Sibtain katika Qur'ani na Hadithi
Assalaam Alaykum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikikutangazieni kutoka mjini Tehran. Tunakukaribisheni katika kipindi kingine cha Sibtain katika Qur'ani na Hadithi ambacho tunatumai kitakunufaisheni vya kutosha. Kama mnavyojua, katika vipindi hivi tunajadili fadhila na sifa za Maimamu Wawili ambao ni wajukuu wapendwa na maua ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) na amabo si wengine bali ni Imam Hassan na Hussein (as).
Ndugu wasikilizaji, Mwenyezi Mungu aliwachagulia walimwengu Mitume na kuwateulia Mitume hao (as) mawasii wa kuwarithi. Kuhusu hilo kulikuwepo na udharura wa kuwaandaa mawasii hao katika ulimwengu wa kabla ya ulimwengu huu na kuwapa fadhila, ukamilifu, vipawa na sifa za kipekee ambazo zingewatenganisha na wanadamu wengine wa kawaida kwa upande mmoja na kwa upande wa pili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao ya mbinguni bila ya kukabiliwa na kikwazo chochote katika utekelezaji wa majukumu hayo. Katika uwanja huo Mwenyezi Mungu aliwapa vipawa vikubwa vya kielimu, takwa, umaasumu (kutotenda dhambi), nuru, mwongozo wa mbinguni, utukufu na heshima ya hali ya juu katika mwanzo wa maisha yao. Miongoni mwa watukufu waliopata hadhi hiyo kubwa ya mbinguni ni Mtume Mtukufu (saw). Ni wazi kuwa kwa sifa hizo aali, watukufu hao walipata fursa ya kuwa na sifa maalumu ambazo watu wengine wa kawaida hawakujaaliwa kuwa nazo.
Ndugu wasikilizaji, huenda baadhi ya watu wasioamini suala hili wakahitajia dalili na hoja maalumu ya kuthibitisha suala hilo kwa sababu huenda wakawachukulia Mitume na Maimamu (as) kuwa ni watu wa kawaida tu ambao hawana sifa, ukamilifu wala vipawa vyovyote maalumu vya mbinguni vinavyowatofautisha na wanadamu wengine. Bila shaka walio katika mustari wa mbele wa sifa na fadhila hizi aali za mbinguni ni Mtume Muhammad (saw) na Ahlu Bait wake watoharifu (saw). Ni vipi hilo? Hili ndilo jambo tunalotazamia kulijadili katika kipindi chetu hiki cha leo, karibuni.
***********
Maadh bin Jabal amenukuliwa katika vitabu vya Ilal Sharai' cha Sheikh Swadouq, Dalail al-Imama cha Tabarsi, Bihar al-Anwaar cha Sheikh al-Majlisi na Nasikh at-Tawarikh cha Muhammad Taqi akisema kwamba Mtume (saw) alisema: 'Hakika Mwenyezi Mungu aliniumba mimi, Ali, Fatwimah Hassan na Hussein kabla ya kuumba dunia kwa miaka elfu saba.' Maadh akamuuliza: Basi mlikuwa wapi ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu? Akamjibu kwa kusema: 'Tulikuwa mbele ya Arshi tukimsabihi Mwenyezi Mungu, kumtukuza na kumsifu.' Maadh akasema: Mlikuwa katika umbo gani? Akasema (saw): '(Tulikuwa) Pepo za nuru, hadi ulipowadia wakati wa Mwenyezi Mungu kutuumba, akawa ametuumba katika sura ya nguzo za nuru. Kisha akaturusha katika uti wa mgongo wa Adam, kisha akatuweka katika uti wa mgongo wa akina baba na tumbo za akina mama, na kamwe haikutugusa najisi ya shirki wala uchafu wa kufri (kukufuru). Baadhi ya watu walipata saada kupitia kwetu na wengine wakapotoka.'
Nam wapenzi wasikilizaji, hupata saada kupitia watukufu hao wale wanaowakubali, kuwapenda, kuwafuata na kuwaamini katika fadhila, sifa na ubora wao. Miongoni mwa sifa na utukufu wa kipekee wa watukufu hao ni kile Mtume (saw) alichombainishia Maadh kuhusu jinsi alivyokuwa yeye na Ahlu Bait wake (as). Ama kuhusu hali yake na watukufu wengine wa Ahlul Bait (as) miaka elfu mbili kabla ya kuumbwa wanadamu, alimbainishia suala hilo Ibn Masoud kama inavyofafanuliwa na Al-Karakchi katika kitabu cha Kanzul Fawaid, Sayyid Hashim al-Bahrani katika Hilyatul Abrar, Istarabadi katika kitabu cha Ta'weel Ayaat adh-Dhwahira na wengine wengi kwamba alisema: 'Ewe Ibn Masoud! Hakika Mwenyezi Mungu aliniumba mimi, Ali, Hussan na Hussein kutokana na nuru ya adhama yake kabla ya viumbe wengine kwa miaka elfu mbili, wakati ambao hakukuwepo na tasbihi wala utukuzaji. Alipoamua kuumba viumbe, alipasua nuru yangu na kuumba mbingu na ardhi kutokana nayo, na mimi Wallahi! Ni mtukufu na mbora kuliko mbingu na ardhi, na kisha akapasua nuru ya Ali na kuumba kutokana nayo Arshi na Kiti cha Enzi na Ali Wallahi! Ni mtukufu na mbora kuliko Arshi na Kiti cha Enzi, kisha akapasua nuru ya Hassan na kuumba Loho na Kalamu kutokana nayo na Wallahi! Hassan ni mtukufu na mbora kuliko Loho na Kalamu na hatimaye akapasua nuru ya Hussein na kuumba kwayo Pepo na Hurul Ain, naye Hussein Wallahi! Ni mtukufu na mbora kuliko viumbe viwili hivyo.
Mashariki na Magharibi zikawa zimepata giza na Malaika wakamlalamikia Mwenyezi Mungu Mtukufu wakimwambia: Ewe Mwenyezi Mungu! Tufariji na utuondolee giza hili kutokana na utukufu wa pepo hawa wema uliowaumba…. Mwenyezi Mungu Mtukufu akaumba Roho na kuiunganisha na nyingine. Akaumba nuru kutokana nayo kisha akaiunganisha nuru hiyo na ile Roho na akamuumba kutokana nayo Fatwimatu Az-Zahra….. na hapo ndipo akaitwa Zahra, na kisha Mashariki na Maghajribi zikawa zimewaka na kuangaza kutokana na nuru hiyo.'
***********
Hivi, wapenzi wasikilizaji, ndivyo alivyoumbwa Bwana wetu Mtume (saw) pamoja na Ahlu Bait wake watoharifu (as) hadi nuru yao ilipoangaza na kufika ardhini ambapo walilakiwa, kupendwa na kufuatwa na baadhi ya watu kama anavyonukuu Muhammad bin Abu al-Qassim at-Tabari katika kitabu chake cha Bisharat al-Mustafa Lishiat al-Murtadha akimnukuu Abu Huraira kwamba alisema: 'Nilimsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) akimwambia Ali: 'Je, nikubashirie jambo ewe Ali? Akajibu: Ndio, baba na mama yangu wawe fidia kwako ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Akasema: Mimi, wewe, Fatwimah, Hassan na Hussein tumeumbwa kutokana na dongo moja, na Mashia na wafuasi wetu (wanaotupenda) wameumbwa kutokana na udongo uliosalia (mabaki ya udongo huo).'
Mwanazuoni wa Kihanafi as-Sheikh Jamal ad-Deen Muhammad bin Ahmad al-Muswili, mashuhuri kwa jina la Ibn Hassanawiyia katika kitabu chake cha Durr Bahar al-Manaqib anamnukuu Ibn Yasir akisema: Mtume (saw) alisema: 'Usiku niliopaishwa Miiraji kwenda mbinguni, Mwenyezi Mungu aliniteremshia Wahyi kwa kusema: Ewe Muhammad! Utamwachia nani Umma wako? Nikasema: Allahumma! Hilo liko juu yako… Akasema: Umesema kweli. Mimi ni khalifa wako juu ya watu wote ewe Muhammad! Nikasema: Labaika, umetukuka ewe Mola! Akasema: Nimekuteua wewe uwe mjumbe wangu na wewe ni mlinda amana wa Wahyi wangu. Kisha nilimuumba kutokana na dongo lako mkweli mkuu na mbora wa mawasii, nikamjaalia Hassan na Hussein. Ewe Muhammad! Ali ni tawi lake (yaani la mti), Fatwimah majani yake na Hassan na Hussein ni matunda yake. Nilikuumbeni kutokana na udongo wa walio juu zaidi na kuwajaalia (kuwaumba) Mashia wenu kutokana na udongo wenu uliobakia. Ni kutokana na hilo ndipo nyoyo na miili yao ikawa inakuelekeeni nyinyi.'
Nam wapenzi wasikilizaji, suala hilo linasisitizwa na Swadouq katika katika kitabu cha Maani al-Akhbar, Hurr al-Amili katika al-Jawahir as-Sunniyat fi al-Ahadeeth al-Qudsiyya na wengineo ambapo wanasema kuwa Imam Swadiq (as) alisema: 'Mwenyezi Mungu aliumba roho kabla ya miili kwa miaka elfu mbili, na roho zilizokuwa tukufu na bora zaidi zilikuwa roho za Muhammad, Ali, Fatwimah, Hasanain (Hassan na Hussein) na Maimamu wengine tisa kutoka katika kizazi cha Hussein bin Ali (as). Kisha alisiwasilisha roho hizo mbele ya mbingu, ardhi na milima. Nuru ya maasumu hao kumi na wanne iliangaza kila mahali ulimwenguni. Hapo Mwenyezi Mungu Mtukufu akazihutubu mbingu, ardhi na milima kwa kusema: Hawa ni marafiki na mawalii wangu, nao ndio hujja zangu kwa viumbe wangu wote na Maimamu wa viumbe wangu. Sikuumba kiumbe kingine chochote ninachokipenda zaidi yao. Nimeumba Pepo yangu kwa ajili ya watu wanaowapenda (wafuasi wao) na Moto wangu wa Jahannam kwa ajili ya wapinzani na maadui zao.
Hivyo kila mtu anayedai kuwa na utukufu na nafasi ya hali ya juu kama yao, nitamuadhibu adhabu ambayo sijawahi kumuadhibu kiumbe mwingine yeyote na kumtumbukiza kwenye tabaka la chini zaidi la Moto mkali wa Jahannam pamoja na mushrikina. Na watakaofuata wilaya yao na kutodai utukufu na nafasi yao aali tutawaingiza wote kwenye bustani za Pepo yangu. Watapewa humo kila jambo watakaloniomba. Watakuwa pembeni (ya rehema) yangu na kuwakubalia shufaa yao kwa watenda dhambi wanawake kwa wanaume. Hivyo wilaya yao ni amana yangu kwa viumbe wangu.'
Na kufikia hapa wapenzi wasikilizaji ndio tunafikiwa mwisho wa kipindi hiki kwa leo. Basi hadi tutakapokutana tena juma lijalo kwa ajili ya kusikiliza kipindi kingine, panapo majaaliwa, tunakuageni nyote kwa kusema, kwajerini.