Nov 06, 2022 15:05 UTC
  • Akhlaqi Katika Uislamu (18)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yako mpendwa msikilizaji popote pale ulipo wakati huu. Nakukaribisha kusikiliza sehemu hii ya 18 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu nikiwa na matumaini kuwa, mimi pamoja na wewe tutanufaika na yale tutakayoyasikia katika kipindi hiki. Endelea kuwa nami basi hadi tamati ya mazungumzo yetu.

Kwa kila msikilizaji wa kawaida wa kipindi hiki bila shaka angali anakumbuka kuwa katika kipindi kilichopita tulizungumzia umuhimu wa umoja kwa Ulimwengu wa Kiislamu unaosimama juu ya msingi wa imani juu ya Mwenyezi Mungu; na tukakumbusha na kutanabahisha kuwa katika karne hii, ambapo maadui wamejizatiti na kujifunga kibwebwe ili kuuangamiza Uislamu na Waislamu, kwa kutumia akili kidini na kisiasa, tutabaini kuwa, Waislamu, hawana njia nyingine ya kufanya isipokuwa kuungana na kuasisi kambi moja yenye nguvu na iliyo kitu kimoja kwa ajili ya kukabiliana na maadui wa Ulimwengu wa Kiislamu; na mpambano huo utakaoamua juu ya hatima yao, unahitaji subira na istiqama, sambamba na wao wenyewe kuimarisha uhusiano wao katika masuala ya kidini yanayowaunganisha pamoja. Katika aya ya 200 na ya mwisho ya Suratu Aaal-Imran, Mwenyezi Mungu ametilia mkazo udharura wa waumini kuwa na subira na kusimama imara alipotwambia: Enyi mlio amini! Subirini, na shindaneni kusubiri, na kuweni macho, na mcheni Mwenyezi Mungu, ili mpate kufanikiwa. 

Msingi na nguzo muhimu zaidi unayosimamia umoja wa Waislamu ni kuwepo kiongozi mwadilifu wa kidini, ambaye kutokana na kuwa na taqwa na uchaMungu uliojengeka ndani ya nafsi yake huwa hafuati chochote ghairi ya amri za Mwenyezi Mungu. Anapambana na kila aina ya udhaifu wa umimi na ubinafsi na matamanio ya nafsi. Anailinda mipaka ya dini ya Uislamu na thamani zake kwa uwezo wake wote; na kama anawalingania Waislamu kuwa na mshikamano na umoja, basi hafanyi hivyo kwa lengo jengine lolote lile isipokuwa kuilinda dini na kuuletea nguvu, izza na heshima Ulimwengu wa Kiislamu.

Katika aya ya 73 ya Suratul-Anbiyaa Qur'ani tukufu inazitaja sifa maalumu za viongozi wanaofuata miongozo ya Mwenyezi Mungu kwa kusema: Na tukawafanya maimamu wakiongoa watu kwa amri yetu. Na tukawafunulia watende kheri, na washike Sala, na watoe Zaka; na walikuwa wanatuabudu Sisi tu.

Wakati jamii ya Kiislamu inapoongozwa na kiongozi kama huyo, ikafuata miongozo na utaalamishaji wake na ikaendesha mambo yake kwa ajili ya kutaka radhi za Mwenyezi Mungu ndipo huweza kuunda kambi yenye nguvu na iliyo kitu kimoja na kukabiliana na kambi ya adui. Ukweli ni kwamba Waislamu wanaunganishwa pamoja na mambo mengi ya kiitikadi na kimatendo ambayo yanawafungamanisha kwa umadhubuti mkubwa kinyume na mipaka bandia waliyowekewa ya kuwafarakanisha. Mwenyezi Mungu, ambaye ndiye mwenye kuziunganisha nyoyo na kupatikana upendo baina ya watu anatueleza yafuatayo katika aya ya 71 ya Suratu-Tawba: Na Waumini wanaume na Waumini wanawake wao kwa wao ni marafiki walinzi. 

Bwana Mtume SAW, ambaye ndiye aliyeasisi umoja wa Waislamu alipowafungisha masahaba zake ahadi ya udugu baina yao, anaibainisha kama ifuatavyo maana halisi ya mafungamano ya waumini: "Mfano wa waumini katika kupendana kwao, na kuhurumiana kwao na kujaliana kwao ni mithili ya kiwiliwili, kinapoumwa kiungo chake kimoja, viungo vingine vilivyosalia navyo pia hukosa raha na utulivu."

Ushabihishaji huu unabainisha kwamba, jamii ya Waislamu inapasa iwe mithili ya kiwiliwili kimoja, ambapo itokeapo kiungo au mtu mmoja katika jamii ya Kiislamu akasibiwa na jambo au kuumia, wenzake wote katika Ulimwengu wa Kiislamu watahisi wana jukumu na masuulia kwake yeye na watachukua hatua kumsaidia. Katika Hadithi nyingine inayohusiana na maudhui hiyo, Bwana Mtume SAW amesema: "Mtu anayepambazukiwa na asubuhi bila kulipa umuhimu suala la kuchukua hatua ya kutatua matatizo ya Waislamu si Muislamu wa kweli."

Ili kuwafanya Waislamu wawe daima wanaendeleza na kudumisha mshikamano na umoja baina yao, Uislamu umewawekea utaratibu na mazingira ya kuufanya uhusiano wa jamii ya Kiislamu uwe imara na madhubuti.

Miongoni mwa utaratibu huo ni kushiriki Sala ya jamaa, ambapo Waislamu hutakiwa kila siku wahudhurie kwenye ngome kuu na muhimu ya dini yao, yaani misikitini ili kusali kwa pamoja wakiwa kwenye safu zilizoungana na kushikamana. Kushirikiana pamoja katika misiba na furaha na dhiki na raha; kubadilishana mawazo juu ya masuala ya kijamii na ustawi wao wa kiutamaduni, kisiasa na kiuchumi; kuwatatulia shida zao kiuungwana na kuwakidhia mahitaji yao wanyonge na wasio na uwezo miongoni wao, kuchangia shughuli za kijamii na kuitumia pia misikiti yao kuendesha mafunzo ya dini ili kuongeza uwelewa na ufahamu wa waumini na kurasimisha na kuimarisha itikadi na imani zao.

Mazingira na utaratibu mwingine ambao umepangwa na Uislamu kwa ajili ya kudumisha umoja na mshikamano wa Waislamu ni wa Sala ya Ijumaa, ambayo maandalizi yake huwa ya upeo wa juu zaidi na mahudhurio na ushiriki wake huwa wa idadi kubwa zaidi ya waumini, ambapo Khatibu wa Sala hiyo hutakiwa aitumie fursa katika hotuba zake kuwabainishia na kuwataalamisha waumini juu ya masuala yote yanayoendana na wakati kulingana na mahitaji ya jamii yao.

Kielelezo na dhihirisho la upeo wa juu kabisa la umoja wa Ulimwengu wa Kiislamu linaonekana katika kongamano la Hija, ambapo kila mwaka mamilioni ya Waislamu hukusanyika mbele ya Al Kaaba kuunadi wito wa tauhidi na imani ya Mungu mmoja wa haki. Katika hadhara hiyo adhimu ubora wote wa kidhahiri na kimaada hutoweka, kwa watu wote kuvaa vazi la aina moja na rangi moja ili kutekeleza amali za Hija. Kongamano hilo huwabainishia maadui adhama ya Ulimwengu wa Kiislamu, ambapo waumini hupaza sauti zao kutangaza kujibari na kujitenga kwao na makafiri na washirikina na wakati huo huo kuonyesha upendo na mshikamano baina yao, sifa na hali ambayo imebainishwa kwa uwazi na kama ifuatavyo katika aya ya 29 ya Suratu-Fat-h:  Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu. Na walio pamoja naye wana nguvu mbele ya makafiri, na wanahurumiana wao kwa wao. 

In shaa Allah katika zama zetu hizi, ambapo Ulimwengu wa Kiislamu umepata uhai na mwamko mpya, Waislamu washikamane barabara na mafundisho ya Uislamu wao wa asili na kuunganisha zaidi na zaidi safu zao ili kutowapa mwanya wowote maadui zao kujipenyeza na kupandikiza mbegu za unafiki na mfarakano baina yao wakapata fursa ya kuwadhibiti tena na kuwatawalia mustakabali wao. Na kwa dua hiyo ya kheri mpendwa msikilizaji, niseme pia kwamba sehemu ya 18 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu imefikia tamati. Hivyo sina budi kukuaga hadi wakati mwingine inshallah, tutakapokutana tena katika sehemu ya 19 ya kipindi hiki. Namuomba Mola wa haki akubariki; na amani, rehma na baraka zake ziendelee kuwa juu yako…/

 

 

 

Tags