Pezeshkian: Iran haina nia ya kuingia katika mzozo na nchi za eneo
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i137296-pezeshkian_iran_haina_nia_ya_kuingia_katika_mzozo_na_nchi_za_eneo
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Masoud Pezeshkian, amesisitiza kwamba Iran haitaki vita au uhasama na nchi za eneo, bali inalenga tu vituo vinavyotumiwa kama chanzo cha mashambulizi dhidi ya ardhi yake.
(last modified 2026-03-11T22:54:06+00:00 )
Mar 11, 2026 22:54 UTC
  • Pezeshkian: Iran haina nia ya kuingia katika mzozo na nchi za eneo

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Masoud Pezeshkian, amesisitiza kwamba Iran haitaki vita au uhasama na nchi za eneo, bali inalenga tu vituo vinavyotumiwa kama chanzo cha mashambulizi dhidi ya ardhi yake.

Kwa mujibu wa taarifa ya Shirika Rasmi la Habari la Iran, IRNA, Rais Pezeshkian ameyasema hayo katika mazungumzo ya simu na Waziri Mkuu wa Pakistan, Shehbaz Sharif, ambapo wamejadili hali ya mambo katika eneo na mahusiano ya pande mbili.

Rais Pezeshkian amesema: “Kwa bahati mbaya, wavamizi wamekuwa wakitumia nchi jirani kufanya mashambulizi dhidi ya miundombinu, maeneo ya umma, hospitali na shule nchini Iran. Katika tukio moja pekee, wanafunzi 168 wasio na hatia walifariki na wengine kujeruhiwa kufuatia shambulio la kinyama kwenye shule ya Minab.”

Rais Pezeshkian amebainisha wazi mkakati wa ulinzi wa Iran kwa kusema: “Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haina dhamira ya kulenga au kupambana na majirani wake wa kikanda. Hatua zake zote za kijeshi zinafanyika ndani ya mipaka ya kujilinda kihalali.”

Aidha, ameonya kuwa: “Iwapo jumuiya ya kimataifa na mashirika ya kimataifa hayatatoa kipaumbele kwa wale walioanzisha vita hii na uvamizi huu wa kijeshi dhidi ya Iran, hali ya utulivu na mpangilio wa dunia utayumba na kuwa hatarishi.”

Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Pakistan, Shehbaz Sharif, amesisitiza msimamo wa msingi wa serikali yake kukemea vikali uvamizi unaoongozwa na Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran, na kuonesha mshikamano wa kina wa serikali na wananchi wa Pakistan na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Sharif amemalizia kwa kubainisha hamu ya kuendeleza juhudi za pamoja kuboresha mahusiano ya nchi hizo mbili jirani za Kiislamu, na kuimarisha umoja na ushirikiano miongoni mwa mataifa ya Kiislamu katika eneo la Asia Kusini na Mashariki ya Kati.