Jumatatu, Septemba 19, 2022
Leo ni Jumatatu tarehe 22 Mfunguo Tano Safar 1444 Hijria sawa na tarehe 19 Septemba 2022 Milaadia.
Katika siku kama ya leo miaka 218 iliyopita alizaliwa mwanazuoni wa Kiislamu, Muhammad Baqir Zainul Abidin Khansari katika mji wa Isfahan nchini Iran. Alikuwa hodari katika elimu za fiqhi na hadithi na alipewa ijaza ya kunukuu Hadithi na wanazuoni wakubwa katika taaluma hiyo. Baada ya muda msomi huyo mkubwa ambaye alikuwa gwiji wa wasifu na shajara za maulamaa na wataalamu wa fiqhi ya Kiislamu, alishika hatamu za kuongoza chuo kikuu cha kidini cha Isfahan. Mirza Muhammad Baqir Khansari ameandika vitabu vingi na miongoni mwa vitabu vyake ni Raudhaatul Jannat, Ahsanul Atiyyah, Qurratul Ain na Hashiyatu Sharhil Lum'ah.

Siku kama ya leo miaka 115 iliyopita, mafuta ya petroli ya kutumia makaa ya mawe yalizalishwa kwa mara ya kwanza katika historia ya juhudi za mwanadamu za kupata vyanzo au mada za kuzalisha nishati. Mada hiyo mpya ya kuzalisha joto na nishati ilivumbuliwa na James Young, mwanakemia wa Scotland. Young alikuwa mmiliki wa mgodi wa makaa ya mawe na alifanikiwa kutengeneza mafuta ya petroli kwa kutumia makaa hayo kupitia njia inayojulikana kitaalamu kama (distillation).

Katika siku kama ya leo miaka 64 iliyopita, serikali ya kwanza huru iliundwa na viongozi wa mapinduzi nchini Algeria. Harakati za wananchi wa Algeria dhidi ya mkoloni Mfaransa zilianza mwanzoni wa Novemba 1954 sambamba na kushika kasi harakati za kupigani uhuru za wananchi hao. Nalo Jeshi la Ukombozi wa Algeria likaundwa kwa shabaha ya kuratibu mapambano. Tarehe 19 Septemba mwaka 1958 serikali ya muda ya Algeria ikatangaza uwepo wake. Hatimaye kushindwa jeshi la Ufaransa kusambaratisha harakati ya wananchi wa Algeria, kulipelekea Algeria ijitangazie uhuru mwaka 1962.
Miaka 41 iliyopita katika siku kama ya leo, mji wa Susangerd moja kati ya miji ya magharibi mwa Iran ulikombolewa na wapiganaji wa Iran na hivyo kuondoka katika uvamizi wa vikosi vya utawala wa Kibaathi wa Iraq. Ushindi huo mkubwa ilikuwa matokeo ya ushirikiano na uratibu wa karibu baina ya vikosi vya jeshi na makundi ya kujitolea ya wananchi.

Siku kama ya leo miaka 31 iliyopita Kuwait na Marekani zilisaini makubaliano ya kijeshi. Makubaliano hayo yalisainiwa karibu miezi sita baada ya Iraq kuhitimisha kuikalia kwa mabavu Kuwait. Viongozi wa Kuwait walidai kwamba, lengo la makubaliano hayo, ni kuzuia kutokea tena uvamizi mwingine wa Iraq dhidi ya nchi hiyo. Kwa mujibu wa makubaliano hayo ya kijeshi, Marekani iliruhusiwa kutumia bandari za Kuwait na kutuma wanajeshi na zana zake za kijeshi katika ardhi ya nchi hiyo na nchi mbili hizo kufanya mazoezi ya pamoja ya kijeshi. Mwaka 1991, Kuwait ikatiliana saini makubaliano kama hayo na Uingereza na Ufaransa. Miaka iliyofuatia, Bahrain, Qatar, Oman na Umoja wa Falme za Kiarabu zilisaini makubaliano ya kijeshi na Marekani, Uingereza na Ufaransa. Hata hivyo kinyume na matarajio ya viongozi wa nchi hizo za Ghuba ya Uajemi, makubaliano hayo badala ya kuwaletea amani, yalipelekea kutokea ushindani wa kumiliki silaha na kushadidi ukosefu wa amani katika Mashariki ya Kati.

Na miaka 28 iliyopita katika siku kama ya leo, wanajeshi elfu 20 wa Marekani walifanya mashambulizi ya anga na baharini na kuikalia kwa mabavu nchi ndogo ya Haiti inayopatikana katika bahari ya Caribean huko kusini mwa Marekani. Washington ilidai kuwa imeishambulia Haiti ili imrejeshe madarakani Rais Jean Bertrand Aristide wa nchi hiyo. Mwezi Septemba mwaka 1991 Jenerali Raoul Cedras alimpindua Aristide ambaye ndio kwanza alikuwa uongozini kwa muda wa miezi minane. Baada ya mapinduzi hayo Rais Jean Bertrand Aristide alikimbilia Marekani.