May 27, 2022 02:14 UTC
  • Ijumaa, Mei 27, 2022

Leo ni Ijumaa mwezi 25 Mfunguo Mosi Shawwal 1443 Hijria sawa na Mei 27 Mei mwaka 2022 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 1295 iliyopita Imam Ja'far Sadiq mmoja wa wajukuu wa Mtume Mtukufu amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake na Ali zake, aliuawa shahidi kwa amri ya mtawala dhalimu wa Kiabbasi, Mansur al Dawaniqi. Imam Sadiq alizaliwa mwaka 83 Hijria katika mji mtakatifu wa Madina. Alishika hatamu za kuongoza Umma wa Kiislamu akiwa na umri wa miaka 31 baada ya kuuawa shahidi baba yake Imam Muhammad Baqir. Imam Sadiq ambaye kipindi cha uongozi wake kilisadifiana na zama za mapigano makali kati ya watawala wa Kiamawi na Kiabbasi, alitumia fursa hiyo kueneza elimu na maarifa sahihi ya Kiislamu. Alifanikiwa kulea na kutayarisha wasomi hodari katika taaluma mbalimbali kama tiba, kemia, hesabati, nujumu hadithi na kadhalika. Jabiri bin Hayyan ambaye anatambuliwa hii leo kuwa ndiye baba wa elimu ya kemia alikuwa mwanafunzi wa Imam Ja'far Saqid (as). Ushawishi wa Imam ulienea kwa kasi katika ulimwengu wa Kiislamu, jambo ambalo halikuwafurahisha watawala wa Kiabbasi. Hatimaye mtawala Mansur al Dawaniqi aliamuru Imam apewe sumu. Mtukufu huyo aliuawa shahidi kwa sumu hiyo katika siku kama ya leo na akazikwa katika makaburi ya Baqii mjini Madina.

Siku kama ya leo miaka 539 iliyopita alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 82, Luca della Robbia, msanii mkubwa wa uhunzi wa Italia. Akiwa kijana alijifundisha kazi ya ufuaji dhahabu, hata hivyo aliachana na kazi hiyobaadaye na kujihusisha na uhunzi wa masanamu. Katika kipindi hicho alipata kuunda masanamu na athari mbalimbali za kale. Athari kadhaa za Luca della Robbia zipo katika majengo tofauti ya maonyesho duniani.

Luca della Robbia

Siku kama ya leo miaka 185 iliyopita sawa na tarehe 27 Mei 1837, ulitiwa saini mkataba wa amani kati ya Ufaransa na Amir Abdulqadir wa Algeria kiongozi wa wapigania uhuru wa nchi hiyo. Tangu mwaka 1832 baada ya mashambulizi ya jeshi la Ufaransa nchini Algeria Amir Abdulqadir aliendesha mapambano dhidi ya wavamizi huko Algeria na kusimama kidete dhidi yao kwa miaka kadhaa na kujulikana kama kiongozi wa wanamapambano wa Algeria dhidi ya Ufaransa. Baada ya kufikiwa makubaliano hayo maeneo mengi ya Algeria yaliyokuwa chini ya Ufaransa yalipewa uhuru.

Amir Abdulqadir

Siku kama ya leo miaka 112 iliyopita, aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 67 Robert Koch, mgunduzi wa vijidudu maradhi aina ya bakteria na tabibu mashuhuri wa Kijerumani aliyegundua chanzo cha maradhi ya kifua kikuu au TB. Daktari Robert Koch alianza kutwalii na kufanya utafiti mkubwa juu ya sababu au vyanzo vya kutokea baadhi ya magonjwa kama vile kipindupindu, kimeta na kifua kifuu, baada ya kuhitimu masomo yake katika fani ya tiba. Mwaka 1882 Miladia, Robert Koch alifanikiwa kugundua vijidudu maradhi vinavyoitwa mycobacterium tuberculosis vinavyosababisha kifua kikuu. Ili kukamilisha uchunguzi wake tabibu huyo Mjerumani alisafiri katika nchi za Afrika Kusini, Misri na India na kutwalii magonjwa mengineyo maarufu katika maeneo hayo kama vile Malaria. Mwaka 1905 Robert Koch alitunukiwa Tunzo ya Nobel katika uwanja wa Tiba. 

Siku kama ya leo miaka 96 iliyopita, harakati ya mapambano ya Riffi nchini Morocco dhidi ya mkoloni Muhispania na Ufaransa, ilipata pigo. Kwa miaka kadhaa Muhammad Abdul-Karim al-Khitwabi, maarufu kwa jina la Amir Muhammad Riffi, kiongozi wa harakati hiyo, alifanya mapambano mengi na wavamizi wa Uhispania huku akifikia ushindi kadhaa. Ushindi wake dhidi ya majeshi vamizi ya Uhispania uliitia khofu Ufaransa. Mwanzoni mwa mwaka 1924 Miladia askari wa Ufaransa waliingia Morocco kwa ajili ya kuwasaidia wenzao wa Uhispania dhidi ya harakati hiyo ya Riffi. Katika kipindi hicho askari hao wa Ufaransa walifanya mauaji makubwa dhidi ya raia wa nchi hiyo. Aidha baada ya askari vamizi wa Ufaransa na Uhispania kumtia mbaroni Muhammad Abdul-Karim al-Khitwabi walitekeleza jinai kubwa dhidi ya maelfu ya wafuasi Waislamu wa harakati ya Riffi.

Amir Muhammad Riffi

Siku kama ya leo miaka 73 iliyopita muwafaka na Khordad 6 mwaka 1328 Hijiria Shamsia, alifariki dunia Allama Muhammad Qazwini, mwanafasihi, mtafiti na mwanahistoria wa zama hizi wa Iran. Tangu utotoni Allama Qazwini kwa msaada wa baba yake alijifunza masuala mengi kuhusu fasihi na elimu ya itikadi. Mwanazuoni huyo amecha vitabu vingi katika uwanja wa fasihi, falsafa na historia.

Allama Muhammad Qazwini

 

Tags