Jul 01, 2021 02:24 UTC
  • Alkhamisi tarehe Mosi Julai 2021

Leo ni Alkhamisi tarehe 20 Dhulqaada 1442 Hijria sawa na tarehe Mosi Julai 2021.

 Miaka 986 iliyopita katika siku kama ya leo sawa na tarehe 20 Dhulqaada mwaka 456 alifariki dunia Abu Ali Qirawani, mshairi, mwanafasihi na mkosoaji wa fasihi wa Morocco. Mshairi huyo aligundua muundo mpya wa kukosoa kazi za fasihi na kuacha athari nyingi katika uwanja huo.

Siku kama ya leo miaka 233 iliyopita alizaliwa Jean Victor Poncelet mwasisi wa uchambuzi wa maumbo. Victor Poncelet aliyekuwa mtaalamu maarufu wa hisabati wa Ufaransa, alitambulika kuwa mwasisi wa uchambuzi wa maumbo. Poncelet alikuwa mmoja wa maafisa wa jeshi la Napolione na alitekwa nyara na Warusi wakati jeshi la Ufaransa lilipokuwa likirejea nyuma kutoka Urusi ya zamani. Hata hivyo katika kipindi cha kutekwa alijiendeleza kielimu na kukamisha elimu yake ya uhandisi. Jean Victor Poncelet alifariki dunia tarehe 22 Disemba 1867. 

Jean Victor Poncelet

Siku kama ya leo miaka 154 iliyopita, nchi ya Canada ilijitangazia uhuru kutoka kwa mkoloni Mwingereza. Canada iligunduliwa mwishoni mwa karne ya 15 Miladia na kuanzia wakati huo kwa zaidi ya karne mbili, Uingereza na Ufaransa zilikuwa zikishindana katika ardhi ya nchi hiyo kwa lengo la kupanua udhibiti wao. Ushindani huo ulipelekea kujiri vita kati ya mataifa hayo ya kikoloni ambapo mwaka 1689 vita hivyo vilidumu kwa karibu miaka 75 vilimalizika kwa kushindwa Ufaransa. Kuanzia mwanzoni mwa karne ya 19 taratibu zilianza harakati za kupigania uhuru wa Canada ambazo zilizaa matunda mwaka 1867 katika siku kama ya leo.

Bendera ya Canada

Miaka 61 iliyopita katika siku kama ya leo, sehemu mbili za Somalia ya Uingereza na ya Italia ziliungana na kuunda nchi moja ya Somalia yenye kujitawala. Karne kadhaa nyuma, Somalia iliwahi kujitawala kwa kipindi kifupi. Mwaka 1884 Uingereza iliiweka katika himaya yake sehemu ya ardhi ya nchi hiyo. Miaka mitano baadaye Italia nayo ikakoloni baadhi ya sehemu za Somalia. Harakati za mapambano za Muhammad Abdullah Hassan dhidi ya Waingereza kuanzia mwaka 1901 hadi 1920 hazikuzaa matunda. Mwaka 1950 Umoja wa Mataifa uliitaka Italia iandae mazingira ya kujitawala na kuwa huru nchi ya Somalia.

Somalia

Katika siku kama ya leo miaka 59 iliyopita, nchi ndogo ya Burundi ilijitangazia uhuru wake. Kuanzia mwaka 1899 hadi 1917 Burundi pamoja na Rwanda ilikuwa sehemu ya makoloni ya Mjerumani huko Afrika Mashariki. Baada ya Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia na kushindwa Ujerumani katika vita hivyo, Umoja wa Mataifa uliikabidhi Ubelgiji ardhi ya Burundi. Mwaka 1962 Burundi ilipata uhuru ikiwa na mfumo wa utawala wa kifalme. Hata hivyo miaka minne baadaye wapigania jamhuri walimuondoa madarakani mfalme na kuanzisha mfumo wa serikali ya jamhuri. 

Bendera Burundi

Na siku kama ya leo miaka 59 iliyopita, Rwanda ilipata uhuru. Rwanda ina historia inayofanana na jirani yake wa kusini yaani Burundi ambapo kabla ya nchi hizo kujitangazia uhuru zilikuwa zikikoloniwa na Ubelgiji. Baada ya mapambano mtawalia ya wapigania uhuru wa Rwanda, hatimaye mnamo mwaka 1962, nchi hiyo ilipata uhuru na kabila kubwa la Wahutu likashika hatamu za uongozi wa nchi. Mwaka 1973, Meja-Jenerali Juvenal Habyarimana alichukua madarakani baada ya kufanya mapinduzi yasiyo na umwagaji damu. Hata hivyo mwaka 1994 kulitokea mauaji ya kimbari ambapo zaidi ya watu laki 8 waliuawa wengi wao wakiwa ni wa kabila la Tutsi.

Bendera ya Rwanda