Wanaspoti wa Iran watwaa dhahabu Dubai Grand Prix
Wanaspoti wa Iran watwaa dhahabu Dubai Grand Prix
Wanariadha nyota wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wameendelea kuzoa medali kochokocho katika Mashindano ya Riadha ya Walemavu ya Dubai Grand Prix katika Umoja wa Falme za Kiarabu.
Siku ya Ijumaa, Mahdi Moradi aliishindia nchi hii medali ya dhahabu baada ya kuibuka kidedea katika mashindano ya kuruka ya Long Jump T/F13 kwa upande wa wanaume kwa kuruka umbali wa mita 6.57. Mkazaki na Mchina walitwaa nafasi ya pili na tatu kwa usanjari huo katika kitengo hicho. Ijumaa hiyo pia, Muirani mwigine, Mahdi Olad aliipa nchi hii medali nyingine ya dhahabu katika mchezo wa kurusha kisahani (Discus) baada ya kukirusha umbali wa mita 39.06 katika siku ya tatu ya mashindano hayo. Nafasi za pili na tatu ziliwaendea Mrussia na raia wa Uzbekistan. Iran iliyaanza mashindano hayo vizuri siku ya Jumatano, baada ya kuondoka uwanjani wa medali tatu za dhahabu, fedha na shaba katika michezo mitatu tofauti. Muirani Hamed Amiri alitwaa medali ya dhahabu ya kuibuka mshindi katika mchezo wa kurusha mkuki (Javelin) baada ya kuurusha umbali wa mita 30.96 katika kategoria ya F54. Saman Pakbaz alitwaa medali ya fedha katika mchezo wa kurusha tufe (shot put) kategoria ya F12 huku Vahid Alinajimi walitwaa medali ya shaba mbio za mita 100 kitengo cha T13. Mashindano hayo ya kimataifa yanayofahamika kwa Kiingereza kama Dubai 2021 World Para Athletics Grand Prix yalianza Jumatano ya Februari 10 na yanatazamiwa kufunga pazia lake Februari 16 huko Dubai, UAE. Mashindano hayo ambayo yamewaleta pamoja wanariadha 600 kutoka nchi 63 duniani, ni moja ya michuano saba ya kufuzu Michezo ya Olimpiki ya Tokyo Japan mwaka huu kwa upande wa walemavu.