Nov 06, 2022 10:44 UTC
  • Akhlaqi Katika Uislamu (10)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yako mpendwa msikilizaji popote pale ulipo wakati huu. Nakukaribisha kusikiliza sehemu hii ya 10 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu nikiwa na matumaini kuwa, mimi pamoja na wewe tutanufaika na yale tutakayoyasikia katika kipindi hiki. Endelea kuwa nami basi hadi tamati ya mazungumzo yetu.

Kwa mnaofuatilia kwa karibu kipindi hiki bila shaka mngali mnakumbuka kuwa katika mfululizo wetu wa tisa tulieleza kwamba, ili kuweza kujenga na kustawisha thamani za kiakhlaqi katika kila mfumo na jamii, kuna haja ya kuandaa mazingira mwafaka ya kisiasa, kiutamaduni na kiuchumi. Kuhusiana na nukta hiyo tulizungumzia kwa muhtasari mchango wa masuala ya kisiasa na kiutamaduni na tukabainisha kwamba, ikiwa watu safi na wastahiki watashika hatamu za uongozi katika jamii yenye mfumo wa kisiasa, yataweza kuandaliwa mazingira mwafaka ya kujenga na kukuza maadili bora ya kiakhlaqi; na kinyume chake, endapo walioshika hatamu za utawala watakuwa watu waovu na mafisadi, jamii itapotoka na kuporomoka, na mienendo potofu na ya utovu wa maadili na akhlaqi njema ndiyo itakayotawala. Ukiachilia mbali mifumo ya kisiasa, utamaduni pia unatoa mchango mkubwa katika kujenga au kubomoa thamani na tunu za kiakhlaqi. Mchango wa utamaduni ni wenye taathira kubwa kwa kiasi ambacho, madola makubwa ya dunia hutumia kila aina ya mbinu na hila kuhujumu kwa kila namna uhuru na kujitawala kiutamaduni kwa mataifa mengine; na kwa njia hiyo kuhakikisha tamaduni tegemezi za maadili yao ya ufuska na upotofu zinatawala na kufuatwa ndani ya jamii za mataifa hayo, hususan kwenye mifumo yenyewe ya nchi na viongozi mamluki na vibaraka wanaotawala nchi hizo.

Jambo jengine muhimu na lenye kutoa mchango mkubwa katika kujenga mazingira chanya au hasi ya akhlaqi ni sera za kiuchumi. Ukweli ni kwamba, tutarajie thamani za kiakhlaqi kuchanua na kung'ara katika jamii yoyote ile, ikiwa mbali na mifumo safi na sahihi ya kisiasa na kiutamaduni, uchumi safi na sahihi pia utatanda kwenye anga ya jamii hiyo. Lakini iwapo mfumo wowote ule wa utawala, utaongozwa na viongozi na wadau wa sekta ya uchumi walio mafisadi, walariba, walimbilikizaji mali na utajiri kwa njia ya haramu na wafanyaisrafu na mabwanyenye; na mamafia wa mali na madaraka wakawa ndio washika hatamu za uendeshaji ulimwengu wa uchumi, hapana shaka hayatopatikana tena mazingira ya kulelewa na kujitokeza watu waaminifu, wakinaifu, wenye moyo wa kujitolea na wenye kuwaonea uchungu watu; na kwa hali hiyo hatutaweza kupata hata ishara au harufu ya akhlaqi za kiuchumi katika ulimwengu wa uchumi wenye mazonge na misokotano chungu nzima iliyofichikana na isiyojulikana.

Kwa hivyo, kama tunataka kweli watu wazishike barabara thamani za kiakhlaqi, inapasa kila mmoja wetu ahisi kuwa ana jukumu la kujenga mifumo safi ya kisiasa, kiutamaduni na kiuchumi; na kwa muktadha huo tuchape kazi mtawalia na bila kupumua ya kutaalamisha umma na kuzipiga vita tawala na viongozi mafisadi. Tuwe na hima na bidii ya kutokomeza madola yanayoharibu na kufisidi watu wa mataifa mengine na badala yake tuandae mazingira mwafaka ya kujenga thamani za kiutu na kiakhlaqi katika jamii, zitakazotuwezesha kuishi katika dunia inayotawaliwa na maadili mema na usafi wa tabia na akhlaqi. Na ili kuweza kulifikia lengo na tamanio hili takatifu, inatakiwa tuzitakase na kuzijenga kwanza nafsi zetu wenyewe; kwa sababu kila mtu mmoja mmoja katika jamii atakuwa na akhlaqi njema na matokeo yake yatakuwa ni kupatikana jamii njema na safi. Na ndani ya jamii kama hiyo, watapatikana watu safi na wateule wa kushika hatamu za mali na madaraka; na kupitia utamaduni safi na athirifu wa jamii, kutaandaliwa mazingira mwafaka ya kujengwa na kustawishwa tabia na akhlaqi njema. Kuhusiana na nukta hii, kuimarisha mahusiano na mafungamano ni jambo lenye ulazima na udharura mkubwa zaidi. Na njia ya kulifanikisha hilo ni kuufanyia kazi msingi wa "kupata wengi zaidi; na ikibidi, kuwakosa wachache tu".

Ili kuweza kuwafanya watu wengi zaidi wavutiwe na utamaduni wa Uislamu safi na wa asili uliolinganiwa na kufunzwa na Bwana Mtume Muhammad SAW kuna mwongozo wa msingi unaopatikana katika sira ya mtukufu huyo na waja wateule na watoharifu wa kizazi chake, ambao ni nadra kushuhudiwa katika vyuo vingine vya fikra za akhlaqi; kwa sababu katika fikra zingine za akhlaqi, hufuatwa zaidi ule msingi wa 'akutendaye mtende', wa mtu kulipa ubaya kwa ubaya anaotendewa. Lakini katika chuo cha fikra cha akhlaqi za Uislamu, mwenendo na matendo mabaya hulipwa kwa mema na mazuri. Qur'ani tukufu ambayo imejaa mafunzo ya akhlaqi njema, inatueleza yafuatayo katika aya ya 34 ya Suratu-Fuss'ilat: "Mema na maovu hayalingani. Pinga uovu kwa lilio jema zaidi. Hapo yule ambaye baina yako naye pana uadui atakuwa kama rafiki jamaa wa kukuonea uchungu."

Hapana shaka kuwa wanadamu wote hawaachi kuteleza na kufanya makosa, hasa katika kuamiliana na kulahikiana na wenzao. Sababu ni kwamba, kuna wakati, uelewa wa mtu huathiriwa na hisia na hata hasira, mpaka akafika hadi ya kushindwa kudhibiti hisia zake na kufanya mambo ambayo huja kuyajutia pale moto wa hasira alizokuwa nazo unapopoa, akaishia kuomba radhi na kutegemea asamehewe. Ili kuhuisha na kuupa nguvu moyo wa usamehevu katika nafsi za waja wake wanaokosewa, Mwenyezi Mungu Mtukufu, ambaye ni dhihirisho la rehma na usamehevu anatuambia yafuatayo katika sehemu ya mwisho ya aya ya 22 ya Suratu-Nnur: "Na wasamehe, na waachilie mbali. Je! Nyinyi hampendi Mwenyezi Mungu akusameheni? Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu."

Imam Sajjad AS, ambaye ni shakhsia aliyekulia kwenye chuo cha fikra cha akhlaqi cha Qur'ani na ambaye ni ruwaza njema ya sifa zote za kiakhlaqi amenukuliwa akisema: "Kitakaposimama Kiyama, Mwenyezi Mungu Mtukufu atawakusanya wanadamu wote wa tokea mwanzo hadi mwisho wa ulimwengu wa viumbe, kisha atanadi mwenye kunadi "Wako wapi wale wenye fadhila na sifa bora zaidi?  Hapo utajitenga umati mkubwa wa watu, ambao malaika watakwenda kuwalaki na kuwauliza, nini sababu ya nyinyi kuwa bora na wenye fadhila zaidi kuliko watu wengine? Watu hao watajibu: Tuliungana na watu waliokata uhusiano nasi, tuliwasaidia watu waliotunyima tulipokuwa na shida, na tuliwasamehe watu waliotudhulumu na kutufanyia ubaya. Hapo malaika watasadikisha matendo hayo mema ya watu hao na kuwaambia: ingieni peponi."

Kwa hakika kama tutajengeka na tabia na mwenendo huu wa kulipa mema na mazuri kwa mabaya tunayotendewa, tutaishi maisha ya peponi kuanzia papa hapa duniani. Mwenyezi Mungu ajaalie mwenendo na utamaduni huu wa kiakhlaqi utawale katika jamii mbalimbali za watu.

Na kwa maelezo hayo basi mpendwa msikilizaji niseme pia kwamba, sehemu ya 10 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu imefikia tamati. Hivyo sina budi kukuaga hadi wakati mwingine inshallah, tutakapokutana tena katika sehemu ya 11 ya kipindi hiki. Namuomba Mola wa haki akubariki; na amani, rehma na baraka zake ziendelee kuwa juu yako…/