Jumapili, Juni 12, 2016
Leo ni Jumapili tarehe sita Ramadhani mwaka 1437 Hijria sawa na tarehe 12 Juni 2016 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 974 iliyopita, alifariki dunia mjini Tabriz, moja ya miji ya kaskazini magharibi mwa Iran Hamzah Bin Abdul-Aziz Dailami, maarufu kwa jina la Sallar, mmoja wa wataalamu wa sheria za Kiislamu katika karne ya tano Hijiria. Allamah Sallar alikuwa mkazi wa mji wa Tabarestan, kaskazini mwa Iran huku lakabu yake ikiwa ni Abu Ali. Aidha Abu Ali alikuwa mmoja wa wanafunzi mashuhuri wa Sheikh Mufid na Sayyid Murtadha Alamul-Huda. Miongoni mwa athari kubwa za msomi huyo ni kitabu alichokipa jina la 'Al-Maraasimul-Alawiyyah wal-Ahkaamun-Nabawiyyah' 'Jawaamiul-Fiqhi' 'Al-Abwaabu wal Fusuul' na 'At-Taqriib.'
Siku kama ya leo miaka 974 iliyopita alifariki dunia Abu Yaala Jaafari, mmoja wa wasomi wakubwa wa karne ya tano Hijiria. Abu Yaala alikuwa mtaalamu wa elimu ya theolojia na sheria za Kiislamu huku akiwa naibu wa Sheikh Mufid enzi zake. Aidha msomi huyo aliishi kipindi kimoja na Sheikh Tusi, mmoja wa maulama wakubwa wa Kiislamu huku akijishughulisha na ufundishaji pia. Vitabu vya 'Milad Swahibuz-Zaman' na 'Takmilat' ni miongoni mwa athari mashuhuri za msomi huyo.
Siku kama ya leo miaka 476 iliyopita inayosadifiana na tarehe 12 Juni 1540, Uhispania iliikalia kwa mabavu ardhi ya Chile iliyoko magharibi mwa Amerika ya Latini. Kabla ya hapo, Wahindi Wekundu wa Chile walizima shambulio la Uhispania iliyotaka kuivamia na kuidhibiti nchini hiyo. Mara baada ya Uhispania kuidhibiti Chile, mapambano ya Wahindi Wekundu yaliendelea katika kukabiliana na wakoloni hadi ulipofika mwaka 1817, ambapo Jose de San Martin Kamanda wa Kiajentina aliwashambulia wakoloni wa Kihispania huko Amerika ya Kusini, na kuandaliwa mazingira ya kujipatia uhuru nchi hiyo mwaka 1818.
Na siku kama ya leo miaka 377 iliyopita, ulianza uasi wa kihistoria uliofahamika kwa jina la Mwamko wa Pekupeku katika jimbo la Normandy, nchini Ufaransa. Uasi huo ambao ulifahamika katika historia ya nchi hiyo kwa jina la Vanupié, ulisababishwa na malalamiko ya jamii kubwa ya watu masikini nchini humo dhidi ya Mfalme Louis XIII na Cardinal Richelieu, aliyekuwa Kansela wa mfalme huyo. Harakati hizo za mwamko kama zilivyokuwa harakati nyingine, zilishuhudia mauaji makubwa na utiwaji mbaroni wa idadi kubwa ya watu.
Na Siku kama ya leo miaka 102 iliyopita inayosadifiana na tarehe 12 Juni 1914, kwa mara ya kwanza kabisa yalifanyika majaribio ya kutumia nishati ya joto la jua pambizoni mwa Cairo mji mkuu wa Misri. Mbunifu na mtekelezaji wa mpango huo, alikuwa mwanafizikia wa Kijerumani, ambaye aliweza kukusanya miale ya jua, na kufanikiwa kuwasha mashine ya mvuke yenye kutumia 'horse power' 50.