Alkhamisi, Juni 2, 2016
Leo ni Alkhamisi tarehe 22 Shaaban mwaka 1437 Hijiria, inayosadifiana na Juni 2 2016 Miladia
Siku kama ya leo miaka 53 iliyopita, wananchi Waislamu wa Iran baada ya kupata habari kwamba Imam Khomeini (MA) alikuwa amekamatwa na utawala dhalimu wa Shah, walifanya maandamano makubwa kote nchini dhidi ya utawala huo. Siku kadhaa nyuma, Imam alikuwa ametoa hotuba kali katika Chuo cha Kidini cha Faidhiyya akifichua maovu yaliyokuwa yakifanywa na utawala wa Shah, jambo lililouchukiza sana utawala huo na kuamua kumtia nguvuni, Imam. Suala hilo liliwakasirisha sana wananchi wa Iran ambao waliamua kufanya maandamano ya kushinikiza kuachiliwa kwake mara moja. Ili kukabiliana na wimbi la malalamiko hayo, utawala wa Shah uiliamua kuwashambulia waandamanaji ambapo uliua na kuwajeruhi wengi kati yao. Harakati hiyo ya mapambano ambayo inafahamika humu nchini kama Mapambano ya Tarehe 15 Khordad, kwa hakika ulikuwa mwanzo wa mapambano ya mapinduzi ya Kiislamu ya wananchi shupavu wa Iran dhidi ya utawala wa kitaghuti wa Shah, mapambano ambayo yaliainisha mustakbali wa kisiasa na kijamii wa Iran. Mapambano hayo yaliendelea kwa uongozi shupavu wa Imam Khomeini hadi Mapinduzi ya Kiislamu yalipofikia ushindi hapo mwaka 1979.
Siku kama ya leo miaka 134 iliyopita alifariki dunia kamanda mwenye mielekeo ya utaifa wa vita vya umoja wa Italia Giuseppe Garibaldi. Alizaliwa mwaka 1807 na kujishughulisha na kazi mbalimbali katika kipindi cha ujana wake. Baadaye Garibaldi alijiunga na jeshi na hatimaye kuwa kamanda wa wapigania uhuru wa Italia. Alifanya juhudi kubwa kwa ajili ya kuitumikia nchi hiyo hali iliyopelekea kutambuliwa katika historia ya Italia kuwa shujaa wa taifa.
Na miaka 74 iliyopita katika siku kama ya leo sawa na terehe Pili Juni 1942, wakati wa Vita vya Pili vya Dunia, yalianza mashambulizi makubwa ya kulipiza kisasi ya Ujerumani dhidi ya vikosi vya Uingereza yaliyoongozwa na Mashal Erwin Rommel huko kaskazini mwa Afrika yaaliyojulikana kama Mbweha wa Jangwani. Kabla ya mashambulizi hayo, Waingereza waliivamia na kuikalia Libya iliyokuwa ikidhibitiwa na jeshi la Ujerumani ya kinazi. Katika mashambulizi hayo ya kulipiza kisasi yaliyochukua mwezi mmoja, askari wa Ujerumani mbali na kuidhibiti tena Libya, walifika hadi eneo la al-Alamin kaskazini mwa Misri karibu na bandari muhimu ya Alexandria. Kama mashambulizi hayo ya Ujerumani yangeendelea, vikosi vya nchi hiyo vingeweza kukomboa mfereji wa kistratejia wa Suez uliokuwa chini ya mahasimu wao.