Jul 14, 2022 09:37 UTC
  • Sibtain katika Qur'ani na Hadithi

Assalaam Alaikum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran na karibuni kusikiliza sehemu ya 23 ya kipindi hiki cha Sibtain katika Qur'ani na Hadithi.

Imenukuliwa katika Tafsiri ya al-Qummi kwamba siku moja Amru bin al-Aas alimuona Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) akiingia msikitini na kumuita kwa matusi: "Ewe mwenye kukatikiwa"! Katika zama hizo za ujahilia kila mtu ambaye hakuwa na mtoto alikuwa akitusiwa kwa jina hilo la 'abtar' yaani aliyekatikiwa na kizazi. Kisha Amru akasema: Kwa hakika mimi ninamchukia sana Muhammad. Hapo Mwenyezi Mungu akateremsha Sura ya Kauthar akimwambia Mtume wake mtukufu (saw): Hakika tumekupa kheri nyingi. Basi swali kwa ajili ya Mola wako na uchinje. Hakika anayekuchukia ndiye mwenye kukatikiwa. Yaani anayemchukia, ambaye ni Amru bin al-Aas ndiye mwenye kukatikiwa, kwa maana kuwa hana dini wala kizazi."

Na kuhusiana na Sura hii al-Fakhr ar-Razi anakiri katika kitabu chake cha Tafsiri al-Kabir kwamba kizazi cha Mtume (saw) ndicho kizazi kikubwa zaidi kwa mtu kuwahi kuwa nacho katika historia ya mwanadamu, licha ya vita vikubwa alivyopigwa, kufukuzwa kutoka kwenye makazi yake, kufungwa, kuzingirwa na kuteswa. Mwenyezi Mungu alitaka kizazi chake (saw) kitokane na binti yake mtukufu, Bibi Fatwimat az-Zahraa (as), ambaye ni mke wake Imam Ali Amir al-Mu'mineen (as). Kizazi hicho kitukufu cha Mtume (saw) kilikuwa na kuenea duniani kupitia wajukuu wake wema na watukufu ambao ni Imam Hassan na Hussein (as).

Fakhr ar-Razi anasema kuhusu jambo hilo kuwa: "Kauli ya tatu kuhusu 'Kauthar' ambayo maana yake ni kheri nyingi, ni watoto wake (saw). Wanasema: Hii ni kwa sababu Sura hii ya Kauthar iliteremshwa kuwajibu watu waliomdhihaki na kumfanyia dharau kutokana na kutokuwa na watoto. Maana yake ni kuwa Mwenyezi Mungu aliahidi kumpa kizazi ambacho kingebakia duniani milele."

Kisha Fakhr ar-Razi anaendelea kusema: "Tazama, ni watu wangapi waliouawa katika Ahlu Bait lakini wakati huohuo tizama ulimwengu ulivyojaa kizazi chao. Katika upande wa Bani Umayyia hakuna yeyote aliyebakia duniani kumuenzi! Tazama jinsi kizazi cha Ahlul Bait kilivyokuwa na maulama na wanazuoni wakubwa, kama vile al-Baqir, as-Swadiq, al-Kadhim na ar-Ridhwa (as)."

Nam wapenzi wasikilizaji, inatosha kushuhudia hapa Aya ya Mubahala ikinasibisha neno 'watoto' wakikusudiwa Hassan na Hussein (as) kwa Mtume Mtukufu (saw). Wajukuu wawili hawa ni katika kizazi cha Mtume (saw) ambao kuzaliwa kwao kulimfanya Mtume, kuwa na kheri nyingi. Imepokelewa kwamba Mtume Mtukufu (saw) alisema: 'Kila Nabii ana kizazi chake kinachonasibishwa kwake, na wana wa Fatwimah ni kizazi changu ambacho tunanasibishwa kwake." Vilevile al-Khatib al-Baghdadi anasema katika kitabu chake cha Tarikh Baghdad kwamba Mtume (saw) alisema: "Hakika Mwenyezi Mungu alijalia kizazi cha kila nabii katika uti wake wa mgongo na akajaalia kizazi changu katika uti wa mgongo wa huyu hapa." Na hapo akawa anamuashiria Ali bin Abi Talib (as).

************

Ndugu wasikilizaji, Sheikh al-Majlisi anasema katika kitabu chake cha Bihar al-Anwaar kwamba Imam Ali alimuoa Bibi Fatwimah (as) katika mwaka wa pili Hijiria, na akamwingilia kimwili baada ya tukio (vita) la Badr ambapo alibarikiwa kumzalia wana wao Hassan, Hussein, Zainab al-Kubra na Umm Kulthum al-Kubra. Naye ad-Dulabi anaandika katika kitabu chake cha adh-Dhuriyyat at-Twahira kwa kusema: "Fatwimah bint ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) alimzalia Ali bin Abi Talib (as): Hassan, Hussein na Muhsin ambaye aliaga dunia akiwa angali mtoto mdogo, na kisha akamzalia Umm Kulthum na Zainab.

Na hiki ndicho kizazi kibarikiwa cha Mtume (saw) ambapo Mwenyezi Mungu Mtukufu alitaka kizazi chake kitakatifu na kisafi kitokane na binti yake al-Batul pamoja na Msema Ukweli Mkuu, Amir al-Mu'mineen Ali (as). Kwanza alijaaliwa kumzaa Hassan ambaye ni wema mtupu na Mwenyezi Mungu alimjaalia kupata mimba yake katika mwezi mtukufu wa Rabiul Awwal, mwaka wa tatu Hijra. Baada ya kupata mimba hiyo alimwendea baba yake mpendwa, Mtume Mtukufu wa Mwenyezi Mungu (saw) na kumpa habari ya mimba hiyo. Mtume aliagiza aletewe jegi la maji na baada ya kutamkia humo baadhi ya maneno alitema humo mate yake matakatifu na kumwambia binti yake: Yanywe maji haya. Baada ya kuyanywa joto alilokuwa nalo mwilini likawa limemwondokea…… Na Inasemekana kuwa hali hiyo ilimtokea alipokuwa amebeba mimba ya Imam Hussein (as).

Kitoto hicho kilipotimu umri wa miezi minne kikiwa tumbano mwa mama yake, Bibi Zahra alipata Baraka na heri nyingi katika nyumba yake na hilo likawa limemsahaulisha hofu na uchungu wa kubeba mimba. Baada ya mimba kuingia katika mwezi wake wa sita Bibi Fatwimah (as) hakuhitajia mwangaza wa taa katika hali ya usiku mkubwa, na alipokuwa faraghani kuswali, alikuwa akikisikia kitoto hicho tumboni kikisabihi na kumtukuza Mwenyezi Mungu.

Karama hizo zilikuwa tu kwa ajili ya Ahlul Bait wa Mtume (saw). Ziliendelea hadi ulipotimia mwezi wa Mwenyezi Mungu, yaani mwezi wa Ramadhani katika mwaka wa Badr au mwaka wa tatu wa Hijra ya Mtume (saw). Mwanga wa Mwenyezi Mungu uliweza kuangaza nyumba ya Utume na Uimamum nayo haikuwa nuru nyingine bali ilikuwa ni nuru ya kuzaliwa Imam Hassan al-Mujtaba, mjukuu na ua la Mtume (saw), na Bwana wa Vijana wa Peponi."

Al-Kaf'ami anasema katika kitabu chake cha al-Misbaah: "Al-Hassan (as) alizaliwa Jumanne katikati ya mwezi wa Ramadhani mwaka wa tatu Hijiria." Naye Shahrashub anaandika katika kitabu chake cha Manaqib Aali Abi Talib: 'al-Hassan (as) alizaliwa mjini Madina katika usiku wa katikati ya mwezi wa Ramadhani, mwaka wa Uhud katika mwaka wa tatu Hjiria….' Naye Tabarsi anaashiria suala hilo katika kitabu chake cha I'laam al-Wara bi I'laam al-Hudaa, na kuongeza: 'Na alikuja naye mama yake Fatwimah, mbora wa wanawake wa dunia mbele ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) katika siku ya saba ya kuzaliwa kwake akiwa amembeba kwenye shuka la hariri ambalo Malaika Jibril alimletea Mtume (saw), naye Mtume akampa jina la Hassan……. Na Mtume (saw) aliaga dunia hali ya kuwa Imam Hassan (as) ana umri wa miaka saba na miezi saba.'

************

Ama kuhusu kuzaliwa Imam Hussein (as), wapenzi wasikilizaji, mwanahistoria Muhammad bin Talha as-Shafi' anatwambia katika kitabu chake cha Mataalib as-Saul fi Manaqib Aal ar-Rasul kama ifuatavyo: 'Hussein alizaliwa tarehe 5 Shaaban katika mji wa Madina mwaka wa nne Hijiria, na mama yake Fatwimatul-Batul (as) alipata ujauzito wake nyusiku hamsini baada ya kumzaa kaka yake Hassan. Haya ndiyo mapokezi sahihi na kwa msingi huo hakukuwepo na muda mwingine kati yake na ndugu yake huyo isipokuwa muda huo na wakati wa kubebwa mimba yake…. Alipozaliwa Mtume alipashwa habari naye akawa amemuadhinia katika sikio lake la kulia na kumkimia katika sikio lake la kushoto, na ni sahihi kuwa alizaliwa baada ya kubebwa tumboni kwa miezi sita, na kuhusiana na hilo Mwenyezi Mungu aliteremsha Aya ya 15 ya Surat al-Ahqaf inayosema: Na kuchukua mimba kwake hata kumwachisha ziwa ni miezi thalathini.'

Kuhusiana na suala hili, At-Tabari as-Shafi' anasema katika kitabu chake cha Dhakhairul Uqba fi Manaqib Dhawil Quraba: 'Hakuna mtoto yeyote aliyezaliwa akiwa na miezi sita na akaishi isipokuwa al-Hussein na Isah bin Maryam (as).' Naye Ibn Swabbagh al-Maliki anasema katika kitabu cha al-Fusuul al-Muhima: 'Mtume (saw) alitabiri kuzaliwa kwake na akamuita Hussein.' Al-Juwayni as-Shafi' anaandika katika kitabu cha Faraid as-Simtain akimnukuu Ibn Abbas: 'Hussein bin Ali alipozaliwa Alkhamisi jioni usiku wa kuamkia Ijumaa, Mwenyezi Mungu Mtukufu alimwambia mkuu wa wanaosimamia Moto: Izime mioto hiyo kwa wanaochomeka kwa heshima ya mtoto aliyezaliwa kwa ajili ya Muhammad duniani.' Allahumma Swalli Ala Muhammadin wa Aali Muhammad.

Na hadi hapa wapenzi wasikilizaji ndio tunafikia mwisho wa kipindi hiki kwa leo. Basi hadi tutakapojaaliwa kukutana tena siku nyingine, tunakutakieni kila la heri, kwaherini.