May 31, 2016 21:52 UTC
  • Jumatano, Juni 1, 2016

Leo ni Jumatano tarehe 25 Shaaban mwaka 1437 Hijiria, inayosadifiana na Juni 1 2016 Miladia

Miaka 1300 iliyopita katika siku kama ya leo, yaani tarehe 25 Shaaban mwaka 137 Hijria Qamaria, Abu Muslim Khorassani, kamanda Muirani, aliuawa kwa amri ya Mansour, mtawala wa wakati huo wa Ukhalifa wa Bani Abbas.
Abul Muslim Khorassani alikuwa kiongozi wa mwamko uliojulikana kama "Siyah Jamegan" katika eneo la Khorassan. Mwamko huo ulikuwa dhidi ya watawala wa kiimla. Katika kipindi kifupi, aliweza kupata wafuasi katika aghalabu ya miji na vijiji. Abu Muslim na wafuasi wake walifanikiwa kuwashinda watawala wa Bani Umayya. Kwa msingi huo, baada ya kuanguka utawala wa Bani Umaiyya ulikuja madarakani utawala wa Bani Abbas. Hapo Abu Muslim alikuwa na nguvu na ushawishi mkubwa kiasi cha Mansour, mtawala wa Bani Abbas kuingiwa na kiwewe na hivyo akapanga njama ya kumuua. Baada ya kuuawa Abu Muslim, baadhi ya wafuasi wake walianzisha mapigano ambayo yaliendelea kwa muda mrefu.

Siku kama ya leo miaka 30 iliyopita, wanafunzi kadhaa wa shule za msingi waliwaandikia barua wenzao duniani kote na kuwataka kupitisha muda wao wa siku nzima kwa ajili ya amani. Sehemu moja ya barua ya wanafunzi hao ilisomeka kama ifuatavyo: "Wazazi wanatupenda, kwa kuwa sisi ni watoto wao. Hata hivyo je, mnafahamu ni dunia ya aina ngani waliyotuandalia? Sisi kamwe tusingekuwa na fursa ya kukua, iwapo wazazi wetu wangefanya kosa japo dogo tu. Tunahitaji suhula kwa ajili ya kukua na malezi." Kwa ajili hiyo, siku ya kwanza ya mwezi Juni kila mwaka, ikapewa jina la "Siku ya Watoto Duniani". Kwa ajili hiyo marasimu maalumu hufanyika katika pembe mbalimbali duniani katika kuadhimisha siku hiyo.

Miaka 46 iliyopita, siku kama ya leo, alifariki dunia nchini Iraq Ayatullahi Sayyid Muhsin Hakim mtaalamu wa fiq'hi, msomi mkubwa na mmoja wa maraajii wakubwa wa Kiislamu. Alizaliwa mwaka 1264 Hijiria Shamsia. Ayatullah Hakim alipata kuhifadhi Qur'ani Tukufu akiwa na umri mdogo na baadaye alisoma elimu ya dini kwa walimu wakubwa wa zama zake. Ayatullah Hakim aliongoza mapambanao dhidi ya waliokuwa wakiupinga Uislamu na alitoa fatwa kupinga Ukomunisti. Aidha alitoa fatwa kuhusu Jihadi dhidi ya utawa wa Kizayuyni wa Israel. Kuna athari nyingi kutoka kwa Sayyid Hakim, miongoni mwazo ni pamoja na kitabu kiitwacho "Mustamsikul Urwatul Wuthqaa" kilicho katika juzuu 14, "Haqaiqul Usul" na " Nahjul Fuqaha."

Na siku kama ya leo miaka 64 iliyopita, aliaga dunia John Dewey, msomi na mwandishi mashuhuri wa Marekani. Dewey alizaliwa 20 Oktoba mwaka 1859 na alikuwa amebobea mno katika elimu ya malezi na aliweza kujifunza mengi alipokuwa katika chuo kikuu cha Colombia. John Dewey alifanikiwa kuandika vitabu vingi kuhusiana na malezi na makuzi ya mtoto. Miongoni mwa vitabu mashuhuri alivyoviandika katika kipindi cha uhai wake ni pamoja na "How we think", "The Public and its Problems" na "Freedom and Culture." John Dewey alifariki dunia mwaka 1952 akiwa na umri wa miaka 93.