Nov 09, 2022 07:58 UTC
  • Akhlaqi Katika Uislamu (29)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yako mpendwa msikilizaji popote pale ulipo wakati huu. Nakukaribisha kusikiliza sehemu hii ya 29 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu nikiwa na matumaini kuwa, mimi pamoja na wewe tutanufaika na yale tutakayoyasikia katika kipindi hiki ambacho kwa leo kitazungumzia umuhimu wa kuchungwa haki za mke na mume katika ndoa na familia. Endelea kuwa nami basi hadi tamati ya mazungumzo yetu.

Mpendwa msikilizaji, katika mfumo wa sheria wa Uislamu, kama kuna kitu kinachotiliwa mkazo na kujionyesha kwa uwazi zaidi ni kuzingatiwa na kuchungwa haki za baina ya pande mbili. Mfano wake ni haki baina ya Mwenyezi Mungu na mwandamu, waumini na Mitume, Umma na Imamu wao, viongozi na raia, mhadhiri wa chuo kikuu na mwanachuo, mwalimu na mwanafunzi n.k. Katika muelekeo huohuo, kuna haki za baina ya pande mbili za mke na mume katika taasisi ya ndoa na familia, ambazo nazo pia zimetiliwa mkazo na kupewa uzito mkubwa katika utamaduni wa sheria za Uislamu.

Kitu muhimu zaidi kinachotoa msukumo wa kuheshimiwa haki hizo na kupatikana hakikisho la utekelezaji wake ndani ya taasisi ya kipekee ya familia ni uoni na mtazamo ambao inapasa uwepo kuhusiana na hadhi yenye thamani kubwa waliyonayo mwanamke na mwanamme. Katika Uislamu, ukiondoa tofauti kadhaa zilizopo kati ya mwanamke na mwanamme, ambazo zimetokana na irada yenye hekima maalumu ya Mwenyezi Mungu katika uumbaji wa wawili hao, kwa mtazamo wa kuwa kwao binadamu, wawili hao wana hadhi sawa na za pamoja; na wanaweza kutoa mchango katika nyuga zote za maisha yao. Ili kuliweka wazi zaidi suala hilo, tuisome kwa pamoja tarjumi ya aya ya 97 ya Suratu-Nahl ambayo inasema: "Mwenye kutenda mema, mwanamume au mwanamke, naye akawa ni Muumini, tutamhuisha maisha mema; na tutawapa ujira wao kwa bora ya waliyo kuwa wakiyatenda." Kwa mujibu wa aya hii, Mwenyezi Mungu Mtukufu ameitaja imani na amali njema kuwa ndicho kipimo cha mtu kujaaliwa kuwa na maisha safi na mema na kulipwa malipo mema huko akhera. Na hakuna tofauti wala upendeleo wowote kwa mwanamke na mwanamme juu ya suala hilo. Na katika kuweka wazi zaidi na kutobakisha hata chembe ya utata, kwamba mwanamke na mwanamme watakuwa na malipo sawa kwake Yeye kwa amali yoyote njema watakayofanya, Muumba wa ulimwengu anasisitiza kama ifuatavyo katika sehemu ya aya ya 195 ya Suratu Aal Imran: …”Hakika sipotezi (malipo ya) amali ya mfanyaji yeyote miongoni mwenu, akiwa mwanamume au mwanamke.”

Ukiachilia mbali tofauti za kimaumbile zilizopo baina ya mwanamke na mwanamme, endapo mtazamo huu ndio utakaotawala katika anga ya maisha ya ndoa na familia, hakuna shaka kuwa mfungamano na mshikamano madhubuti usioweza kuyumbishwa utakuwepo baina ya mke na mume; na wote wawili watashirikiana bega kwa bega kuchangia masuala yao yote ya binafsi na ya kijamii. Kwa hakika Qur'ani tukufu imeibainisha kwa sura ya kuvutia kabisa hali hiyo ya kushirikiana na kuwa bega kwa bega wawili hao, kama isemavyo aya ya 35 ya Suratul-Ahzab ya kwamba: "Hakika Waislamu wanaume na Waislamu wanawake, na Waumini wanaume na Waumini wanawake, na wat'iifu wanaume na wat'iifu wanawake, na wasemao kweli wanaume na wanawake, na wanao subiri wanaume na wanawake, na wanyenyekevu wanaume na wanawake, na watoao sadaka wanaume na wanawake, na wanao funga wanaume na wanawake, na wanao jihifadhi tupu zao wanaume na wanawake, na wanao mdhukuru Mwenyezi Mungu kwa wingi wanaume na wanawake, Mwenyezi Mungu amewaandalia msamaha na ujira mkubwa."

Mbali na aya hii kubainisha sifa jumuishi na za ukamilifu za Waislamu wanaume na wanawake walio waumini wa kweli, inatupilia mbali pia aina zote za upendeleo wa kidhulma na udunishaji na hisia za ubinafsi na za taasubi za kujikweza na kujifanya bora zaidi wanaume; iwe ni katika zama za ujahilia wa mwanzoni mwa Uislamu au za ujahilia mamboleo wa zama hizi zilizopo baina ya makabila na mataifa na zilizochangiwa na dini za kikoloni na zilizopotoshwa mafundisho yake ya asili, ambazo zinawanyima wanawake haki zao kutokana na fikra potofu na visingizio hewa na visivyo na msingi. Fikra na mitazamo hii inapingana na mfumo wa haki na sheria wa kiuadilifu wa dini tukufu ya Uislamu ambao umeainisha kuwepo haki za pande mbili katika kila hali baina ya mke na mume.

Miongoni mwa matokeo haribifu ya kuangalia mambo kwa jicho la upande mmoja tu wa mfumodume ni kuendelea kutawala ndani ya nafsi za wanaume hulka ya ubwana wa kijahilia na ya kiburi, inayowapa fursa ya kuwabebesha wanawake matakwa yao yasio na mantiki yoyote. Hali ya kuwa, endapo wanaume na wanawake watajua kwamba kuna haki kwa pande zote mbili baina yao na wakazichunga na kutekelezeana, hapo ndipo utamaduni wa kuheshimiana na kuenziana utatawala, na kufutilia mbali kila aina ya udunishaji na udhalilishaji na hisia za kujikweza kwa lengo la kudhulumiana. Katika aya ya 13 ya Suratul-Hujuraat, Qur'ani tukufu inapinga na kufuta kila ya aina ya upendeleo na kujikweza kusio na msingi, kunakotokana na taasubi na ukereketwa wa kibubusa inaposema: "Enyi watu! Hakika Sisi tumekuumbeni kutokana na mwanamume mmoja na mwanamke mmoja. Na tumekujaalieni kuwa ni mataifa na makabila ili mjuane. Hakika aliye mtukufu zaidi kati yenu kwa Mwenyezi Mungu ni huyo aliye mchamngu zaidi katika nyinyi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye khabari."

Taathira nyingine chanya ya mtazamo huu wa kitauhidi na kiutu ni kujenga utamaduni wa umoja na kuwa kitu kimoja ndani ya taasisi ya familia, kufuta dhana ya mimi na asiyekuwa mimi baina ya mume na mke na kupatikana umoja katika fikra na matendo baina ya wawili hao. Lakini mbali ya hayo, wakati linapofanyiwa kazi suala la haki kwa pande zote mbili; na utamaduni na desturi ya kuenziana na kuheshimiana ikachukua nafasi ya tabia na mtazamo wa kudharauliana, athari yake ambayo ni ya msingi, hushuhudiwa pia katika adabu za uzungumzaji na mwenendo wa mke na mume. Kila hali hiyo inapostawi zaidi ndani ya ndoa husaidia kuimarisha na kuidumisha taasisi hiyo; na kinyume chake, ikiwa hulka ya kujikweza na kujipa ubwana itatawala baina ya mke na mume, matokeo yake yatakuwa ni kukoseana adabu ndani ya familia katika maneno na vitendo, watu kuacha kuheshimiana, kuvukiana mipaka na kuvunjiana heshima. Mafungamano ya kidhahiri na ya ndani ya nafsi hulegalega; na baada ya muda ndoa huvunjika na familia kusambaratika. Hivi ndivyo inavyokuwa! Wakati mwingine, neno moja tu chafu lisilofaa kusemwa, au kitendo kimoja tu kibaya kisichofaa kufanywa, huiumiza na kuitesa roho na akili ya mtu, kikayafuta mahaba na mapenzi baina ya mke na mume na kuibua chuki na uadui kati yao. Kwa hiyo kuchunga haki za pande mbili katika nyuga na nyanja zote, hususan ndani ya taasisi ya ndoa na familia ni msingi wa kimantiki na wa hekima unaopewa uzito mkubwa katika mfumo wa sheria wa Uislamu; na una uwezo wa kudhamini kwa hali zote kudumu kwa taasisi hiyo muhimu zaidi na ya msingi katika maisha ya wanadamu. Na kwa maelezo hayo mpendwa msikilizaji niseme pia kwamba sehemu ya 29 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu imefikia tamati. Hivyo sina budi kukuaga hadi wakati mwingine inshallah, tutakapokutana tena katika sehemu ya 30 ya kipindi hiki. Namuomba Mola wa haki akubariki; na amani, rehma na baraka zake ziendelee kuwa juu yako…/