Hijria. Msomi huyo alikuwa amebobea katika elimu mbalimbali na kuwa na mitazamo na nadharia za kuzingatiwa katika taaluma nyingi.
Muhammad bin Muhammad ni Hassan Toosi mashuhuri kwa jina la Khajeh Nasir al-Din Toosi, alikuwa mwanafalsafa, mwanateolojia, fakihi, mwanahisabati na mnajimu mkubwa wa Kiirani katika karne ya 7 Hijria. Mwanazuoni huyo aliasisi kituo kikubwa cha kielimu na akademia ya kwanza ya sayansi yaani mahala pa kuangalilia mwenendo wa nyota, mwezi na jua iliyojulikana kwa jina la Maraghe huko kaskazini magharibi mwa Iran. Alimu huyo aligundua namna mpya za kutumia saa ya jua kwa ajili ya kituo hicho. Kituo hicho kilikuwa na suhula muhimu zaidi ambazo kwa miaka 300 baada ya hapo hazikuweza kushuhudiwa katika nchi za Magharibi. Wasomi wakubwa kama Allama Hilli na Qutub al-Din Shirazi alikulia na kuleleka katika maktaba yake. Khajeh Nasir al-Din Tusi alizaliwa mwaka 597 Hijria katika mji wa Tusi kaskazini mashariki mwa Iran. Baba yake Muhammad bin Hassan alikuwa katika orodha ya mafakihi wa Kishia na wataalamu wakubwa wa elimu ya hadithi katika mji wa Tusi.
Nasir al-Din Tusi alikipitisha kipindi cha masomo yake ya msingi kando ya baba, mama na mjomba wake na baada ya hapo akaanza kuhudhuria darsa na vikao vya kielimu vya wasomi na wanazuoni watajika wa zama hizo katika mji wa Tusi. Alikuwa na kiu kali na bidii kubwa ya kusoma na kujiendeleza; na historia inaonyesha kuwa, alikuwa na kipaji cha ajabu ambacho kiliwashangaza walimu wake. Shakhsia wakubwa wa zama hizo katika mji wa Tusi walimshauri Nasir al-Din Tusi ahajiri na kwenda Neishabour kwa ajili ya kujiendeleza zaidi kimasomo.

Huu ndio uliokuwa mwanzo wa safari za kielimu za Nasir al-Din Tusi. Baadaye alielekea katika miji ya Rey, Qum na Isfahan na kisha akaelekea nchini Iraq. Hatimaye msomi huyo alibobea katika taaluma za fikihi, falsafa, teolojia, hisabati na nujumu baada ya kufikia daraja za juu kabisa za masomo katika elimu hizo. Ni kipindi hicho ndipo alipoamua kurejea mahapa alipozaliwa.
Hata hivyo akiwa Khorasan, Khajeh Nasir al-Din Tusi hakuweza kufikia utulivu alioukusudia wa kufanikisha malengo na mapenzi yake ya kielimu, kwani zama hizo zilisadifiana na hujuma na mashambulio ya utawala wa Mongolia dhidi ya Iran. Mongolia iliwaua kikatili wananchi wengi wa Iran na kufanya uharibifu mkubwa usio na maelezo. Kaumu hiyo isiyo na utamaduni na ambayo haikuwa ikithamini utamaduni na ustaarabu wa mwanadamu iliharibu na kuchoma moto kila ilichokiona kuwa ni kikwazo katika kufikia malengo yake.
Nasir al-Din Tusi alikuwa msomi aliyekamilika na kubobea katika nyanja zote. Licha ya kuwa katika uga wa siasa alikuwa mahiri pia na hata kuwa na taathira katika mustakabali na hatima ya Ulimwengu wa Kiislamu, lakini shakhsia yake haikuathirika katu na siasa. Msomi huyo ameacha athari nyingi za kielimu hususan hisabati na nujumu ambazo mpaka kufikia karne ya saba Hijria zilikuwa zimetarjumiwa na zikifundishwa huko barani Ulaya.
Kwa hakika tunaweza kuitaja karne ya saba Hijria kuwa, kipindi cha kweli cha uandishi na kualifu vitabu na athari za kielimu katika uga wa teolojia ya Kishia. Katika zama hizo, Khaje Nasir al-Din Tusi ndiye aliyekuwa kinara wa duru hiyo. Miongoni mwa vitabu vyake ambavyo viliweka wazi na kubainisha haki ya Ushia ni Tajrid al-Aqaid, Fusul al-Aqaid na Qawaid al-Aqaid. Baadhi ya vitabu vyake hivyo hususan kile cha Tajrid al-Aqaid kilikusanya majimui ya rai na mitazamo ya kiitikadi ya Kishia.
Mwanazuoni huyo amefanya kazi kubwa na huduma isiyo na kifani pia katika uga wa falsafa. Aidha katika uwanja wa elimu ya akhlaq na tabia njema, mwangwi wa sauti ya juhudi zake unasikika vyema. Mitazamo yake kuhusiana na akhlaq na malezi inashuhudiwa zaidi katika vitabu vyake vya Akhlaq Nasiri na A'dab al-Mutaalimina.

Miongoni mwa huduma nyingine alizofanya Khajeh Nasir al-Din Tusi ambayo historia katu haiwezi kuisahau ni kuasisi kituo kikubwa cha kielimu na akademia ya kwanza ya sayansi yaani mahala pa kuangalilia mwenendo wa nyota, mwezi na jua iliyojulikana kwa jina la Maraghe huko kaskazini magharibi mwa Iran. Alimu huyo aligundua namna mpya za kutumia saa ya jua kwa ajili ya kituo hicho.
Kwa ajili ya kusaidia kituo hicho mbali na misaada ya kifedha ya serikali, asasi mbalimbali za waqfu katika maeneo mbalimbali nchini Iran wakati huo, zilimsadia Khaje Nasir al-Din Tusi. Eneo hilo halikuwa mahala pa kuangalilia mwenendo wa nyota, mwezi na jua tu, bali Maraghe kilikuwa kituo kikubwa cha kielimu ambacho kilikuwa kikitumiwa kufundishiwa taaluma nyingi na wasomi na wanazuoni wakubwa na mashuhuri wa zama hizo kama Qutub al-Din Shirazi walikuwa wamekusanyika hapo.
Jirani na kituo cha kuangalilia mwenendo wa mwezi, jua na nyota cha Maraghe kulijengwa maktaba kubwa na yenye thamani kubwa ambapo ndani yake mlikuwa na jumla ya vitabu laki nne vyenye thamani kubwa. Nasir al-Din alivikusanya vitabu hivyo kutoka katika maeneo mbalimbali kama Baghdad, Sham, Beirut na Algeria.
Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu kwa leo umefikia tamati tukutane tena wiki ijayo ambapo tutatupia jicho sehemu nyingine ya huduma kubwa iliyotolewa na alimu na msomi huyu wa Kishia kwa ulimwengu wa Kiislamu.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh...