Aug 04, 2022 06:55 UTC
  • Sibtain katika Qur'ani na Hadithi

Assalaam Aalykum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Hii ni sehemu ya 44 katika mfululizo wa vipindi hivi vya Sibtain katika Qur'ani na Hadithi ambavyo tunatumai vinatunufaisha sote kwa pamoja. Hivyo tunakukaribisheni kwa moyo mkunjufu muwe pamoja nasi hadi mwisho wa kipindi ili tupate kunufaika na yale tuliyokuanfalieni kwa juma hili, karibuni.

Kati ya juhudi kubwa zilizofanywa na Mtume Mtukufu (saw) katika kueneza dini ya Uislamu ni kuhakikisha kabla ya kuaga kwake kuchungu kwamba alikuwa ameweka wazi misingi na sheria madhubuti za kudhamini uwepo wa dini hii tukufu. Aliweka nguzo imara za itikadi na sheria na wakati huo huo kutangaza wazi kila lililohitajika kwa ajili ya kueneza mafundisho aali ya dini. Ili kuhakikisha kuwa alikuwa ametimiza ujumbe aliopewa kuufikisha kwa waja wa Mwenyezi Mungu duniani, aliwausia Waislamu kila jambo lililohitajika kwa ajili ya kuulinda ujumbe huo unaowadhaminia walimwengu saada na wokovu wa milele. Miongoni mwa mambo yaliyotangazwa wazi na Mtume katika kufikisha na kutimiza ujumbe huo ni kutangaza viongozi na Maimamu ambao wangeongoza umma wa Kiislamu baada ya kuondoka yeye duniani na kurejea kwa Mola wake, maimamu ambao wote walitokana na nyumba yake toharifu na ambao aliwateua kwa amri ya Mwenyezi Mungu.

Kutokana na umuhimu wa suala hili, Mtume (saw) aliendelea kusisitiza juu ya umuhimu wake na kuwasihi Waislamu washikamane nalo kwa nguvu na uwezo wao wate, hadi katika dakika za mwisho za uhai wake mtukufu humu duniani. Mwanazuoni mashuhuri wa Kihanafi al-Khawarazmi anasema katika kitabu cha Maqtal al-Hussein (as) kwamba Mtume alipozidiwa na maradhi na nyumba yake tukufu kutumbukia kwenye huzuni kubwa, alitaka aitiwe wajukuu wake wawili al-Hassan na al-Hussein na walipofika mbele yake alianza kuwabusu kwa upendo mkubwa hadi akawa amezimia. Ali alipoona hivyo alifanya haraka kwenda kuwatoa wajukuu hao wa Mtume kwenye uso wake lakini Mtume (saw) akafumbua macho ghafla na kusema: "Waache wanufaike nami, nami ninufaike nao kwa sababu watafikwa na mambo makubwa baada yangu." Kisha alisema: "Enyi watu! Nimeacha kati yenu kitabu cha Mwenyezi Mungu, suna na Ahlu Bayt wangu. Hivyo anayepoteza Kitabu cha Mwenyezi Mungu ni sawa na aliyepoteza suna yangu na anayeipoteza suna yangu ni kama aliyepoteza Ahlu Bayt wangu. Vitu hivi havitatengana hadi vitakaponifikia kwenye Hodhi."

********

Hivi ndivyo alivyouaga Mtume umma wake… Kusisitiza, kukumbusha, kuonya na kubashiri. Alisisitiza sana suala hili kiasi kwamba hakukubakia tena nafasi ya mtu mwenye shaka kutilia shaka maneno ayaliyotamka kuhusiana na Kitabu cha Mwenyezi Munbu na Ahlu Bayt wake watukufu (as). Hili ni suala ambalo pia Ibn Abbas amelisisitiza kwenye Riwaya ambayo imenukuliwa na al-Juwainy as-Shafi' katika kitabu cha Faraid as-Simtain na kunukuliwa pia na al-Qanduzi al-Hanafi katika kitabu cha Yanabiul Mawadda.

Hadithi kama hiyo pia imenukuliwa na Sheikh Swadouq katika kitabu cha Ikmal ad-Deen wa Itmam an-Ni'mah ambapo anasema kwamba Mtume Mtukufu (saw) alimjibu Na'thal Myahudi alipomuuliza watu ambao wangemrithi katika uongozi kwa kusema: "Hakika wasii wangu ni Ali bin Abi Talib, na baada yake ni wanawe wawili Hassan na Hussein ambao nao watafuatwa na Maimamu tisa watakaotokana na kizazi cha Hussein." Hapo Na'thal alimwomba Mtume ataje majina yao naye akawa ameyataja moja baada ya jingine.

Kuna Riwaya nyingine inayohusiana na suala hilo na ambayo al-Kanji as-Shafi' ameinukuu katika kitabu chake cha Kifayat at-Talib kutoka kwa Jabir bin Abdallah al-Ansari kupitia Wathila bin al-As'qa' kwamba Mtume (saw) alipoombwa na Jandal bin Khair Myahudi kutaja majina ya Maimamu watakaochukua hatamu za uongozi wa umma wa Kiislamu baada yake alisema: 'Wa kwanza wao ni Bwana wa Mawasii ambaye ni baba wa Maimamu Ali, kisha wanawe Hassan na Hussein…." Aliendelea kuwataja hadi alipofika kwenye jina la mwisho la Maimamu hao ambaye si mwigine bali ni Imam wa Zama al-Mahdi (af). Miongoni mwa Maimau hao watoharifu na wongofu ni Imam Hassan na Hussein ambao walioungoza umma huu kwenye njia ya heri, fadhila, amani, kufuzu, wokovu na salama.

Ni kutokana na umuhimu wa suala hili wapenzi wasikilizaji, ndipo Mtume Mtukufu akawa analizungumzia na kulisisitiza sana katika maneno na hutuba zake mbele ya Waislamu. Suala hilo lilienea na kuwa jambo la kawaida miongoni mwa Waislamu kiasi kwamba baadhi ya Riwaya zinasema kuwa siku moja Hussein (as) alimuuliza babu yake Mtume Mtukufu (saw) kuhusiana na maana ya Aya ya Arham inayosema: Na jamaa wa nasaba wanastahikiana wenyewe kwa wenyewe zaidi katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu (Anfaal:75). Mtume akamjibu kwa kusema: "Wallahi! Mwenyezi Mungu hakukusudia wasiokuwa nyinyi na nyinyi ndio mnaostahiki zaidi katika jamaa wa nasaba. Hivyo iwapo nitakufa mimi basi baba yako Ali ndiye atakayestahiki zaidi kuchukua nafasi yangu ya uongozi, na akifa baba yako ni ndugu yako Hassan ndiye atakayestahiki kuchukua uongozi, na akiaga Hassan basi wewe ndiwe utakayestahiki kuchukua uongozi huo….."

Kisha alitaja majina ya Maimamu wengine tisa baada ya Imam Hussein hadi aliposema: "Maimamu hao wote tiza watatoka katika kizazi chako. Mwenyezi Mungu amewapa elimu na fahamu yangu na udongo wao unatokana na udongo wangu. Ole wao wanaoniudhi kuhusiana nao! Mwenyezi Mungu asijaalie shufaa yangu kwao."

Na tunaendelea kubakia na Mtume Mtukufu (saw) wapenzi wasikilizaji anapousia na kuwatahadharisha Waislamu kuhusiana na Ahlu Bayt wake (as). Kila alipopata fursa alikuwa akiwanasihi Waislamu, kutii, kuheshimu na kufuata mafundisho ya Ahlul Bayt wake watukufu na kutoachwa nyuma na safina yao, la sivyo wangebebwa na tufani ya upotevu na fitina na hivyo kupotea njia ya wokovu. Miongoni mwa Ahlu Bayt wa Mtume kulikuwa na watu waliochelea na kushughulishwa sana na suala la dini. Daima walikuwa ni wenye kumwogopa Mwenyezi Mungu, kuutetea Uislamu na kuogopa matatizo na mashaka ya Siku ya Kiama. Hivyo walikuwa wakimuuliza Mtume (saw) awabainishie watu ambao wangechukua urithi na uongozi wa umma wa Kiislamu baada ya kuga kwake dunia ili kupitia kwao waweze kufuata njia sahihi ya Uislamu na kutopotea kutokana na vishawishi vya humu duniani na miito ya maimamu wa upotovu.

Hivyo mara tu baada ya kuteremka Aya ya Ulil Amr inayosema: Enyi mlio amini! Mt'iini Mwenyezi Mungu, na mt'iini Mtume na wenye madaraka katika nyinyi (Nisaa:59), na Mtume (saw) kuwasomea Aya hiyo masahaba zake hadharani, sahaba mwema na mwenye ikhlasi Jabir bin Abdullah al-Ansari aliuliza: Eeh Mtume wa Mwenyezi Mungu! Tumekwishamjua Mwenyezi Mungu na Mtume wake, lakini ni akina nani hawa wenye madaraka ambao Mwenyezi Mungu ameambatanisha utiifu kwao na utii kwako? Mtume (saw) akajibu kwa kusema: "Wao ni Makhalifa wangu,  na Maimamu wa Waislamu baada yangu ewe Jabir!..... Wa kwanza wao ni Ali bin Abi Talib, kisha Hassan na Hussein, kisha Ali bin Hussein, kisha Muhammad bin Ali ambaye ni mashuhuri katika Torati kwa jina la al-Baqir na utaonana naye eeh Jabir! Utakapokutana naye, utampa salamu zangu. Kisha Swadiq Ja'ffar bin Muhammad, kisha Musa bin Ja'ffar, kisha Ali bin Musa, kisha Muhammad bin Ali, kisha Ali bin Muhammad, kisha Hassan bin Ali, kisha aliye na jina na kunia kama yangu na ambaye ni Hujja wa Mwenyezi Mungu kwenye ardhi yake na bakisho lake kwenye waja wake, mwana wa al-Hassan bin Ali…"

Siku moja Mtume (saw) aliswali na masahaba zake na baada ya kumaliza swala aliwaambia: ''Ninahisi kana kwamba nitaitwa hivi karibuni na kulazimika kujibu wito huo. Nimekuachieni vizito viwili: Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Ahlu Bayt wangu, viwili ambavyo iwapo mtashikamana navyo vilivyo basi hamtapotea baada yangu kamwe. Anayeshikamana na Ahlu Bayt wangu baada yangu atakuwa miongoni mwa waliofuzu na anayetengana nao ni miongoni mwa waliohiliki."

Baada ya maneno hayo ya Mtume (saw) Hudhaifa bin al-Yaman alimuuliza: "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Unatuachia nani kama khalifa baada yako?" Mtume alimjibu kwa swali kwa kumuuliza: "Je, Musa bin Imran alimuacha nani kuwa khalifa katika kaumu yake?"

Hudhaifa akajibu: Yusha' (Joshua) bin Nun." Kisha Mtume (saw) akasema: "Hakika Wasii na khalifa baada yangu ni Ali bin Abi Talib, kiongozi wa wema na muuaji wa makafiri. Amenusurika anayemnusuru na kudhalilika anayemdhalilisha."

Hudhaifa akamuuliza tena: "Eeh Mtume wa Mwenyezi Mungu! Je, Maimamu baada yako watakuwa wangapi?"

Mtume Mtukufu (saw) akamjibu kwa kusema: 'Idadi yao itakuwa sawa na idadi ya viongozi wa Bani Israel. Tisa watatokana na kizazi cha Hussein na ambao Mwenyezi Mungu atawapa elimu na fahamu kama yangu na ambao watakuwa hazina ya elimu ya Mwenyezi Mungu na madini ya wahyi wake…. Haika Mwenyezi Mungu Mtukufu ameuweka uimamu katika kizazi cha Hussein na hilo linatokana na kauli yake Mwenyezi Mungu katika Aya ya 28 ya Surat al-Zukhruf inayosema: Na akalifanya hili liwe neno lenye kubaki katika vizazi vyake… Kisha Mtume (saw) aliwahesabu mawasii wake ambao wangeuongoza umma wa Kiislamu kwa amri yake Mwenyezi Mungu ili   waangamie wenye kuangamia kwa dalili zilizo wazi, na waishi na kufuata njia sahihi wenye kuishi kwa dalili zilizo wazi.

Na kufikia hapa wapenzi wasikilizaji hatuna lililozidi wala kupungua katika kipindi cha leo, na hadi tutakapokutana tena juma lijalo panapo majaaliwa, tunakuageni nyote kwa kusema, Wassalaam Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.