Jumamosi, 28 Agosti, 2021
Leo ni Jumamosi tarehe 19 Mfunguo Nne Muharram 1443 Hijria sawa na tarehe 28 Agosti 2021 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1382 iliyopita, msafara wa mateka wa Karbala uliokuwa na familia ya mjukuu wa Mtume, Imam Hussein (as) na mashahidi wengine waliouawa na utawala wa Yazid bin Muawiya katika medani ya Karbala uliondoka Kufa nchini Iraq ukielekea Damascus, makao makuu ya serikali ya Bani Umayyah. Msafara huo hususan Imam Zainul Abidin na Bibi Zainab binti Ali bin Abi Twalib (as) ulifichua na kuanika maovu ya Yazid bin Muawiyyah na kuwafanya watu wa Kufa wajute sana kwa kumuacha peke yake mjukuu wa Mtume (saw), Imam Hussein katika mapambano ya Karbala. Watu wa mji wa Kufa walisikitika sana kutokana na kumwacha peke yake mjukuu huyo wa Mtume na wasiwasi ulizuka juu ya uwezekano wa kuanza harakati ya wananchi dhidi ya utawala wa Yazid mjini humo. Kwa msingi huo mtawala wa Kufa, Ubaidullah bin Ziyad, alikhitari kutuma wajukuu hao wa Mtume wetu Muhammad (saw) huko Sham kwa mtawala dhalimu Yazid bin Muawiyyah wakitanguliwa na kichwa kilichotenganishwa na mwili cha Bwana wa Vijana wa Peponi, Imam Hussein (as). ***
Tarehe 28 Agosti 1749, miaka 272 iliyopita alizaliwa Johann Wolfgang Von Goethe malenga na mwandishi mkubwa wa Kijerumani. Von Goethe alisoma na kujifunza mambo mbalimbali kama uchoraji na kadhalika katika mji aliozaliwa wa Frankfurt nchini Ujerumani, huku akiendelea na masomo yake ya taaluma ya sheria. Von Goethe ambaye anahesabiwa kuwa mmoja kati ya waenezaji wa fasihi ya lugha ya Kifarsi, alivutiwa mno na fasihi ya Kifarsi na hasa mashairi ya Hafidh, malenga na mshairi mashuhuri wa Kiirani. Mwandishi huyo wa Kijerumani alikipenda sana Kitabu Kitakatifu cha Qur'ani pamoja na dini ya Kiislamu. Johann Wolfgang Von Goethe alifariki dunia mwaka 1832. ***
Siku kama ya leo miaka 64 iliyopita kombora la kwanza la kuvuka mabara lilirushwa hewani na wasomi wa Urusi ya zamani. Siku nne baadaye yaani tarehe 4 Oktoba wasomi wa Urusi walirusha angani satalaiti ya kwanza dunia iliyopewa jina la Sputnik-1kwa kutumia kombora hilo. Hatua hiyo ilipongezwa kote dunia, na wasomi hao walitangaza kuwa watatuma mwanadamu angani katika kipindi cha chini ya miaka mitatu na kwamba watatuma chombo cha anga katika mwezi miaka mitano baadaye. Wasomi hao wa Urusi walitimiza hadi zao.***

Na miaka 28 iliyopita katika siku kama ya leo, kulitiwa saini mkataba wa amani baina ya Yassir Arafat, kiongozi wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina PLO na Yitzhak Rabin, Waziri Mkuu wa wakati huo utawala haramu wa Israel. Bill Clinton baada ya kuchaguliwa kuwa Rais wa Marekani mwaka 1992, aliliweka katika vipaumbele vyake katika sera za kigeni, suala la amani ya Mashariki ya Kati na kupatikana maridhiano baina ya Waarabu na Israel. Baada ya mazungumzo, hatimaye mkataba huo ulitiwa saini katika siku kama ya leo. Kwa mujibu wa mkataba huo, Harakati ya Ukombozi wa Palestina PLO iliutambua rasmi uwepo wa utawala haramu wa Israel; na Israel nayo ikaahidi kuwapatia Wapalestina usimamizi wa sehemu ya maeneo yanayokaliwa kwa mabavu ukiwemo Ukanda wa Gaza. Mkataba huo ulipingwa vikali na Wapalestina. Makundi na harakati mbalimbali za mapambano huko Palestina ziliutaja mkataba huo kama hiana na usaliti kwa malengo matukufu ya Palestina. Licha ya mkataba huo, Israel haikutekeleza ahadi zake na miaka iliyofuata Wazayuni waliendeleza hujuma na uvamizi wao huko Palestina. ***
