Jun 09, 2016 00:25 UTC
  • Alkhamisi, Juni 9, 2016

Leo ni Alkhamisi tarehe 3 Ramadhan mwaka 1437 Hijria, sawa na tarehe 9 Juni mwaka 2016 Miladia.

Miaka 131 iliyopita muwafaka na siku kama ya leo, jeshi la Ujerumani lilivamia ardhi ya Togo huko magharibi mwa Afrika. Wakati huo maeneo ya pwani ya Togo yalikuwa sehemu bora kwa watu wa Ulaya kwa ajili ya biashara ya utumwa. Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana Togo imekuwa maarufu kwa jina la "Pwani ya Utumwa." Wakoloni wa Ujerumani waliendelea kuikalia kwa mabavu ardhi ya Togo hadi wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia. Baada ya hapo Togo ilikoloniwa na Wafaransa na Waingereza. Nchi hiyo ilipata uhuru mwaka 1960.

 XXXXXXXXXXXXXXX

Miaka 46 iliyopita katika siku kama ya leo, aliuawa shahidi msomi mwanamapambano wa Iran, Ayatullah Muhammadreza Saeedi. Ayatullah Saeedi aliuawa baada ya kuteswa kwa kipindi kirefu na askari vibaraka wa Shah katika jela ya utawala huo wa kidikteta. Msomi huyo alijipatia elimu katika chuo cha kidini cha Qum kutoka kwa wanazuoni kama vile Ayatullahil Udhma Boroujerdi na Imam Khomeini MA. Baada ya wananchi Waislamu wa Iran kusimama kidete katika mwamko wa Khordad 15 mwaka 1342 Hijiria Shamsia, wasomi hao wanamapambano walishadidisha harakati zao dhidi ya utawala wa Shah. Ayatullah Saeedi alitumia misikiti na majukwaa mbali mbali na haswa yenye hadhira ya vijana, kuwahamasisha wasimame dhidi ya tawala za kikoloni na haswa njama za utawala wa Kizayuni dhidi ya Palestina. Licha ya kuteswa na kundamizwa, lakini msomi huyo wa Kiislamu alisimama kidete bila kutetereka, jambo ambalo lilipelekea akamatwe na utawala wa Shah. Miongoni mwa vitabu mwa mwanachuoni huyo ni "Umoja wa Waislamu", "Ukombozi wa Wanawake", na "Kazi na Uislamu".

XXXXXXXXXXXXXXX

Na miaka 54 iliyopita sawa na leo, moto mkubwa ulitokea katika Chuo Kikuu cha Algiers mji mkuu wa Algeria. Moto huo ulichoma zaidi ya nakala laki tano za vitabu vyenye thamani kubwa zilizokuwa kwenye maktaba ya chuo hicho. Asilimia kubwa ya vitabu vilivyoungua vilikuwa miongoni mwa marejeo muhimu na nadra. Chuo Kikuu cha Algiers na maktaba yake vilichomwa moto na jeshi la siri la Ufaransa nchini Algeria. Jeshi hilo la siri liliundwa na askari wa Ufaransa waliokuwa wakipinga suala la kupewa uhuru Algeria. Moto huo ulikuwa miongoni mwa makumi ya mioto kadhaa iliyotokea katika siku hiyo nchini Algeria na mingi ilisaabishwa na jeshi la siri la Ufaransa.