Sibtain katika Qur'ani na Hadithi
Assalam Alaykum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran, na karibuni kusikiliza sehemu ya 25 katika mfululizo wa vipindi hivi vya Sibtain ambavyo vinawazungumzia Maimamu wawili al-Hassan na al-Hussein (as) katika Qur'ani na Hadithi tukufu za Kiislamu.
Wapenzi wasikilizaji, bado tunaendelea kuzunumzia fadhila na utukufu wa Maimamu wawili hawa (as) ambao dunia nzima iling'ara na kuangazwa kwa uzawa na uwepo wao. Kama tulivyoona katika vipindi vilivyopita watukufu wawili hawa walizaliwa na kupata mapokezi maalumu kutoka kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake (saw). Mtume aliwapokea na kuwapa malezi maalumu yaliyojaa upendo na huruma ya baba ambapo daima alikuwa akiwashumu na kuwapakata kwenye kifua chake kitakatifu, bali kwenye moyo wake uliojaa upendo na mapenzi. Mara tu walipozaliwa walifunikwa kwa kitambaa na shuka maalumu nyeupe iliyoteremshwa kutoka peponi na kuwapa majina ya Hassana na Hussein kwa amri ya Mwenyezi Mungu Mtukufu.
Baada ya hapo Mtukufu Mtume (saw) aliwaadhinia kwenye masikio yao ya kulia na kuwakimia kwenye masikio yao ya kushoto kama ilivyo mila na desturi ya Uislamu na kisha kuwatolea sadaka pamoja na kuwaombea dua ya kiwakinga na maoavu. Hivi ndivyo anavyonukuu Ibn Asakir ad-Dimishki as-Shafi' katika kitabu cha Tarikh Madinat ad-Dimishq. Anasema Mtume Mtukufu (saw) alipaza sauti kwa kusema: 'Nileteeni wanangu wawili hawa ili nipate kuwaombea dua ya kuwakinga kama alivyofanya Ibrahim juu ya Ismail na Is'haqa. 'Walipofika mbele yake aliwakumbatia kifuani na kusema: Ninakukingeni kwa maneno kamilifu ya Mwenyezi Mungu na maovu ya kila shetani na kiumbe, pamoja na jicho baya.'
Riwaya nyingine inasema kwamba Abdallah bin Omar anasema: 'Hassan na Hussein walikuwa na hirizi mbili ambazo zilikuwa na manyoya ya bawa la Jibril…' Haya yameandikwa katika vitabu vya Sahih Bukhari, Tirmidhi, Ibn Maaja Abi Dawoud, Hulyatul Auliyaa cha Hafidh Abi Naim na Majmau az-Zawaid wa Manbau al-Fawaid cha Haithami as-Shafi'.
**********
Wapenzi wasikilizaji, hapa kuna mfano wa kuvutia wa huruma ya baba aliyoionyesha Mtume Mtukufu kwa Imam Hassan na Hussein (as), kupitia hadithi ambayo imenukuliwa na Ayadh al-Maghribi al-Yahswabi katika kitabu chake cha as-Shifaa Bitaarifi Huquqil Mustafa ambapo anasema: Mtume aliwapa ulimi wake Hassan na Hussein, ambao walikuwa wanalia sana kutokana na kiu kali, waunyonye na baada ya kuunyonya wakawa wamenyamaza na kutulia…. Naye Haithami as-Shafi anazungumzia suala hilo hilo kupitia hadithi aliyoandika katika kitabu chake cha Majmaul az-Zawaid akimnukuu Abu Huraira ambaye anasema: Walipofika njiani, Mtume wa Mwenyezi Mungu aliwasikia Hassan na Hussein wakilia huku wakiwa na mama yao. Aliharakisha matembezi hadi alipowafikia…' Abu Huraira anaendelea kusema: 'Nilimsikia Mtume akisema: Nini kimewapata wanangu? Fatwimah akajibu: Ni kiu…Mtume akaenda kutafuta maji kwenye kiriba lakini hakupata hata tone moja la maji… Akamwambia binti yake Fatwimah: Nipe mmoja wao. Akampa mmoja wao kutoka kwenye vazi lake la stara, na Mtume akawa amemchukua na kumuweka kifuani ambapo alimpa ulimi wake naye mtoto huyo akawa anaunyonya hadi alipotulia, Sikusikia tena akilia. Wa pili naye alikuwa anaendelea kulia. Mtume akasema: Nipe mwingine…. Fatwimah alipompa alifanya kama alivyomfanyia wa kwanza na wawili hao wakawa wamenyamaza kimya wala sikusikia tena sauti yao.'
Hadithi hii pia imenukuliwa na Ahmad Zaini Dahlani, Mufti wa mji mtakatifu wa Makka katika kitabu chake cha as-Siratu an-Nabawiyya, Ibn Hajar al-Askalani katika Tahdhib at-Tahdhib na al-Muttaqi al-Hindi katika kitabu cha Kanzul Ummal.
Kwa hivyo msishangae wapenzi wasikilizaji msomi wa Kihanafi al-Hafidh al-Hakim al-Hasakani anaposema katika kitabu chake cha Shawahid at-Tanzil Liqawaid at-Tafdhil katika ufafanuzi wa Aya 74 ya Surat Furqan inayosema: Na wale wanaosema: Mola wetu! Tupe katika wake zetu na wenetu yaburudishayo macho, na utujaalie tuwe waongozi kwa wachamungu, kwamba Mtume (saw) alimuuliza Malaika Jibril, nani wake zetu kwenye Aya hii? Naye Jibril akamjibu: Ni Khadija. Akauliza tena, na wanetu? Akajibu: Ni Fatwimah. Kisha akauliza tena Mtume (saw): Na yaburudishayo macho? Jibril akajibu: Ni Hassan na Hussein. Akauliza Mtume: Na Utujaalie tuwe waongozi kwa wachamungu? Akasema: Ni Ali bin Abi Talib.
********
Ama kuhusiana na majina ya Maimamu wawili hawa watukufu, wapenzi wasikilizaji, hayo ni miongoni mwa rehema na neema kubwa ya Mwenyezi Mungu juu ya Watu wa Nyumba ya Mtume Mtukufu (saw). Nam, licha ya kuwa vitabu vya historia ya Kiislamu vinasema kuwa ni Mtume ndiye aliyewapa Maimamu hao majina ya Hassana na Hussein pamoja na kunia (lakabu) zao za Abu Muhammad na Aba Abdillah, kwa utaratibu huo, lakini ni wazi kuwa majina hayo matukufu yaliteremshwa kwa mara ya kwanza kutoka mbinguni, na yalikuwa hayajawahi kutumika tena duniani kabla ya kuzaliwa watukufu wawili hao. Hilo limethibiti katika vitabu mashuhuri vya historia kama vile Usudul Ghaaba cha Ibn Athir, ambaye amemnukuu Ibn al-A'rabi akisema kuwa al-Mufadhal amesema: 'Hakika Mwenyezi Mungu aliyapendelea majina ya Hassan na Hussein (as) hadi Mtume akawapa wanae wawili majina hayo al-Hassan na al-Hussein. Ibn al-A'rabi akasema: Na wale walioko Yemen je? Akajibu: Wao ni Hasnun na Hassin.' Pia amemnukuu Amran bin Suleiman akisema: 'Hassan na Hussein ni majina ya peponi ambayo hayakuwepo katika zama za ujahilia.'
Tunamuona Ibn Asakir as-Shafi' akiandika katika kitabu cha Tarikh ad-Dimishq kupitia mapokezi marefu kuwa: 'Jabir ametupasha habari kwamba Ibn Abbas alisema: Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema: Usiku ule nilipopaishwa mbinguni, niliona kwenye mlango wa peponi pameandikwa: La Ilaha Ila Allah, Muhammad Rasullullah, Ali ni kipenzi wa Mwenyezi Mungu, Hassan na Hussein ni wabora (wateule) wake na Fatwimah ni mteule wake. Laana ya Mwenyezi Mungu iwe juu ya wale wanaowachukia.'
Kwa hivyo wasikilizaji wapenzi majina mawawili haya matukufu ni majina ya mbinguni na peponi. Lakini je, nini chanzo cha majina hayo au yametokana na nini? Swali hili halijibiwi na mwingine ila Imam Zeinul Abedeen, Ali bin al-Hussein (as) ambaye anasema: 'Siku moja Mtume Mtukufu (saw) alikuwa ameketi pamoja na Ali, Fatwimah, Hassan na Hussein (as). Akasema Mtume: Ninaapa kwa jina la yule aliyenituma kwa haki niwe mtoa-bishara njema kuwa, hakuna duniani viumbe walio bora na watukufu zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kutuliko sisi hapa. Mwenyezi Mungu Mtukufu alinipa jina kutokana na moja ya majina yake. Yeye ni Mahmoud nami ni Muhammad. Kisha alikupa wewe Ali jina lako kutokana na moja ya majina yake. Yeye ni al-Aliyul A'ala (yaani aliye juu zaidi) na wewe ni Ali (yaani aliye juu). Alikupa wewe Hassan jina lako kutokana na moja ya majina yake kwa kuwa Yeye ni Muhsin na wewe ni Hassan, na akakupa wewe Hussein jina lako kutokana na moja ya majina yake ambapo Yeye ni Mwenye Hisani na wewe ni Hussein. Kisha alikupa jina lako ewe Fatwimah, kutoka katika moja ya majina yake ambapo Yeye ni Fatir (Muumbaji) na wewe ni Fatwimah. Kisha Mtume (saw) akasema: Allahumma, kuwa shahidi yangu kwamba mimi nitakuwa salama kwa yule anayekuwa salama kwao, kumpiga vita atakayewapiga vita, kumpenda atakayewapenda, kumchukia atakayewachukia, adui kwa atakayekuwa na uadui nao na waongoze wanaoongozwa nao, kwa sababu wao ni katika mimi (wanatokana na mimi) nami ni katika wao.'
Nam wapenzi wasikilizaji, la muhimu ni kwamba dua hiyo ya Mtume (saw) ambayo bila shaka ilijibiwa, ilimuomba Mwenyezi Mungu awaongoze wale wote wanaowachukulia watukufu hao kuwa viongozi wao, adui wa wanaokuwa na uadui nao, awapende wanaowapenda na kuwachukia wanaowachukia. Na sisi kwa upande wetu tunamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu atupe taufuiki ya kuwapenda na si miongoni mwa wanaowachukia, wanaokuwa salama kwao na si wale wanaowapiga vita, wanaowaamini na kuwatii na wanaowafuata na kuwanusuru. Amin ya Rabbal Aalameen.
Wassalaam Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.