Nov 06, 2022 11:08 UTC
  • Akhlaqi Katika Uislamu (14)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yako mpendwa msikilizaji popote pale ulipo wakati huu. Nakukaribisha kusikiliza sehemu hii ya 14 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu nikiwa na matumaini kuwa, mimi pamoja na wewe tutanufaika na yale tutakayoyasikia katika kipindi hiki. Endelea kuwa nami basi hadi tamati ya mazungumzo yetu.

Tukiendeleza na mazungumzo yetu kuhusu tabia na akhlaqi njema, kielelezo kingine muhimu cha tabia njema ni kuwa mkweli na kusema kweli, sifa ambayo inapasa ionekane na kushuhudiwa katika maneno na vitendo vya mtu. Kama utakuwepo mlingano, kwa maneno ya mtu kuendana na vitendo vyake, hilo litathibitisha ukweli wa mtu anayesema kweli. Kuhusiana na nukta hii, Mwenyezi Mungu Mtukufu ametajwa ndani ya Qur'ani tukufu kuwa ni dhihirisho la sifa zote za ukweli, ambazo inapasa apambike nazo kila mwenye kushikamana na njia ya tauhidi. Aya ya 87 ya Suratun-Nisaa inaizungumzia hivi nukta hiyo: Mwenyezi Mungu, hapana mungu isipo kuwa Yeye. Kwa yakini atakukusanyeni Siku ya Kiyama. Halina shaka hilo. Na ni nani msema kweli kuliko Mwenyezi Mungu?

Moja ya ishara za wazi na alama kubwa kabisa za ukweli wa Mwenyezi Mungu ni kuthibiti kwa ahadi alizotoa Yeye Mola; ziwe ni ahadi ambazo ameziahidi kutokea hapa duniani, au ahadi alizoahidi kuwa zitatokea katika ulimwengu mwingine wa akhera. Qur'ani tukufu inalizungumzia hilo katika aya ya 122 ya Suratun-Nisaa kwa kusema: … Ndiyo ahadi ya Mwenyezi Mungu iliyo kweli. Na nani mkweli zaidi kwa usemi kuliko Mwenyezi Mungu.

Mwenyezi Mungu, ambaye ni dhhirisho la sifa zote za ukweli na msema kweli anawataka wale wanaofuata njia ya tauhidi na kumwabudu Yeye Mola pekee wa haki wapate ilhamu na kufuata kigezo chake Yeye cha kuwa wakweli na wasema kweli katika tabia, maneno na vitendo na kushikamana na njia hiyo katika tamu na chungu na raha na misukosuko wanayokumbana nayo maishani. Katika aya ya 23 ya Suratul-Ahazab, Qur'ani tukufu inaeleza yafuatayo katika kuwazungumzia watu wanaojipamba na sifa hiyo: Miongoni mwa Waumini wapo watu walio timiza waliyo ahidiana na Mwenyezi Mungu. Baadhi yao wamekwisha kufa, na baadhi wanangojea, wala hawakubadilisha (ahadi) hata kidogo.

Ni kwa sababu hii ndio maana watu wakweli wana hadhi maalumu na ya juu mbele ya Mwenyezi Mungu mpaka kufikia hadi ya kuwekwa na Yeye Mola kwenye daraja na kundi moja na waja wake makhsusi na wateule. Mwenyezi Mungu Mtukufu analieleza hilo katika aya ya 69 ya Suratun-Nisaa isemayo: Na wenye kumt'ii Mwenyezi Mungu na Mtume, hao wa pamoja na wale alio waneemesha Mwenyezi Mungu miongoni mwa Manabii, na Masiddiqi, na Mashahidi, na Watu wema. Na uzuri ulioje kuwa pamoja na watu hao!

Katika ulimwengu huu, upo uwezekano kwa watu kujionyesha kidhahiri kwamba wakweli; na kwa kufanya hivyo wakaweza kuzivuta na kuziteka fikra za waliowengi. Na sababu ni kwamba katika dunia yetu hii, huwa tunawatathmini watu kwa yale tunayonayo katika dhahiri zao; iwe ni maneno au mienendo yao. Na yamkini tukaishi nao hadi mwisho wa uhai wao pasi na kuitambua hakika na dhati yao. Lakini kesho Siku ya Kiyama, ambapo pazia la dhahiri ya mambo litaondolewa na kumfanya mtu asiweze kuficha chochote kuhusu hakika yake, ni ukweli halisi tu wa tabia na matendo yake ndio utakaoweza kumfaa na kuwa na faida naye na kumfanya apate radhi za Mwenyezi Mungu.

Mwenyezi Mungu, Mola Mwenye Enzi, ambaye ni Mjuzi mwenye uelewa kamili, wa kina na wa pande zote wa siri zote za ulimwengu, katika hali zake zote za siri na dhahiri atasema Siku ya Kiyama, kama inavyoeleza aya ya 119 ya Suratul Maaidah ya kwamba:  Hii ndiyo Siku ambayo wasemao kweli utawafaa ukweli wao. Wao watapata Bustani zipitazo mito kati yake. Humo watadumu milele. Mwenyezi Mungu amewawia radhi, nao wawe radhi naye. Huku ndiko kufuzu kukubwa.

 Mojawapo ya njia inayoweza kutufanya tuwatambue watu walio wakweli ni kutathmini mwenendo na matendo yao. Kwa maneno mengine, inapasa tuangalie ni kwa kiwango gani wanaojinasibu kuwa wakweli na wasemakweli wanafungamana na misingi na malengo matukufu wanayoyapigania na kama wako tayari kwa kila walichonacho kujitokeza katika medani za jihadi na mapambano ya kukabiliana na adui ili kuyalinda na kuyafanikisha malengo hayo. Katika aya ya 15 ya Suratul-Hujuraat, Qur'ani tukufu inavitaja vigezo vya kutumia kuwapimia watu hao kwa kusema: Hakika Waumini ni wale walio muamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake tena wasitie shaka kabisa, na wakapigana Jihadi katika Njia ya Mwenyezi Mungu kwa mali yao na nafsi zao. Hao ndio wakweli. 

Bila ya shaka, hakuna jambo linaloweza kuwa na taathira kubwa ya kuziteka na kuzivuta nyoyo na nafsi za watu ziyakubali na kuyafuata malengo na thamani za Kiislamu, kama ulivyo ukweli katika mwenendo na matendo. Kusema kweli, kama mtu anayejifunga na masuala ya dini ataacha kutoa kauli nyepesi na za ujanjaujanja na badala yake akajitahidi kuwa mkweli kwa kauli na matendo yake katika tablighi ya kueneza mafundisho ya Uislamu halisi wa asili na kufanikisha malengo matukufu ya kidini na ya kiutu, hapana shaka kufanya hivyo kutakuwa na taathira kubwa zaidi kuliko jambo jengine lolote.

Imam Jaafar Sadiq AS, ambaye kutokana na ukweli wake wa kauli na matendo alileta mageuzi makubwa zaidi ya kiutamaduni na Kiislamu katika zama zake, katika moja ya miongozo yake athirifu ameusia kwa kusema: Msiwalinganie watu mema na ya kheri kwa ndimi zenu, bali fanyeni hivyo kwa matendo yenu. Inatakiwa watu waangalie jithada zenu za kivitendo (katika nyanja zote), na kushuhudia ukweli na uchaMungu wenu. (Usulul-Kafi, Mlango wa Ukweli na Kuchunga Amana)

Kwa maelezo hayo mpendwa msikilizaji tunafikia hitimisho kwamba, katika zama zetu hizi ambazo zinashuhudia mpambano mgumu na wa wazi kabisa baina ya haki na batili, huku vinara wa ukafiri duniani wakitumia kila mbinu na nyenzo ili kuichafua sura safi ya Uislamu, njia bora zaidi ya kukabiliana na njama na hila zao ni kuitangaza na kuilingania dini yetu hiyo kivitendo na kwa nia safi na ya kweli.

Inatakiwa Waislamu watekeleze jukumu na masuulia mazito waliyonayo zaidi katika zama hizi kuliko ilivyokuwa wakati wowote ule huko nyuma; na badala ya kutoa kauli tupu na za kujionyesha tu wawe wakweli katika mwenendo na matendo yao, ili kwa kufanya hivyo waandae mazingira ya kuufanya Uislamu uzidi kuenea na kuzivutia nyoyo nyingi zaidi duniani siku baada ya siku.

Huku tukiwa na matumaini ya kuthibiti tamanio hilo niseme pia mpendwa msikilizaji kwamba sehemu ya 14 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu imefikia tamati. Hivyo sina budi kukuaga hadi wakati mwingine inshallah, tutakapokutana tena katika sehemu ya 15 ya kipindi hiki. Namuomba Mola wa haki akubariki; na amani, rehma na baraka zake ziendelee kuwa juu yako…/