Akhlaqi Katika Uislamu (27)
Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yako mpendwa msikilizaji popote pale ulipo wakati huu. Nakukaribisha kusikiliza sehemu hii ya 27 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu nikiwa na matumaini kuwa, mimi pamoja na wewe tutanufaika na yale tutakayoyasikia katika kipindi hiki ambacho kwa leo kitaendelea kuzungumzia sifa za familia bora kwa mtazamo wa dini tukufu ya Uislamu. Endelea kuwa nami basi hadi tamati ya mazungumzo yetu.
Kama unavyokumbuka mpendwa msikilizaji, katika sehemu ya 26 ya kipindi hiki tulieleza kwamba katika familia bora ya Kiislamu iliyo mfano wa kuigwa, si tu wazazi wanajipangia ratiba maalumu ya malezi ya watoto wao na kuifanyia kazi kwa juhudi na uwezo wao wote, lakini pia wanaipa uzito mkubwa nafasi na mchango wa familia safi na salama katika vizazi vijavyo. Kwa maneno mengine ni kuwa, akina baba na akina mama walioshika dini na wenye uelewa wa majukumu yao, wanatambua vyema ukweli huu, wa kwamba kama watalea na kukuza watoto wema, hapana shaka watakuwa wametoa mchango athirifu na muhimu sana katika muelekeo wa vizazi vijavyo.
Suala muhimu zaidi na lenye ufanisi mkubwa zaidi katika malezi ni msukumo wa kimaanawi na kiitikadi, ambao vielelezo na madhihirisho yake ni kumkumbuka Mwenyezi Mungu kwa kusimamisha Sala, kuomba dua na kushtakia hali kwake Yeye Mola. Lakini mbali na kuwa na mtazamo wa kitauhidi juu ya ulimwengu, msingi wa maadi au kufufuliwa viumbe ni mwega mwingine imara na madhubuti unaowapa watu mwanga mpya na kubainisha ukweli kwamba, maisha ya mwanadamu hayakomei katika dunia hii ya kimaada yenye mwisho na inayomalizika; na kwamba, baada ya kifo, mwanadamu atapambazukiwa na ulimwengu mwingine wa milele.
Na kutokana na mtazamo huu, kuna mshikano na mfungamano usioweza kutenganika kati ya hatima ya familia katika dunia hii na katika ulimwengu wa baada ya kifo. Kwa ufafanuzi zaidi ni kwamba, jamaa wote walio wema katika kila familia wataungana na kukutana tena kwenye Pepo yenye neema za milele kesho Siku ya Kiyama.
Qur'ani tukufu inaeleza yafuatayo katika aya ya 20 ya Suratu-Ra'ad kuhusu sifa bora ambazo walikuwa nazo watu wa familia bora za Kiislamu: "Wale ambao wanatimiza ahadi ya Mwenyezi Mungu, wala hawavunji maagano."
Madhumuni ya ahadi na maagano hayo, ni ahadi ya tauhidi ambayo Mwenyezi Mungu ameitia kwenye maumbile ya watu wote, ambayo kwayo, wanaomwamini Mwenyezi Mungu wanadhihirisha uja wao Kwake na kumwabudu Yeye peke yake. Hawawi tayari katu kuivunja ahadi hiyo wakamwabudu Shetani, matamanio ya nafsi zao wala mambo ya starehe na anasa. Na huu ni msingi muhimu ambao huivua familia bora pingu na minyororo yote hiyo na kuhuisha moyo wa mja huru kwa watu wa familia hiyo. Aya ya 21 ya Suratu-Ra'ad inazitaja kama ifuatavyo sifa zingine za watu hao: "Na wale ambao huyaunga aliyo amrisha Mwenyezi Mungu yaungwe, na wanaikhofu hisabu mbaya."
Japokuwa watafiti wa masuala ya Qur'ani wanaeleza kwamba uga wa mambo yanayokusudiwa kuungwa ni mpana mno na unajumuisha mawasiliano na mafungamano na Mwenyezi Mungu, Mitume, viongozi wa dini, waja wateule, marafiki, majirani walio ndugu wa kidini na watu wengine wote, lakini uunganishaji na uhusiano uliotiliwa mkazo zaidi hapa kuliko chochote kile ni wa kifamilia na wa jamaa zake mtu.
Hakuna shaka yoyote kuwa, kuimarisha uhusiano wa kifamilia na wa kiudugu ambao ni jambo linalompendeza Mwenyezi Mungu, kunajenga pia utamaduni wa kuimarisha mahusiano ya kijamii. Na bila shaka msukumo na mwega madhubuti zaidi unaolifanya suala la mfungamano na mahusiano liwe thabiti na endelevu ni watu kuzingatia adhama ya Mwenyezi Mungu, ambaye ndiye aliyetuamuru tuimarishe mahusiano ya kifamilia na ya ndugu na jamaa. Kwa upande mwingine, watu hao wanaomzingatia Mwenyezi Mungu katika kila jambo lao, huyakumbuka pia mazito na matokeo machungu ya ulimwengu mwingine; na kwa sababu wanajua kuwa, kukata uhusiano mtu na jamaa zake ni dhambi kubwa itakayomweka mbali na rehma za Mwenyezi Mungu, huwa wanaihofu adhabu ya dhambi hiyo. Lakini pamoja na kuwepo sifa zote hizi chanya, familia bora ya Kiislamu haiwezi kusalimika kikamilifu na matukio ya misukosuko na madhara.
Kwa hivyo inapokumbwa na misukosuko na matukio ya aina hiyo, sifa nyingine bora inayokuwa nayo familia hiyo ni subira na uvumilivu katika hali zote za maisha. Subira hiyo ni katika kutii amri za Mwenyezi Mungu; kujizuia na kujiweka mbali na maasi; kustahamili masaibu ya kimaumbile, matatizo ya kimaisha na vilevile kuwa wavumilivu na thabiti katika medani za jihadi na kupambana na adui. Na subira zote hizo zinakuwa na faida na thamani, pale zinapokuwa na msukumo wa sababu moja tu, nayo ni kutaka kupata radhi za Mwenyezi Mungu. Na ndivyo sehemu ya mwanzo ya aya ya 22 ya Suratu-Ra’ad inavyosema: “Na ambao husubiri kwa kutaka radhi ya Mola wao Mlezi…”
Jambo lenye taathira kubwa zaidi ya kuifanya subira itawale ndani ya taasisi ya familia ni kusimamisha Sala kunakoifanya nafsi ya mtu iwe muda wote inamkumbuka na kumdhukuru Mwenyezi Mungu; na sambamba na hilo, ni watu wa familia kuwa na moyo wa utoaji kwa siri na kwa dhahiri kwa kila neema waliyojaaliwa na Mola ili kuwasaidia wanyonge na wahitaji; ambapo kwa kufanya hivyo mawasiliano na mafungamano na Mwenyezi Mungu na vilevile na waja wake, yatakuwa yametawala muda wote katika maisha yao ya kifamilia. Sehemu inayofuatia ya aya ya 22 ya Suratu-Ra’ad inalizungumzia hilo kwa kusema: “na wakashika Sala, na wakatoa, kwa siri na kwa uwazi, katika tulivyo wapa…”
Nukta na sifa nyingine muhimu yenye kutoa mchango mkubwa wa kuimarisha familia ni watu wake kuwa na mwenendo wa kulipa mema kwa mabaya wanayotendewa. Sifa hii chanya na zingine tulizotangulia kuzitaja zina taathira kubwa kwa familia bora ya Kiislamu, kama inavyomalizia kueleza sehemu ya mwisho ya aya ya 22 ya Suratu-Ra’ad ya kwamba: “na wakayaondoa maovu kwa wema. Hao ndio watakao pata malipo ya Nyumba ya Akhera.”
Baadhi ya wataalamu wa masuala ya Qur’ani wameitolea ufafanuzi sehemu hii ya mwisho ya aya hii ya Suratu-Ra’ad kwa kusema: “familia bora ya Kiislamu, si tu itakuwa na maisha maridhawa na tulivu katika dunia hii, lakini matunda na taathira yake watakwenda kuishuhudia pia watu wake katika ulimwengu wa milele kwa kupewa hadhi na daraja maalumu”. Na kwa maelezo hayo mpendwa msikilizaji niseme pia kuwa, sehemu ya 27 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu imefikia tamati. Hivyo sina budi kukuaga hadi wakati mwingine inshallah, tutakapokutana tena katika sehemu ya 28 ya kipindi hiki. Namuomba Mola wa haki akubariki; na amani, rehma na baraka zake ziendelee kuwa juu yako…/