Jun 05, 2016 07:54 UTC
  • Jumapili, Juni 5, 2016

Leo ni Jumapili tarehe 29 Shaban mwaka 1437 Hijiria, inayosadifiana na tarehe 5 Juni 2016 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 34 iliyopita, alifariki dunia Bi. Nusrat Amin, mwanamke wa kwanza aliyefikia daraja la mujtahid katika ulimwengu wa Kiislamu. Bi. Nusrat alizaliwa mjini Isfahan, Iran mnamo mwaka 1308 Hijiria. Akiwa na umri wa miaka minne alianza kwenda katika maktaba na kujifundisha Qur'ani Tukufu na lugha ya Kifarsi. Ni wakati huo ndipo alipotokea kusomea dini ya Kiislamu na kufikia daraja ya juu katika uwanja huo. Alilipa umuhimu mkubwa suala la kusoma huku akitabahari katika elimu ya Fiq'hi, Usulu na lugha ya Kiarabu. Miongoni mwa maulama wakubwa waliomfundisha elimu ya fiq'hi ni Ayatullah Najaf Abad.

Siku kama ya leo miaka 1218 iliyopita alifariki dunia Fadhlu Bin Dukin maaruf kwa jina la Ibn Naim, mtaalamu wa hadithi, fiq'hi na mwanahistoria. Ibn Naim aliyezaliwa mwaka 130 Hijiria nchini Iraq, alikuwa mmoja wa wapokezi wa hadithi huku akipewa heshima na maulama wakubwa wa Kiislamu wa enzi hizo. kitabu cha 'as-Swalat' ni miongoni mwa vitabu vya msomi huyo mkubwa wa Kiislamu.

Siku kama ya leo miaka 1119 iliyopita alifariki dunia Ibn Mundhir, mtaalamu wa sheria za Kiislamu, mfasiri wa Qur'ani Tukufu na mtaalamu wa hadithi wa Kiislamu. Ibn Mundhir alijifunza elimu ya fiq'hi na hadithi kutoka kwa wasomi wakubwa wa zama zake huku akifanya safari pia kuelekea mjini Makkah, ambapo alisikiliza na kujifunza elimu ya hadithi hadi mwisho wa uhai wake. Aidha akiwa mjini Makkah alijishughulisha na uandishi wa vitabu tofauti. Katika kitabu cha 'Al-Ijmaa' alibainisha na kufafanua nadharia tofauti za wasomi katika uwanja wa sheria za Kiislamu.

Na siku kama ya leo miaka 49 iliyopita inayosadifiana na tarehe 5 Juni 1967 vilianza vita vya tatu kati ya utawala wa Kizayuni wa Israel unaoikalia kwa mabavu Quds Tukufu na mataifa ya Kiarabu. Katika siku hiyo, vikosi vya anga vya utawala wa Israel vilishambulia majeshi ya nchi tatu za Misri, Syria na Jordan kwa muda wa masaa mawili baada ya kufanya operesheni ya kushtukiza kwa kuvuka mipaka ya nchi hizo. Majeshi ya utawala wa Israel yalitekeleza operesheni hiyo kwa kuungwa mkono na serikali za Marekani na Uingereza.