Nov 07, 2022 09:03 UTC
  • Akhlaqi Katika Uislamu (24)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yako mpendwa msikilizaji popote pale ulipo wakati huu. Nakukaribisha kusikiliza sehemu hii ya 24 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu nikiwa na matumaini kuwa, mimi pamoja na wewe tutanufaika na yale tutakayoyasikia katika kipindi hiki ambacho kwa leo kitazungumzia nafasi na umuhimu wa suala la Kuamrisha Mema na Kukataza Mabaya katika Uislamu. Endelea kuwa nami basi hadi tamati ya mazungumzo yetu.

Mpendwa msikilizaji, bila shaka ungali unakumbuka kuwa katika sehemu kadhaa zilizopita za kipindi hiki tumezungumzia baadhi ya thamani za kiakhlaqi, ambazo zinatakiwa zitawale katika jamii ya Kiislamu na tukasisitiza kuwa haitupasi kwa namna yoyote na katika mazingira yoyote yale kughafilika na mambo yanayoweza kuidhuru jamii hiyo kwa kuondoa umoja na kuleta utengano; badala ya mshikamano ukazuka mfarakano na makabiliano baina ya Waislamu; badala ya wao kutetea uadilifu wakawa waungaji mkono na waridhiaji wa dhulma; na badala ya kuishi kwa suluhu na amani wakajitumbukiza kwenye lindi la vita na umwagaji damu baina yao.

Njia bora na athirifu zaidi ambayo Uislamu umeiweka kwa ajili ya kulinda mipaka ya thamani na tunu za Kiislamu na kukabiliana na mambo yaliyo dhidi ya thamani hizo aali na ambayo inaweza kuhafifisha madhara ya mambo hayo hadi kiwango cha chini kabisa ni kuzingatia misingi miwili mikuu ya "Kuamrisha Mema", yaani kulingania kufanya mema na "Kukataza Mabaya", yaani kuzuia mambo ya dhalala na upotofu; misingi ambayo ina nafasi maalumu na umuhimu mkubwa wenye taathira isiyo na kifani katika utamaduni adhimu wa Kiislamu.

Ili kupata ufahamu na uelewa mpana zaidi wa suala hili, tunayaanza mazungumzo yetu kwa maneno matukufu ya wahyi kama anavyotuhutubu Mwenyezi Mungu Mtukufu katika aya ya 104 ya Suratu Aal Imran ya kwamba: Na liwepo miongoni mwenu kundi lenye kulingania kheri na kuamrisha mema na kukataza maovu. Na hao ndio wenye kufaulu.

Kwa hivyo kuwaamrisha watu watunze thamani za kimaadili na kupambana na mambo yaliyo dhidi ya thamani hizo ni suala la kidini, linalowabebesha jukumu zito watu wote katika jamii hasa viongozi wa kidini na kisiasa wa jamii ya Kiislamu. Ili kuonyesha nafasi na umuhimu mkubwa wa misingi hii miwili ya kiakhlaqi na ya mwenendo wa kijamii, Mwenyezi Mungu Mtukufu anatueleza hivi katika ya 110 ya sura hiyohiyo ya Aal Imran: "Nyinyi mmekuwa umma bora mliotolewa kwa watu, kwa kuwa mnaamrisha mema na mnakataza maovu, na mnamuamini Mwenyezi Mungu.”

Hakuna shaka yoyote kuwa, umma wa Kiislamu utaweza kubaki kuwa na hadhi na nafasi hii ikiwa utaendelea kutekeleza jukumu na masuulia haya makubwa na kudumu katika kulinda thamani za mambo mema na kupambana na maovu na mabaya, yaliyo dhidi ya thamani hizo. Msingi mkuu unaoakisi hali na sifa hiyo maalumu ni wa imani juu ya Mwenyezi Mungu, ambao unawafanya waumini waasisi kambi moja iliyoungana ndani ya jamii, inayolinda thamani za maadili mema katika nyanja zote za kidini, kisiasa, kiakhlaqi, kiutamaduni na kiuchumi; na kuzuia kupenya mambo yanayokinzana na thamani hizo ili kuhakikisha jamii inapambika kwa sifa njema za kiakhlaqi na za kiutu na kutoharibiwa na aina yoyote ile ya uchafu wa maovu na ufisadi.

Qur'ani tukufu inatupa taswira ya kambi hiyo iliyoungana na inayotambua na kutekeleza ipasavyo wajibu na majukumu yake, kama inavyoeleza aya ya 71 ya Suratu-Tawba ya kwamba: "Na Waumini wanaume na Waumini wanawake wao kwa wao ni marafiki walinzi. Huamrisha mema na hukataza maovu, na hushika Sala, na hutoa Zaka, na humt'ii Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Hao Mwenyezi Mungu atawarehemu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mtukufu Mwenye nguvu, Mwenye hikima."

Kwa mtazamo wa kiujumla tunaweza kufikia hitimisho kwamba katika jamii ambayo ni ya Kiislamu, inapasa watu wake wawe waumini wa kweli; na moyo wa utiifu kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake uonekane katika matendo yao; na daima wawe na hima na bidii ya kulinda thamani za mambo mema na kupambana na mambo yaliyo dhidi ya thamani hizo; wajihisi wana jukumu na masuulia, na wala wasipuuze na kudharau kutimizia wajibu wao kwa namna yoyote ile.

Ili tuwe na uelewa na ufahamu wa kina zaidi kuhusu nafasi ya msingi wa kuamrisha mema na kukataza mabaya na kutambua ni taathira gani za msingi unaweza kutoa katika mageuzi ya pande zote ya jamii ya Kiislamu, hebu tuyategee sikio kwa pamoja maneno matukufu ya Imam Muhammad Baqir (as), ambaye ni mhuishaji wa utamaduni wa Uislamu asili. Mtukufu huyo anasema: "Kuamrisha mema na kukataza mabaya ni mwenendo na sira ya Mitume wa Mwenyezi Mungu na mwenendo na mwongozo unaofuatwa na watu wema. Mawili haya yana hadhi na nafasi kubwa, kwa sababu mambo mengine ya wajibu katika dini yanaweza kusimamishwa kutokana na hayo. (Kwa kuzuiliwa ulajimali wa haramu), njia za kwenda na kurudi za kutafuta riziki zinakuwa katika amani na mapato huwa ya halali, haki (zilizonyimwa za waliodhulumiwa) zinalindwa, mali zilizoporwa zinarejeshwa kwa wamiliki (halisi), ardhi zilizoghusubiwa (na wanyang'anyi wenye vyeo na madaraka zinarejeshwa na) zinastawishwa, maadui wanalipiziwa visasi na hatimaye masuala yote (na mambo ya uendeshaji wa jamii) yafanywayo ndivyo sivyo na kwa ukiukaji wa sheria yanarekebishwa na kuwekwa sawa. (Al-Kafi 1/56/5)

Hakuna shaka yoyote kuwa, mafanikio yote haya chanya na mazuri hupatikana, pale watu wote katika jamii ya Kiislamu wanapotekeleza jukumu lao la kijamii la kulinda thamani za maadili mema na kupambana na mambo yaliyo dhidi ya maadili hayo. Vyenginevyo, watu hao watahiliki kwenye maangamizi ya dhulma za madhalimu na majabari na hawatampata yeyote wa kuwasaidia.

Imam Ali (AS) anatubainishia taswira hiyo kwa kutuusia kama ifuatavyo:” Msiache kuamrisha mema na kukataza mabaya na wala msighafilike nako; kwani kama mtaacha kutekeleza majukumu haya mawili, waovu watakutawalini. Na itapofika hali hiyo, dua zenu mtakazoomba kwa Mwenyezi Mungu hazitajibiwa.” (Nahjul-Balaghah, Barua ya 47).

Na kwa wasia huo wa Imam Ali (AS) niseme pia kuwa, sehemu ya 24 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu imefikia tamati. Hivyo sina budi kukuaga mpendwa msikilizaji hadi wakati mwingine inshallah, tutakapokutana tena katika sehemu ya 25 ya kipindi hiki. Namuomba Mola wa haki akubariki; na amani, rehma na baraka zake ziendelee kuwa juu yako…/