Jumanne tarehe 21 Septemba 2021
Leo ni Jumanne tarehe 14 Safar 1443 Hijria sawa na Septemba 21 mwaka 2021.
Katika siku kama ya leo miaka 811 iliyopita sawa na tarehe 14 Safar mwaka 632 Hijria alifariki dunia Abul Mahasin Bahauddin mashuhuri kwa jina la Ibn Shidad, fakihi, kadhi na mwanahistoria wa Kiislamu. Alizaliwa mwaka 539 huko Mosul, moja ya miji ya Iraq na alihifadhi Qur'ani akiwa bado mtoto na baadaye akajifunza hadithi, tafsiri na kusoma Qur'ani na kupata umahiri mkubwa katika taaluma hizo. Ibn Shidad alifanya safari katika nchi mbalimbali za Kiislamu kwa ajili ya kutafuta elimu. Miongoni mwa vitabu vyake mashuhuri ni an Nawadir al Sultwaniya, Dalailul Ah-kam na al Aswaa kinachozungumzia maisha ya Nabii Musa A.S. na mapambano yake dhidi ya Firauni.
Miaka 436 iliyopita katika siku kama hii ya leo alizaliwa Mulla Muhsin Faidh Kashani, aliyekuwa faqihi, mpokezi wa hadithi, mwanafalsafa na arifu mkubwa wa Kiislamu nchini Iran. Faidh Kashani alipata elimu za fiqhi, hadithi, tafsiri na falsafa kwa wanazuoni wakubwa wa zama zake kama Muhammad Taqi Majlisi, Sheikh Bahai na Mulla Sadra. Msomi huyo mkubwa ameandika vitabu vingi, mashuhuri zaidi vikiwa ni tafsiri ya Qur'ani ya al Swafi, Mafatiihu Sharaai', al Wafi na al Mahajjatul Baidhaa.
Siku kama ya leo miaka 189 iliyopita, inayosadifiana na 21 Septemba 1832, aliaga dunia Sir Walter Scott, mwandishi wa riwaya, mshairi na mwanahistoria mahiri wa Uskochi. Alizaliwa 15 Agosti mwaka 1771 na baada ya kuhitimu masomo yake katika taaluma ya sheria, alifanya kazi ya uwakili kwa muda wa miaka 14. Hata hivyo, Sir Scott alikuwa na shauku na mapenzi makubwa na taaluma ya fasihi ya lugha.
Siku kama ya leo miaka 112 iliyopita, yaani 21 Septemba 1909, alizaliwa Dakta Osagyefo Kwame Nkrumah mwanasiasa na shujaa wa uhuru wa Ghana. Nkurumah alishiriki kikamilifu katika harakati za kupigania uhuru za wananchi wa Ghana dhidi ya mkoloni Muingereza. Baada ya kujipatia uhuru, kulijitokeza na kushuhudiwa njama kadhaa za kutaka kumuondoa madarakani na hata kumuua Nkrumah. Mwaka 1966 wakati Dakta Nkrumah akiwa safarini nchini China, Jenerali Joseph Ankrah alifanya mapinduzi na kuiondoa madarakani serikali Nkrumah. Mwanamapinduzi huyo aliaga dunia mwaka 1972 akiwa uhamishoni nchini Romania. Kwame Nkrumah alikuwa na nafasi muhimu katika kuasisiwa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote NAM pamoja Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika OAU.
Na siku kama ya leo miaka 27 iliyopita Bunge la Taifa la Ufaransa lilipasisha sheria iliyopiga marufuku vazi la staha la mwanamke wa Kiislamu, hijabu katika shule za nchi hiyo. Ufaransa ilipasisha sheria hiyo inayowazuia wanafunzi wa kike Waislamu kwenda mashuleni wakiwa na vazi la hijabu licha ya kudai kuwa ni kitovu cha demokrasia na uhuru. Baadaye sheria hiyo ilipanuliwa zaidi na kupiga marufuku vazi la hijabu katika vyuo vikuu na idara za umma. Wachambuzi wengi walikosoa vikali sheria hiyo wakisema inapingana na Katiba ya Ufaransa na Tangazo la Kimataifa la Haki za Binadamu zinazosisitiza kuwa kila mtu ana uhuru wa kukubali na kutekeleza itikadi zake za kidini maadamu hazina madhara kwa watu wengine.