Sibtain katika Qur'ani na Hadithi
Assalaam Alaykum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran.
Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema zake, ambaye ametuwezesha kukutana tena katika kipindi kingine cha Sibtain katika Qur'ani na Hadithi. Salamu zake zimwendee Mtume wetu Mtukufu ambaye ni mbora wa mitume na viumbe wote duniani, Muhammad (saw). Kama mnavyojua wapenzi wasikilizaji kipindi hiki cha Sibtain katika Qur'ani na Hadithi ni katika mfululizo wa vipindi vinavyozungumzia fadhila za wajukuu wawili wa Mtume Mtukufu (saw) ambao si wengine bali ni Imam Hassan na Hussein (as) kwa mujibu wa kitabu kitakatifu cha Qura'ni na Hadithi za Kiislamu. Hivyo tunakuombeni muwe nasi hadi mwisho wa kipindi ili tupate kunufaika kwa pamoja na yale tuliyokuandalieni kwa juma hili, karibuni.
Kama mnavyojua wapenzi wasikilizaji suna za Mtume (saw) zinajumuisha maneno vitendo na ishara zake na zote hizo zilibainisha na kuweka wazi mapenzi makubwa aliyokuwanayo kwa wajukuu wake wawili hao al-Hassan na al-Hussein (as). Si hayo tu bali kuna mambo muhimu yaliyotokana na suna hizo yanayothibitisha na kusisitiza wazi kwamba wajukuu wawili hao walikuwa na nafasi muhimu na maalumu mbele ya Mtume (saw) na Mwenyezi Mungu, Subhanahu wa Taala. Mtume mwenyewe alibainisha katika sehemu na matukio mengi tofauti utukufu na fadhila nyingi walizokuwanazo wajukuu wake hao mbele ya Mwenyezi Mtukufu, pamoja na isma na wilaya yao kwa Waislamu. Sifa na fadhila zote hizo zinathibitisha wazi kwamba watukufu hao walikuwa na haki ya kufuatwa, kuheshimiwa, kutiiwa na kuwaongoza Waislamu kuliko watu wengine wote, baada ya Mtume (saw) na baba yao mpendwa Imam Ali (as).
Wapenzi wasikilizaji zifuatazo ni baadhi ya Hadithi za Mtume alizotuachia kuhusiana na fadhila na utukufu wa Maimamu wawili hao ambao ni wajukuu wake wapendwa (as), ambazo tutazisikiliza hivi punde.
***********
Hafidh bin Asakir ad-Dimashki anamnukuu katika kitabu chake cha Tarikh ad-Dimashki Said bin Rashid ambaye anamnukuu Ya'li kwamba alisema: 'Hassan na Hussein walimkimbilia Mtume naye akawabeba mmoja katika mkono wake wa kulia na mwingine katika mkono wake wa kushoto huku akisema: Wawili hawa ni mau yangu mawili duniani, anayenipenda basi na awapende pia.'
Hakuna shaka yoyote wapenzi wasikilizaji kwamba Mtume (saw) anapendwa na Mwenyezi Mungu bali ndiye kiumbe anayependwa zaidi na Mwenyezi Mungu kuliko viumbe wake wengine wote. Kwa msingi huo ni wazi kuwa imani inawalazimisha Waumini kumpenda yeye na Aali zake kuliko hata nafsi zao. Hadithi tukufu tuliyotangulia kuisoma inawataka Waislamu wote kuwapenda Hassan na Hussein (as) na hivyo kuwepo mfungamano wa moja kwa moja kati ya kuwapenda wawili hao na kumpenda Mtume Mtukufu (saw). Kwa maelezo hayo ni wazi kuwa kuwapenda wawili hao ni suala muhimu mno katika imani ya dini ya Kiislamu, na je, itawezekanaje kwa Mwislamu kutowapenda watukufu hao hali ya kuwa walikuwa maua mawili yaliyomvutia sana Mtume? Walikuwa wakirukaruka kwenye mgongo wa Mtume akiwa anaswali naye Mtume akiwachukua na kuwaweka miguuni kwake na kusema: 'Wawili hawa ni maua yangu duniani." Hadithi hii pia imepokelewa na kunukuliwa na Muttaqi Hindi katika kitabu chake cha Kanzul Ummal, adh-Dhahbi Shafi katika Tadhkirat al-Hafidh, az-Zarandi al-Hanafi katika Nadhm Durar as-Simtain na vitabu vingie vingi.
Ama Sheikh Swadouq amemnukuu sahaba mwema Jabir bin Abdallah al–Ansari katika kitabu chake cha Aamali kwamba alisema: 'Nilimsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) akimwambia Ali bin Abi Talib siku tatu kabla ya kuaga kwake: 'Salamu za Mwenyezi Mungu ziwe juu yako ewe Baba wa Maua Mawili! Ninakuusia uyalinde maua yangu haya duniani.'
Nam, aliwakumbatia, kuwashumu na kuwausia Waislamu wawapende na kuwalinda hadi alipokata roho akiwa kwenye hali hiyo hiyo na wajukuu wake hao wapendwa.
*********
Kama tulivyotangulia kusema katika vipindi vilivyopita Maimamu wawili hawa wa Nyumba ya Mtume Mtukufu (saw) wametajwa na utukufu wao kusifiwa sana katika vitabu vingi vya kuaminika vya Waislamu. Moja ya Riwaya hizo ni ile mbayo imenukuliwa na Ibn Asakir ambapo anasema kupitia Ibn Sakhita kwamba Mtume (saw) alimwambia binti yake Fatwimah (as): 'Ewe Fatwimah! Mimi, wewe na wawili hawa (yaani Hassan na Hussein) na huyu ambaye amelala (akiwa anamuashiria Imam Ali as) tutakuwa sehemu moja Siku ya Kiama.'
Baada ya kurasa kadhaa, mwanahistoria huyo mashuhuri wa Kishafi' anamnukuu Zaid bin Aslam, kupitia baba yake Aslam kupitia Omar bin Khattab kwamba Mtume (saw) alisema: "Hakika Fatwimah, Ali, Hassan na Hussein watakuwa peponi kwenye kuba jeupe lililo na Arshi ya Mwenyezi Mungu kwenye paa lake." Ni utukufu na fadhila kubwa iliyoje hii ambayo Mwenyezi Mungu amewapa na kuwatunuku mawalii wake!!
Mwanazuoni mwingine wa Kihanafi al-Khawarazmi anasema katika kitabu chake cha Maqtal al-Hussein (as) kwamba Mtume Mtukufu (saw) alisema: "Kwenye pepo kuna daraja ambalo linaitwa 'al-Wasila'. Kila mnapotaka kuniombea jambo kutoka kwa Mwenyezi Mungu wakati mnapoomba dua, basi niombeeni na 'Wasila.' Badhi ya masahaba wakamuuliza: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Je, unaishi na nani kwenye pepo hiyo? Mtume (saw) akawajibu: Ali, Fatwimah, Hassan na Hussein."
Khawarazmi ananukuu Hadithi nyingine kutoka kwa Abu Said al-Khidri inayohusiana na usiku aliopaishwa mbinguni Mtume Mtukufu (saw) ambapo huko alikutana na Malaika wa Mwenyezi Mungu waliompongeza na kumwambia: "Pongezi kwako ewe Muhammad! Umepewa jambo ambalo hakupewa yeyote kabla yako na wala hatapewa atakayekuja baada yako. Umepewa Ali bin Abi Talib kuwa ndugu yako, Fatwimah ambaye ni mke wake kuwa binti yako, Hassan na Hussein kuwa watoto wako na wafuasi wao kuwa Mashia wako…. Ewe Muhammad! Wewe ndiye mbora wa Mitume, Ali mbora wa Mawasii, Fatwimah mbora wa wanawake wa ulimwengu, Hassan na Hussein ni wabora wa walioingia peponi kati ya watoto wa Mitume na Mashia wao ni wabora kati ya wale waliokingwa kutokana na misukosuko ya Siku ya Kiama."
Naye Khatib al-Baghdadi anatunukulia Hadithi nyingine katika kitabu chake cha Tarikh Baghdadi kupitia Ibn Abbas ambaye alisikia na kunukuu hadithi nyingi kutoka kwa Mtume (saw) kwamba alisema: "Katika usiku ule niliopaishwa mbinguni, niliona pameandikwa kwenye mlango wa pepo maneno yafuatayo: Hakuna mungu anayeabudiwa kwa haki isipokuwa Allah, Muhammad ni Mtume wake, Ali ni kipenzi chake, Hassan na Hussein ni wateule wake na Fatwimah ni mbora wake, laana ya Mwenyezi Mungu iwateremkie wale wote wanaowachukia."
Ndugu wasikilizaji, vitabu vingi vya historia bila kujali mielekeo ya kimadhehebu na kifikra ya waandishi wake, vinatuambia kwamba Mtume Mtukufu (saw) alikuwa akibainisha na kufafanua wazi sifa, fadhila na utukufu wa Ahlu Bait wake watoharifu (as) kwa ajili ya kuwatambulisha kwa Waislamu na kuwakinaisha waweze kuwakubali na kuwafuata katika masuala yao ya kisheria na kidini. Aliweka wazi fadhila utukufu na sifa hizo ili wapate kujua kwamba walipaswa kuongozwa humu duniani na watu wema na watukufu ambao wangewaongoza kwenye njia nyoofu kuelekea kwenye maisha yaliyojaa saada na mafanikio mbele ya Muumba wao, Mwenyezi Mungu Mtukufu. Ni wazi kuwa dini na akili iliyo salama inahukumu kuwa mwanadamu anapasa kuwafuata viongozi walioteuliwa na Mwenyezi Mungu na ambao hawafanyi makosa wala dhambi kama Imam Hassan na Hussein (as) ili kwa njia hiyo aweze kuishi humu duniani maisha yanayomridhisha Muumba wake na hivyo kumfanya aweze kufikia maisha mema na ya milele huko Akhera kama alivyoahidiwa na Mwenyezi Mungu mwenyewe, Subhanahu wa Taala.
Na hadi hapa wapenzi wasikilizaji, ndio tunafikia mwisho wa kipindi chetu hiki cha Sibtain katika Qur'ani na Hadithi kwa juma hili, kipindi ambacho kimekujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Basi hadi tutakapopata fursa nyingine ya kuwa pamoja nanyi tena katika kipindi kingine panapo majaliwa, tunakuageni nyote kwa kusema, Wassalam Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.