Akhlaqi Katika Uislamu (3)
Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yako mpendwa msikilizaji popote pale ulipo wakati huu. Nakukaribisha kusikiliza sehemu hii ya tatu ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu nikiwa na matumaini kuwa, mimi pamoja na wewe tutanufaika na yale tutakayoyasikia katika kipindi hiki. Endelea kuwa nami basi hadi tamati ya mazungumzo yetu ya leo ambayo yataangazia baadhi ya misingi ya kifikra ya akhlaqi katika Uislamu.
Kama ujuavyo mpendwa msikilizaji, katika vipindi vilivyotangulia tulipoashiria udharura wa mtu kufungamana na thamani za kiakhlaqi tulieleza kwamba, hatua kuu na muhimu zaidi katika suala hilo ni kuzingatia msingi wa mtu "kuitambua nafsi yake". Hapana shaka kuwa, kama tutaitambua johari hiyo yenye thamani adhimu tuliyotunukiwa na Mola, na tukaielewa hadhi ya juu tuliyojaaliwa kuwa nayo katika mfumo wa ulimwengu wa maumbile, tutaichunga kwa nguvu na uwezo wetu wote mipaka ya thamani za kiakhlaqi. Hii ni pamoja na kwamba, mbali na Mwenyezi Mungu Mtukufu kumuumba mwanadamu katika umbo bora kabisa, amempulizia pia roho yake, kisha akamfanya khalifa na mfwatizi wake katika ardhi na akayafanya maumbile yake kuwa yenye kiu ya kumjua Yeye Mola wake. Ili mwanadamu asije akapotoka katika utambuzi wa akhlaqi nzuri na mbaya, amempa ilhamu pia ya kubaini mema na mabaya. Lakini mbali na yote hayo, ili kuhakikisha mwanadamu anabaki kwenye mkondo wa njia ya kumfikisha kwenye ukamilifu wa kiutu, Mola Muumba alimtayarishia pia suhula zote za kimaada na kimaanawi atakazohitajia. Kwa upande wa mahitaji ya kimaada, yawe ya angani au ardhini, akamtiishia vyote vilivyomo humo, kama anavyoeleza katika aya ya 13 ya Suratul-Jaathiya ya kwamba: Na amefanya vikutumikieni vilivyomo mbinguni na vilivyomo katika ardhi, vyote vimetoka kwake.

Ijapokuwa katika karne zilizopita, mwanadamu alinufaika na kufaidika sana na maliasili na hazina za kustaajabisha za ulimwengu wa maumbile kwa ajili ya maendeleo yake ya kisayansi na kujenga ustaarabu, lakini katika zama zetu hizi, mbali na kuitiisha ardhi ameweza pia kufika kwenye vina vikubwa vya angani na baharini na kupata mafanikio muhimu na ya mageuzi makubwa. Na mbali na suhula na nyenzo za kimaada, katika upande wa kimaanawi, Mwenyezi Mungu amemtunukia mwanadamu neema zisizo na kifani na zenye umuhimu wa kipekee kwa hatima na majaaliwa yake.
Moja ya neema hizo za kipekee ni kupelekewa Mitume na kuteremshiwa vitabu vya mbinguni. Ni sawa kwamba mwanadamu ameumbwa akiwa amejaaliwa kuwa na uwezo mkubwa na ukwasi mwingi wa sifa za maadili mema, lakini ni pale anapokulia kwenye njia sahihi ya malezi, ndipo huweza kuvistawisha na kuvitumia vipawa hivyo vya kimaumbile ili kumkurubisha kwenye ukamilifu wa kiutu. Lengo la kubaathiwa na kutumwa Mitume na kuteremshwa vitabu vya mbinguni, ambavyo ndani yake imebainishwa miongozo mikuu ya kufuata mwanadamu katika hali zake zote za shida na raha na kwa ajili ya mahitaji yake ya kimaumbile yanayojenga maisha yake, ni kumlea na kumjenga itakiwavyo kiumbe huyo. Anapolelewa kwa kufuata mfumo wa malezi wa Mitume wa Mwenyezi Mungu, mwanadamu hupambika kimaadili na kuweza kufikia ghaya na lengo kuu la kuumbwa kwake. Qur'ani tukufu imelieleza hilo katika aya nyingi, ikiwemo ya 25 ya Suratul-Hadiid isemayo: Kwa hakika tuliwatuma Mitume wetu kwa dalili waziwazi, na tukateremsha Kitabu pamoja nao na Mizani, ili watu wasimamie uadilifu, na tumeteremsha chuma chenye nguvu nyingi na manufaa kwa watu, na ili Mwenyezi Mungu amjue anaye mnusuru Yeye na Mitume wake kwa ghaibu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu Mwenye kushinda.

Lakini ili kuhakikisha pia kwamba bango la mchoro wenye kupendeza wa uumbwaji wa mwanadamu haliharibiwi, mbali na wajumbe wake waletaji wahyi, Mwenyezi Mungu amemwekea pia kiumbe huyo ndani ya nafsi yake kurunzi ing'arayo ya kumwongoza, aliyoipa jina la "akili" ili kwa kuzitumia tunu na neema mbili kuu za "akili na wahyi" ailinde na kuichunga kwa uelewa mipaka mitukufu ya thamani za kiutu na kiakhlaqi na cheo kilichotukuka alichopewa na Mola wake na kujiepusha na kufuata matamanio ya nafsi na wasiwasi atiwao na shetani unaomuelekeza kwenye upotofu na maangamizi. Lakini mbali na sifa zote hizo maalum na za kipekee tulizoashiria, ambazo Mola Muumba amemjaalia mwanadamu, ili kumfanya mwanadamu asighafilike na kusahau hadhi na thamani aliyopewa, Mwenyezi Mungu Mtukufu amemtunukia pia kiumbe wake huyo nishani nyingine ya heshima, aliposema katika aya ya 70 ya Suratu-Israa ya kwamba: Na hakika tumewatukuza wanaadamu, na tumewapa vya kupanda nchi kavu na baharini, na tumewaruzuku vitu vizuri vizuri, na tumewafadhilisha kwa fadhila kubwa kuliko wengi miongoni mwa tulio waumba.
Hebu na tujiulize mpendwa msikilizaji, kuna cheo na hadhi gani yenye thamani kubwa zaidi ya hiyo, tunayoweza kuitasawari kuwa atunukiwe mwanadamu? Ni ipi miongoni mwa hadhi na vyeo vya kidunia, vya kijamii na kisiasa, na ambavyo si vya kudumu, bali ni vya kuja na kuondoka tu, kinaweza kulinganishwa na hadhi na heshima aliyopewa mwanadamu na Mola wake? Katika kuonyesha kwamba ni Yeye Mola tu ndiye mwenye kumuenzi kwa maana halisi kiumbe wake huyo, katika sehemu ya mwisho ya aya tuliyosoma hivi punde Allah SWT ametilia mkazo kwa kusema: "na tumewafadhilisha kwa fadhila kubwa kuliko wengi miongoni mwa tulio waumba."

Kwa maelezo tuliyotoa kuhusu nakshi za kuvutia za mchoro wa kustaajabisha wa nafsi ya mwanadamu, tunaweza kubaini na kupata taswira safi na wadhiha ya nafasi ya akhlaqi katika utamaduni uliotukuka na wa kumjenga mwanadamu, wa dini tukufu ya Uislamu. Na sababu ni kwamba, ni kwa kujipamba kwa vito vya thamani aali za kiakhlaqi tu, ndipo thamani ya mwanadamu inapodumu; na kwa sababu hiyo, ndiyo maana wakati Mwenyezi Mungu Mtukufu alipotaka kuitaja sifa bora na tukufu zaidi ya Bwana Mtume Muhammad SAW, kati ya sifa nyingi zisizo na kifani alizopambika nazo mjumbe wake huyo na mbora wa viumbe wake, aliichagua sifa ya tabia na akhlaqi za mtukufu huyo, kama alivyosema katika aya ya nne ya Suratul-Qalam ya kwamba: Na hakika wewe una tabia tukufu. Lakini hata Bwana Mtume SAW mwenyewe, alipotaka kutubainishia sisi watu wa umma wake falsafa ya kubaathiwa na kupewa kwake Utume alisema: "Sikutumwa, isipokuwa nije kukamilisha matukufu ya tabia njema."
Mpendwa msikilizaji sehemu ya tatu ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu imefikia tamati. Hivyo sina budi kukuaga hadi wakati mwingine inshallah, tutakapokutana tena katika sehemu ya nne ya kipindi hiki. Namuomba Mola wa haki akubariki; na amani, rehma na baraka zake ziendelee kuwa juu yako…/