Akhlaqi Katika Uislamu (11)
Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yako mpendwa msikilizaji popote pale ulipo wakati huu. Nakukaribisha kusikiliza sehemu hii ya 11 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu nikiwa na matumaini kuwa, mimi pamoja na wewe tutanufaika na yale tutakayoyasikia katika kipindi hiki. Endelea kuwa nami basi hadi tamati ya mazungumzo yetu.
Kwa kila mfuatiliaji wa karibu wa kipindi hiki bila shaka angali anakumbuka kuwa, katika kipindi kilichopita tulieleza kwamba, kwa mujibu wa mafundisho ya dini ya Uislamu, ikiwa tunataka mahusiano ya kiutu yawe imara na madhubuti, inapasa tufumbie macho miamala mibaya ya watu wanapoteleza na kutukosea na tujitahidi kuchukua misimamo chanya na athirifu ili tuweze kuvutia zaidi watu. Moja ya sifa za kiakhlaqi yenye taathira kubwa sana katika kuzikurubisha nyoyo na kuzifanya ziwe kitu kimoja, ni msingi wa "hulka njema". Ifahamike vyema kwamba madhumuni ya hulka njema si tabia na mwenendo wa muda, wa kimaslahi na wa kujionyesha tu. Lakini madhumuni hasa ni tabia njema ya kudumu na endelevu isiyochanganyika na aina yoyote ile ya ufanyaji mambo kwa kujionyesha ili kuwahadaa watu. Mtu aliyelelewa na kukulia katika chuo cha malezi ya kiakhlaqi cha Uislamu, huwa katika kila hali anaamiliana na watu kwa hulka na muamala mwema bila ya kuwa na nia au matashi yoyote mabaya. Mtu mmoja alimuuliza Imam Jaafar Sadiq AS, "mtu mwenye akhlaqi njema huwa na sifa na alama gani?" Mtukufu huyo akawambia: "huwa mpole na mnyenyekevu kwa wenzake, anasema maneno mema na mazuri na anaamiliana na watu kwa bashasha."
Katika utamaduni wa malezi ya Uislamu wa asili, kuna mfungamano wa msingi kati ya imani na itikadi za kidini kwa upande mmoja na misingi na thamani za kiakhlaqi kwa upande mwingine; suala ambalo linabainishwa na maneno matukufu ya Imam Muhammad Baqir AS aliposema: "Waliokamilika kiimani ni wale walio na akhlaqi njema zaidi miongoni mwa watu."
Kudhihiri na kushuhudiwa msingi huu inapasa kuthibiti ndani ya jamii yenyewe na katika tabia za watu wenyewe. Bwana Mtume Muhammad SAW, ambaye ni dhihirisho na nembo kuu ya thamani na matukufu ya kiakhlaqi alikuwa akiwaambia masahaba zake: "Walio wabora zaidi katika nyinyi ni wale wenye mlahaka mzuri zaidi wa kiakhlaqi wanapolahikiana na watu; na wanaoamiliana na watu kwa unyenyekevu; wanaojenga mazoea nao (kwa kusuhubiana nao kwa uchangamfu) kiasi cha wao pia kuonyesha hamu kubwa ya kujenga mazoea na uhusiano nao."
Kielezi kingine cha thamani za Uislamu ni jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu, ambayo imetiliwa mkazo sana na kwa wingi katika aya za Qur'ani na Hadithi; kiasi kwamba hadhi na daraja ya juu waliyonayo mujahidina na wanaopigana katika njia ya Mwenyezi Mungu vimeadhimishwa kwa namna isiyo na kifani. Ni muhimu kuashiria pia kwamba katika utamaduni wa kiakhlaqi wa Uislamu, malipo ya thawabu ayapatayo mtu mwenye tabia na akhlaqi njema yanalingana na ya mwenye kupigana jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu. Imam Jaafar Sadiq AS amesema: "Ni hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu anawapa malipo ya thawabu watu wenye tabia njema, sawa na thawabu anazopata mtu anayepigana jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu asubuhi na jioni."
Lakini mbali na hayo, akhlaqi nzuri na tabia njema huotesha mbegu ya huba ndani ya nyoyo na ndiyo sababu kuu ya kuimarika uhusiano wa kirafiki na wa kiupendo, kwa sababu kwa kawaida, watu wa jamii yoyote ile huvutiwa na kuwapenda watu tabia na akhlaqi njema. Imam Muhmmad Baqir AS amelielezea hilo kwa kusema: "Waja wema wenye akhlaqi nzuri na wacheshi huwafanya watu wawapende…"
Kwa upande mwingine, wakati manukato ya machanuo ya mahaba na upendo yanaposambaza harufu yake ndani ya anga ya jamii; na maua na mimea ya huba na upendo yakatoa matunda yake, nyasi, miba na magugu ya uvundo wa kinyongo hung'oka na kutoweka kikamilifu. Bwana Mtume Muhammad SAW, ambaye kutokana na tabia na akhlaqi yake njema aliweza kuuzima katika zama za ujahilia moto wa ghadhabu na vinyongo na kujaza katika jamii aliyoishi ndani yake mapenzi na utangamano na kuziunganisha pamoja nyoyo za watu, amesema kuhusu jambo hilo ya kwamba: "Tabia njema na bashasha huondoa kinyongo ndani ya moyo."
Mpendwa msikilizaji, vilevile inapasa tufahamu kwamba, tabia na akhlaqi njema zinachangia pia katika ujenzi na ustawi wa jamii ya wanadamu; na kutokana na mchango wake wa kuzipa utulivu roho na akili, huandaa mazingira ya kupatikana maisha ya raha, uchangamfu na uchapajikazi na hivyo kuongeza na kurefusha kiwango cha umri na mategemeo ya kuishi kwa watu. Imam Jaafar Sadiq (as) ameitilia mkazo nukta hii kwa kusema: "Wema na tabia njema huzistawisha nyumba na kuongeza umri."
Huenda mtu ikampitikia akilini mwake kujiuliza suali hili, kwamba kuna uhusiano gani kati ya tabia na akhlaqi njema na kustawi kwa nyumba na familia na kuongezeka umri na uhai wa mtu? Hakuna shaka kuwa, wakati utamaduni wa wema na tabia nzuri unapotanda ndani ya anga ya jamii yoyote ile, matokeo na matunda yake huwa ni kupatikana suluhu, utulivu, amani na upendo na nyumba na taasisi zote za ujengaji familia na maisha katika jamii hubakia imara, pasi na kuwepo ishara na alama yoyote ya chuki, vinyongo, ugomvi na vita; na wala nyoyo za watu hazitawaliwi na tafrani wala msongo wa mawazo; na matokeo yake huwa ni kurefuka umri wao na kuongezeka kiwango cha matarajio yao ya kuishi. Ikiwa katika zama zetu hizi tunashuhudia ongezeko la takwimu za watu wenye msongo wa mawazo na vifo vya mapema na kabla ya wakati, tujue kwamba sababu muhimu zaidi ya kushamiri mabalaa hayo ni kutoweka na kupotea utamaduni wa kufanyiana wema, upendo, akhlaqi na tabia njema; na badala yake taasisi na duru za wenye nguvu za utajiri wa mali na madaraka kutawaliwa na chuki, vinyongo, mifarakano na hulka za kushupalia na kuwasha moto wa vita; ambayo ni mambo yanayoinyima na kuikosesha jamii usingizi wa amani na utulivu; kwa sababu badala ya kuzistawisha na kuzinawirisha nyumba na maskani za watu, huzigeuza magofu na vihame kwa kuziangamiza na kuzidamirisha kutokana na kuharibu taasisi za maisha na familia; na matokeo ya sera na mwenendo huo huwa ni kuifanya jamii nzima ya wanadamu duniani ikose raha na utulivu.
Na kwa maelezo hayo basi mpendwa msikilizaji niseme pia kuwa, sehemu ya 11 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu imefikia tamati. Hivyo sina budi kukuaga hadi wakati mwingine inshallah, tutakapokutana tena katika sehemu ya 12 ya kipindi hiki. Namuomba Mola wa haki akubariki; na amani, rehma na baraka zake ziendelee kuwa juu yako…/