May 30, 2016 01:35 UTC
  • Jumatatu, Mei 30, 2016

Leo ni Jumatatu tarehe 23 Shaaban mwaka 1437 Hijiria, inayosadifiana na tarehe 30 Mei 2016 Miladia

Siku kama ya leo miaka 1133 iliyopita, yaani tarehe 23 Shaaban mwaka 304 Hijria aliaga dunia Abu Muhammad Hassan bin Ali Ut'rush, mwenye lakabu ya "Naasir Kabir", alimu na mujahidina mkubwa miongoni mwa wajukuu wa Bwana Mtume Muhammad SAW. Alizaliwa mwaka 230 hijria mjini Madina; na baada ya watawala wa Bani Abbas kuwabaidishia mjini Samarra kaskazini mwa Baghdad watu kadhaa wa kizazi cha Bwana Mtume akiwemo Imam Hassan al-Askari (as) pamoja na baba yake Hassan Ut'rush, yeye mwenyewe pia alipelekwa katika mji huo wa Iraq. Hassan bin Ali alijifunza elimu za dini katika miji ya Baghdad na Kufa na kuwa alimu mtajika katika zama zake. Alishiriki pia katika harakati za kisiasa; na katika kipindi cha mapambano na hatimaye kutawala Maalawi katika mji wa Tabaristan kaskazini mwa Iran, yeye pia alielekea huko. Mjukuu huyo wa Bwana Mtume SAW alifanya jitihada kubwa sana katika tablighi na kuitangaza dini ya babu yake na kuwafanya maelfu ya watu wasilimu na kufuata dini tukufu ya Uislamu. Aliacha athari za makumi ya vitabu vikiwemo vya "Al-Basat", "Tafsirul-Ut'rush" na "Al-Imamatul-Kabir".

&&&&

Miaka 98 iliyopita, muwafaka na 30 Mei 1918, yalimalizika mapigano makubwa ya Maren yaliyotokana na Vita vya Kwanza vya Dunia kati ya jeshi la Ujerumani na vikosi vya waitifaki vilivyozijumuisha Marekani, Uingereza na Ufaransa. Vita hivyo vya siku 5 vilijiri katika eneo lililoko karibu na Mto Maren ulioko kaskazini mashariki mwa Ufaransa, na majeshi ya Ujerumani yalijipatia ushindi na kuwashikilia mateka wanajeshi elfu 55 wa majeshi ya waitifaki.

&&&&

Na siku kama ya leo miaka 238 iliyopita sawa na tarehe 30 Mei 1778, Francois- Marie Arouet maarufu kwa jina la Voltaire, mwanafalsafa na mwandishi wa Kifaransa alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 84. Katika maisha yake, Voltaire aliwahi kuwekwa mahabusu mara mbili na kubaidishwa kwa muda wa miaka mitatu nchini Uingereza. Kitendo hicho kilimkasirisha sana Voltaire na kumfanya kuwa dhidi ya utawala wa Ufaransa.

&&&&