May 30, 2016 23:05 UTC
  • Shujaa Mandela
    Shujaa Mandela

Leo ni Jumanne tarehe 24 Shaaban mwaka 1437 Hijiria, inayosadifiana na tarehe 31 Mei 2016 Miladia


Miaka 125 iliyopita katika siku kama ya leo, yaani tarehe 24 Shaaban mwaka 1312 hijria,  Mirza Muhammad Hassan Shirazi, mmoja wa wanazuoni na mar'ja' mashuhuri wa Kiislamu aliaga dunia. Alizaliwa Shiraz kusini mwa Iran na baada ya kuhitimu masomo yake ya msingi alielekea katika mji mtakatifu wa Najaf nchini Iraq kuendeleza masomo yake ya kidini ambapo alisoma kwa wanazuoni mashuhuri wa mji huo kama vile Sheikh Murtadha Ansari. Bidii yake kwenye masomo ilimuwezesha kukwea haraka daraja za elimu na kuwa mhadhiri na mwanazuoni wa ngazi za juu mjini hapo na katika ulimwengu mzima wa Kiislamu. Jina la Mirza Shirazi ni mashuhuri mno kutokana na fatua yake ya kuharamisha tumbaku katika kipindi cha utawala wa Mfalme Nassir Deen Shah wa ukoo wa Qajaar. Fatuwa yake hiyo ya kuharamisha tumbaku na matumizi ya sigara, bidhaa ambayo ilikuwa imehodhiwa na Uingereza, ilitoa pigo kubwa kwa ukoloni wa Uingereza nchini Iran. Fatuwa hiyo ilichukuliwa kuwa mapambano ya moja kwa moja dhidi ya utawala wa Shah na ukoloni wa Uingreza nchini Iran. Kwa hakika iliandaa uwanja wa mapambano ya baadaye ya wananchi wa Iran dhidi ya dhulma, ukandamizaji na ukoloni wa wageni nchini.


Siku kama ya leo, miaka 184 iliyopita, yaani tareh 31 Mei mwaka 1832 miladia aliuawa Évariste Galois, mtaalamu mwenye kipawa cha hesabati wa Ufaransa.  Évariste Galois alizaliwa katika mji wa Bourg-la-Reine karibu na mji mkuu wa nchi hiyo, Paris. Hadi kufikia umri wa miaka 12, Galois hakuwa na mwalimu mwengine zaidi ya mama yake. Kuanzia rika la uchipukizi alianza kusoma vitabu vya kiwango cha juu mno vya hesabati na hivyo kuinukia kielimu. Baada ya hapo alijiunga na chuo, ambapo alikuwa akishika nafasi ya kwanza darasani katika kila somo. Baadaye Évariste Galois alianza kutalii elimu ya hisabati. Akiwa na umri wa miaka 18 alikamilisha kazi ya uandishi wa kitabu cha ukweli wa hisabati na baada ya hapo akaandika vitabu vitatu vipya katika taaluma hiyo na kujipatia umashuhuri mkubwa. Galois aliuawa akiwa na umri wa miaka 21 hapo tarehe 29 mwezi Mei mwaka 1832 Miladia, baada ya kutiwa jela wakati wa harakati zake za kisiasa nchini Ufaransa. Weledi wanaamini kuwa, kama Galois hangeuawa mapema, basi angepiga hatua kubwa katika uga wa hisabati duniani.


Na siku kama ya leo miaka 106 iliyopita, yaani tarehe 31 Mei mwaka 1910 miladia, nchi ya Afrika Kusini iliundwa katika eneo la kusini mwa Afrika kwa kuunganishwa makoloni mawili ya Uingereza na kupewa uhuru. Muungano huo ulipata uhuru kamili mwaka 1931. Hata hivyo hatamu za madaraka ya nchi ziliingia mikononi mwa wazungu wachache. Lakini hatimaye baada ya mapambano makali ya waafrika kusini wazalendo wakiongozwa na shujaa Nelson Mandela, mnamo mwaka 1991 wazungu makaburu walilazimika kuhatimisha mfumo wa ubaguzi wa rangi wa Apartheid katika nchi hiyo…/