Jumapili tarehe 16 Oktoba 2022
Leo ni Jumapili tarehe 19 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1444 Hijria sawa na Oktoba 16 mwaka 2022.
Siku kama ya leo miaka 229 iliyopita, yaani tarehe 16 Oktoba mwaka 1793, aliuawa kwa kukatwa kichwa kwa shoka, malikia wa Ufaransa Marie Antoinette kwa amri ya Baraza la Katiba la nchi hiyo na pia amri ya Maximilien Robespierre. Louis wa 16 aliyekuwa mume wa Antoinette miezi 10 kabla ya hapo alikuwa tayari amepatwa na hatma hiyo hiyo iliyomkuta mke wake. Marie Antoinette alikuwa binti wa Maria Theresa Walburga, mtawala wa Austria na Ufaransa. Antoinette aliolewa na Louis, mrithi wa kiti cha ufalme wa Ufaransa, mnamo mwaka 1770 akiwa na umri wa miaka 14. Hatua ya Louis ya kumuoa mwanamke huyo ilikuwa na nia ya kuzikurubisha pamoja nchi za Austria na Ufaransa ambazo wakati huo zilikuwa zikishindana barani Ulaya. Hata hivyo Wafaransa wengi hawakuridhia ndoa hiyo kiasi cha kuwafanya kuendelea kumwita ‘Muaustria’ hata kipindi alipokuwa tayari ni malikia wa Ufaransa.
Katika siku kama ya leo miaka 168 iliyopita alizaliwa Oscar Wilde mwandishi mashuhuri Dublin huko Ireland. Oscar Wilde alipata elimu ya msingi katika mji wa Skyline kaskazini mwa Ireland na akajiunga na chuo kikuu cha Trinity na baadaye Oxford. Oscar Wilde alipata umaarufu baada ya kuandika mfululizo wa vitabu vya kisa cha Mwanamfalme Mwenye Furaha (The Happy Prince).
Siku kama ya leo miaka 77 iliyopita liliasisiwa Shirika la Chakula Duniani (FAO). Hati ya kuasisiwa shirika hilo ilipasishwa Oktoba 16 mwaka 1945 katika mji wa Québec nchini Canada. Lengo ya kuasisiwa shirika la FAO ni kuzisaidia nchi wanachama kukusanya taarifa, ripoti na takwimu zinazohusiana na chakula, kilimo, utunzaji wa misitu na uvuvi na kufanya tathmini kuhusu uzalishaji wa chakula, ugavi wake na juhudi za kuboresha uzalishaji, masoko ya chakula, kulinda maliasili, kupanga sera zinazohusiana na kilimo na chakula na kadhalika. Siku hii pia inatambuliwa kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Chakula.
Miaka 76 iliyopita katika siku kama ya leo, mwafaka na tarehe 16 Oktoba 1946, kwa mujibu wa hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Nuremberg walinyongwa viongozi 10 wa Ujerumani ya utawala wa Kinazi baada ya kupatikana na hatia za kutenda jinai za kivita. Herman Goering aliyekuwa Kamanda Mkuu wa kikosi cha Jeshi la Anga la Ujerumani na msaidizi wa dikteta Adolphe Hitler ambaye alikuwa amehukumiwa adhabu ya kifo, pia aliamua kujinyonga yakiwa yamebakia masaa machache kabla ya kutekelezwa hukumu hiyo ya kifo. Hali kadhalika mahakama hiyo iliwahukumu adhabu ya kifungo cha muda mrefu viongozi wengine 9 wa Ujerumani ya Wanazi na wengine watatu hawakupatikana na hatia. Mahakama ya Nuremberg iliyoundwa na wawakilishi wa Marekani, Urusi ya zamani, Uingereza na Ufaransa kwa shabaha ya kuwahukumu maafisa 22 wa Manazi wa Ujerumani kwa tuhuma za kufanya jinai za kivita ilikamilisha shughuli zake tarehe 30 Septemba mwaka 1946.
Na siku kama ya leo tarehe 24 Mehr miaka 44 iliyopita, kulitokea maafa makubwa kwenye Msikiti Mkuu wa Kerman, huko magharibi mwa Iran baada ya polisi na askari usalama wa utawala wa mfalme Muhammad Reza Pahlavi kuwashambulia kwa risasi wananchi waliokusanyika kwenye eneo hilo la msikitini kwa shabaha ya kuwaenzi na kuwakumbuka mashahidi waliouawa tarehe 17 Shahrivar mjini Tehran. Shambulio hilo la askari usalama wa Shah liliamsha hasira na wimbi jipya la harakati za wananchi za kupinga utawala kibaraka wa Mfalme Muhammad Reza Pahlavi.