Aug 22, 2021 03:46 UTC
  • Jumapili, 22 Agosti, 2021

Leo ni Jumapili tarehe 13 Muharram 1443 Hijria Qamaria ambayo inasadifiana na tarehe 22 Agosti 2021 Miladia.

Tarehe 13 Muharram mwaka wa 61 Hijria yaani siku kama hii ya leo miaka 1382 iliyopita Abdullah bin Afif aliuawa shahidi na gavana wa Yazid bin Muawiya, Ubaidullah bin Ziad. Afif alikuwa mtu wa kwanza kuanzisha malalamiko na upinzani wa wazi wazi dhidi ya jinai za Ubaidullah bin Ziad za kumuua shahidi mjukuu wa Mtume (saw), Imam Hussein (as). Baada ya Ubaidullah bin Ziyad kuwashambulia kwa maneno makali na kuwavunjia heshima mateka wa Karbala waliokuwa wamepelekwa katika majlisi yake, Abdullah bin Afif ambaye alikuwa miongoni mwa wachamungu wakubwa wa mji wa Kufa huko Iraq na wafuasi wa kweli wa Amirul Muuminin Ali bin Abi Twalib (as), alikerwa mno na mwenendo huo wa gavana wa Yazidi wa kuwavunjia heshima Watu wa Nyumba ya Mtume (saw) na kumjibu mtawala huyo kwa hasira. Ubaidullah ambaye hakutarajia kuona majibu kama hayo baada ya kuua watu wa Nyumba ya Mtume (saw) alitoa amri ya kukamatwa Afif na kupelekwa kwake. Hata hivyo watu wa kabila lake walizuia kitendo hicho. Askari wa utawala wa Bani Umayyah walivamia nyumba ya Abudullah bin Afifi usiku na kumtoa nje kisha wakamuua shahidi kwa kumkata kwa mapanga. 

 

 

Katika siku kama ya leo miaka 394 iliyopita vilijiri vita vya mwisho vya La Rochelle kati ya Wakatoliki na Waprotestanti wa Ufaransa. Vita hivyo vilianza baada ya Waprotestanti kuchochewa na Uingereza. Wakatoliki ambao walikuwa wakiungwa mkono na vikosi vya jeshi la serikali ya Ufaransa chini ya uongozi wa Richelieu, Kansela mashuhuri wa nchi hiyo, walipigana vita na Waprotestanti ambao walikuwa wakipigania maeneo yao katika bandari ya La Rochelle. Vita hivyo vilimalizika baada ya mwaka mmoja kwa kupata ushindi Wakatoliki na kutekwa La Rochelle. ***

Miaka 323 iliyopita katika siku kama ya leo, mkataba wa pande tatu wa Russia, Poland na Denmark ulitiwa saini dhidi ya Sweden. Wafalme wa nchi hizo tatu walikuwa na lengo la kumuangusha Sharel XII mfalme kijana wa Sweden ili kuikalia kwa mabavu nchi hiyo. Ni kwa msingi huo ndipo miaka miwili baadaye mnamo mwezi Aprili mwaka 1700 Miladia nchi wanachama wa mkataba huo wa pande tatu zikaamua kuishambulia Sweden, hata hivyo jeshi la mfalme Sharel XII likakabiliana vilivyo na kutoa pigo kwa nchi vamizi.  Baada ya kufikia mapatano na Denmark, mwaka 1704 akaishambulia Poland na kuikalia kwa mabau. Hata hivyo mashambulio ya Sharel dhidi ya Russia hayakuzaa matunda. ***

Sharel XII

 

Siku kama ya leo miaka 161 iliyopita Paul Gottlieb Nipkow mmoja wa wavumbuzi wa televisheni alizaliwa huko Ujerumani. Nipkow alikulia katika familia maskini, lakini juhudi na irada kubwa ilimuwezesha kuendeleza masomo yake ya fizikia hadi chuo kikuu. Paul Gottlieb Nipkow alifanya utafiti mkubwa na hatimaye alifanikiwa kuvumbua transimita ya televisheni. Chombo hicho kilichobuniwa na Nipkow kiliweza kurusha mawimbi ya televisheni katika umbali wa mita 30 na baadaye transimita iliyotengenezwa na mvumbuzi huyo wa Kijerumani ilikamilishwa na wabunifu wengine. ***

 

Miaka 157 iliyopita katika siku kama hiii ya leo, mkataba wa kihistoria wa Geneva ulitiwa saini baina ya nchi kadhaa za Ulaya, Asia na Amerika. Lengo la mkataba huo lilikuwa ni kuwasaidia majeruhi katika medani za vita.  Kwa mujibu wa mkataba huo, timu za madaktari, watoaji misaada na zana zao zinapaswa kutoegemea upande wowote na zisishambuliwe bali zibakie katika amani wakati wa vita. Mbunifu wa mkataba huo alikuwa Henry Dunant raia wa Uswisi. *